MAHAKAMA
ya wilaya ya Rungwe juzi ilijikuta inasitisha kwa dakika kadhaa
kusikiliza kesi baada ya mkazi wa kaya ya Masukuru wilayani hapa
aliyefahamika kwa jina la Tiger Mwaigomole (70) kufariki dunia ghafla
akiwa ndani ya chnumba cha mahakama wakati mashitaka yakiendelea.
Mwaigomole
alianguka ghafla mahakamani hapo na kufariki dunia alipokuwa akiendelea
kufuatilia kesi ya kupigana na kujeruhi inayomkabili mtoto wake
anayefahamika kwa jina la Gwakisa Tiger(40) iliyokuwa ikiendelea
mahakamani hapo.
Tukio
hilo ambalo ni nadra sana kutokea,lilitokea majira ya saa 9 alasiri
ndani ya Mahakama hiyo ambapo marehemu alifika mahakamani hapo akiwa na
mwanaye aliyejulikana kwa jina la Lusajo Tiger wakiwa na lengo la
kumwekea dhamana Gwakisa Tiger ambaye alifikishwa mahakamani hapo
akituhumiwa kwa kosa la kupigana na kujeruhi katika ugomvi uliotokea
kijijini kwao.
Kwa
mujibu wa Lusajo wakati kesi ikiendelea mbele ya hakimu wa mahakama
hiyo Omary Kingwele, ndugu yao alipandishwa kizimbani kusomewa mashtaka
yanayomkabili ndipo marehemu alipoanza kutetemeka kwa madai kuwa
anajisikia baridi kali sana.
Alisema
kutokana na marehemu kulalamikia baridi aliamua kumnunulia chai ya moto
ili anywe na kupunguza baridi ambapo baada ya kufanya hivyo marehemu
alikata roho muda mfupi baada ya kumaliza kunywa chai aliyokuwa
amepelekewa huku akiwa amekaa ndani ya chumba cha mahakama hiyo.
Kutokana
na tukio hilo askari polisi waliokuwepo mahakamani hapo waliuchukua
mwili wa marehemu na kuukimbiza katika Hospitali ya Wilaya ya Rungwe
Makandana kwa ajili ya vipimo lakini hata hivyo mwili ulikabidhiwa kwa
ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi ingawa ripoti ya kifo chake
haikutolewa mapema.
Wakati
huo huo hukumu ya kesi ya mauaji dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Rungwe na pia mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)
wilaya hiyo, John Mwankenja inayowakabili Hakimu Mwakalinga na wenzie
watatu huenda ikatolewa kesho(Oktoba 29).
Uhakika
wa kufika kwa ukomo wa shitaka hilo unatokana na mahakama kuu kanda ya
Mbeya chini ya Jaji Samwel Karua kumaliza kusikiliza ushahidi wa upande
wa mashtaka pamoja na utetezi kwa upande wa washitakiwa wote.
Mwishoni
mwa wiki jana Jaji Karua alisema baada ya kumaliza kusikiliza pande
zote mbili atatumia muda wa siku mbili kwa ajili ya kuandika hukumu
ambayo anatarajiwa kuitoa jumanne hii kesi ambayo inasimamiwa na
Mwanasheria wa Serikali Archiles Mulisa wakati washitakiwa wanatetewa na
mawakili wa kujitegemea Victor Mkumbe na Simon Mwakolo.
0 comments:
Post a Comment