Mshambuliaji wa Yanga na
timu ya Taifa (Taifa Stars), Mrisho Ngassa ameamua kulipa mwenyewe deni
lake la Sh45 milioni anazotakiwa kuilipa klabu ya Simba baada ya
kuhukumiwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF).
Awali Ngassa alikuwa
ameweka ‘ngumu’ kulipa fedha hizo na kuzua tafrani kwa mashabiki na
wanachama wa Yanga kuhusiana na adhabu yake ya kulipa fidia iliyotolewa
na Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi ya Wachezaji ya TFF.
Kamati hiyo ilimfungia
Ngassa kucheza mechi sita, adhabu ambayo amekwisha itumikia na
kilichobakia sasa ni kulipa fedha hizo ili aweze kucheza mechi za Ligi
Kuu ya Tanzania Bara.
Pamoja na Ngassa
kuonyesha juhudi kubwa mazoezini, sakata la ulipaji wa fedha hizo
lilizua tafrani nyingine huku uongozi ukitaka kulipa fedha hizo, lakini
kwa masharti ya kuongeza mkataba mwingine.
Hali hiyo ilizua maswali
mengi kutokana na ukweli kuwa muda wa kuingia mkataba kwa mujibu wa
taratibu za TFF ulikuwa umekwisha na suala hilo lingeweza kufanikiwa
wakati wa dirisha dogo la usajili.
Baada ya kukaa kimya cha
muda mrefu, Ngassa ameamua kutangaza waziwazi kuwa atalipa fedha hizo
alizochukua kutoka Simba na faini ambayo Kamati ya Sheria, Maadili na
Hadhi ya Wachezaji iliyoamua. Kamati hiyo ilimtaka Ngassa kulipa fidia
ya asilimia 50 ya fedha Sh30 milioni alizochukua kutoka Simba.
Ngassa alisema kuwa
ameamua kutoa fedha hizo kutoka katika vitega uchumi vyake na amefanya
hivyo kwa sababu suala hilo linamhusu yeye huku klabu yake ya Yanga
ikiadhibiwa pasipo sababu.
“Nina magari na biashara
zangu, nitalipa fedha hizo na nitarejea Jumamosi kucheza mechi yangu ya
kwanza ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting, mpira ni
kazi yangu na hili nimelifanya kutokana na mapenzi yangu ya dhati na
Yanga,” alisema Ngassa.
Alisema kuwa hajisikii
vizuri kukaa nje ya uwanja huku akiamini kuwa kipaji chake kinapotea.
“Nimekaa nje, sikuwa na raha, sasa narejea kwa nguvu zote ili kuendeleza
gurudumu la Yanga, mawazo yangu ya kucheza nje ya nchi kwa sasa
nimeyafuta na hasa baada ya kupata ushauri kutoka kwa marafiki zangu,
nawaomba radhi mashabiki na wanachama wa Yanga,” alisema Ngassa.
0 comments:
Post a Comment