Ninaigeuza nyuma, nakutana na kitu kingine kinachoyavuta macho yangu, nakunifanya niyakodoe pima kama fundi saa, aliepoteza nati. Ninajikaza kiume ili nisipoteze fahamu kwani akili imezidiwa na mawazo ya vitu ninavyokutana navyo. Sijawahi katika maisha yangu yote,kuona ndani ya chakula nawekewa picha! Ndiyo picha tena ya mtu alieniingiza katika ulimwengu wa mahaba, ambao hakika ni mpya kwangu pamoja na Matentelee yangu yote. Baby Girl atabakia kuwa ni fundi kwangu asie na mpinzani, katika kuogelea bahari ya mahaba. Mwanamtama ni Profesa wa mapenzi..
Picha niionayo ni ya kwake, najiuliza nani ameiweka katika chakula hiki?! Nikiwa bado ninastaajabu kuwekewa picha, nyuma ya picha hiyo kumeandikwa maneno, yanayonitatiza zaidi ya sana.
Dobe Boy, uwa la roho yangu nilipo ninakuwaza. Miss you sana, nimeyamiss Matentelee yako, njoo nilipo nikusabilie vyote!
Maneno hayo yameandikwa nyuma ya picha kipande ya Baby Girl Mwanamtama, au naweza mwitwa Nyakanga wa Manyakanga.
Akili inaniduru kwa kuwa mwisho wa maneno hayo, kumeandikwa tarehe ya siku ya leo! Yaani maana yake ujumbe huu umeandikwa leo hii hii! Japokuwa siujui mwandiko wa Mwanamtama, lakini sipati uelewa kama haya niyasomayo yameandikwa naye. Nafsi yangu inakataa kwa vile Baby Girl ameshakufa! Angewezaje kuandika ujumbe nae ni maiti? Angewezaje kupika chakula hiki ilihali mwili wake alipo, hawezi hata kumpangusa sisimizi anaemtambaa?!
Haya, anaponambia niende alipo akanisabilie vyote, nende kaburini au alikuwa na maana nife tukakutane huko Ahera?!!! Mmmmh sidhani! Hapo ndipo mawazo, akili, na fikra zinaposhindwa kufanya kazi zao sawasawa.
Najaribu kuhisi labda kuna mtu upande wa marehemu, ameamua kunichezea picha hiyo nichanganyikiwe. Ninajiuliza kwa nini afanye hivyo! Kisha iweje? Chakula kinanitumbukia nyongo, ladha yake inanipotea, nakiona kama mauzauza tu hivi.
Nimebung’aa tu kama mwehu, akili imesimama kwa muda. Mara mlio wa simu unanirudisha tena katika ufahamu wangu. Ninashangaa kwani mie sina simu nilipo, hii inayolia ni ya nani? Nageuka upande simu inapolilia ninavuta hatua hadi kitandani kwangu, ninaufata mlio unapotokea. Ninauinua mto, hatimae ninaiona simu ya kisasa aina ya Verssed Platnum Android ikiendelea kuita, nami ninabaki kuikodolea macho.
Najiuliza na kujipa majibu labda huyo alieleta chakula atakuwa ameisahau simu yake!
Mara simu inakatika kwa kutokupokelewa. Moyo wangu unakataa mawazo kuwa alieleta chakula, ameisahau simu yake kwa sababu imewekwa sehemu kwa kukusudiwa bila shaka. Ingelikuwa kusahauliwa ingekuwa sehemu yakuonekana kirahisi, lakini siyo chini ya mto, tena mto wa pili badala ya uliokuwa mbele, lazima kuna kitu hapa.
Ninapeleka mkono wangu ilipo simu, ninaiinua ninaishika. Nikiwa najiandaa kuibonyeza niione namba iliyokuwa inapiga, simu ikaanza kuita tena. Ninaitazama namba naiona ni ngeni machoni mwangu. Ninajiuliza mara mbili niipokee au nisiipokee?
Nikiwa katika kujiuliza, moyo nao unaongeza mapigo lakini unanisukuma niipokee. Ila inanitahadharisha niwe kimya nisiseme hata “Halow.”
Kwa mkono wenye kitetemeshi ninaipokea na kuiweka sikioni mwangu bila kusema neno. Upande wa pili nao unakaa kimya,nadhani unasubiri sauti yangu! Ninakaa hivyo kwa dakika mbili hakuna neno kwangu wala kwa mpigaji, ninaamua kuikata. Mara ninasikia mlio wa gari likisimama nje ya nyumba. Nikahisi mwenye simu sasa amefata simu yake. Haraka nikairejesha ilipokuwa kisha nikaubwaga chini upande wa khanga niliojistiri nao, nikavuta suruali yangu ya jinzi nikaivaa na kuwa tayari kwa lolote litalojiri nipambane nalo.
Sekunde zilikatika, dakika zikaenda lakini sikusikia mlango wa gari ukifunguliwa kisha kufungwa. Nikapata shauku nitoke nje kuitazama.
Ninapiga hatua moja tu simu inaita tena upyaa.
Nikawa kati sijui nende nje kutazama gari, au nibakie ndani nipokee simu. Nikaona nende nje haraka ikiwa anaeipiga yupo nje ninaweza kumuona nikamtambua.
Haraka ninavuta fulana iliyokuwa katika msumari wa mlango, ninaitupia kwa haraka mwilini huku ninatembea.
Nikiwa nje ninaishuhudia gari ndogo aina ya IST yenye vioo vya kiza, ikiwa mlango wa abiria upo wazi.
Ninashangaa kwani sehemu mlango ulipokuwa wazi, hakukuwa na mtu. Najiuliza kwa nini asiufunge alipotoka? Ninaisogelea gari kwa karibu kwa kupitia mlango uliokuwa wazi ninaweza kuona ndani ya gari hiyo kukiwa patupu hamna mtu ndani.
Eboo nini maana yake?
Ninajisemea kimoyomoyo, hatimae ninaamua kurudi ndani, ninajipa moyo labda dereva kaamua kutokea kwa abiria pengine mlango wake umegoma kufunguka, na kwamba atakuwa ameenda dukani. Mara wazo linanijia ghafla kuwa maduka hapa yapo mawili na yote ninaweza kuyaona nikiwa barazani. Ninageuka kwa haraka na kuyatazama maduka hayo ninaona katika duka moja, watoto wadogo wawili bila shaka wananunua pipi. Katika duka la pili kulikuwa hakuna mtu. Watu walikuwa wakipita na hamsini zao hakuna aliekuwa anashughulika na mie.
Nikakata shauri niingie ndani. Ninaona lazima nifanye kitu, tena nifanye haraka.
Ninaingia ndani na kuelekea moja kwa moja kwenye nguo zangu, ninaanza kufungasha niondoke mahala hapa nitokomee mbele kwa mbele. Ninafungasha vitu vyangu, lakini kabla sijesha kufunga simu inaita tena. Ninaamua niipokee kisha nimtukane mitusi nende zangu.
“Halow.”
Ninasema kwa hasira, huku nikijiandaa kuteremsha kamusi ya matusi, lakini masikio yangu, yanapoisikia sauti ya upande wa pili, yanatahayari. Mdomo wangu unapata kigugumizi, maneno yananikauka kinywani, nabaki kuwa msikilizaji.
Sauti hii, sitaki kukubali, hapana siyo!
Ninajisemea moyoni peke yangu. Nguvu zinanisha, ninashindwa kuendelea kusimama nakaa kitako kitandani. Machozi yananitoka sina habari, na sijui kwa nini yananitoka.
Nikiwa katika mawazo, bado simuni mawimbi ya sauti ya upande wa pili, yanarindima masikioni mwangu. Upande wa pili unaendelea kuzungumza kwa utuo na ufasaha wa hali ya juu. Mzungumzaji anajua anachokifanya. Hatimae ninatanabahi ninajibu swali ninaloulizwa simuni.
“Ndiye mwenyewe Dobe Boy, hujakosea hata kidogo”
“Amini nikwambiayo na fata maelekezo niliyokupa, haraka usishangae!”
Busu mwanana ninapigwa na simu inakatwa.
Ninaendelea kuishikilia simu sikioni kwangu, japo haiongei, nazama kwenye lindi la fikira hatimae, ninaisikia katika mawazo sauti ikinambia taratibu.
Amini nikwambiayo na fata maelekezo niliyokupa, haraka usishangae.
“My God!”
Ninatamka maneno hayo kisha ninaiweka simu mfukoni mwangu, ninakurupuka mbio.
Ninafika barazani ninaingia ndani ya gari IST, ninaufunga mlango wa abiria, kisha ninatazama kupitia vioo vya pembeni na cha ndani ya gari, kama kuna mtu anaenifatilia, sioni mtu kila kitu kipo sawa.
Ninainama chini ya kiti cha dereva, kama maelekezo niliyopewa katika simu, ninauona ufunguo ya gari. Ninauchukua na kuiwasha gari, ninatia gia naingia barabarani, naitafuta Ubungo.
********
Naegesha gari katika maegesho ya Hoteli Sharom nyuma ya kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani.
Ninashuka nakwenda mapokezi, ninamkuta muhudumu wa mapokezi, akizungumza na simu.
“Nikusaidie kaka yangu tafadhali.”
Ananambia huku ananitazama usoni, kisha anaikata simu aliyokuwa akizungumza nayo.
“Naitwa Dobe boy.”
“Ahaa sawa, ninazo taarifa za ujio wako, chukua lifti panda gorofa ya tatu, ukishuka kwenye lifti tu chumba unachokitazama ndicho kinakuhusu.”
Majibu hayo ya muhudumu ninataka kuhoji vitu, lakini ninaona siyo sehemu yake, kwa vile wahaka umenijaa, ninaamua kuingia kwenye korido ninaufungua mlango wa kioo, ili nende kwenye lift, kabla sijamaliza kuufunga mlango, ninalisikia jina langu likitajwa nyuma yangu.
“Dobe Boy, ndani ya nyumba.”
Ninageuka nyuma ninamuona muhudumu akiongea na simu ya mezani.
Ninahisi labda anamfahamisha mwenyeji ujio wangu. Sijali wala sirudi nyuma. Nasonga mbele ninaufungua mlango, kisha ninauachia mlango ujifunge nyuma yangu. ninaziendea lifti, ninaibonyeza ili ifunguke, Lifti ipo chini nilipo haifanyi khiyana inafunguka milango yake ninajichoma ndani.
Ninaibonyeza namba tatu, kuiruhusu lifti ili ikifika ghorofa hiyo isimame, chombo kinainuka juu, hadi ghorofa ya tatu, kinasimama milango inafunguka ninatoka nje ninatizamana ana kwa ana na mlango wa chumba ninachotakiwa kuingia.
Mapigo ya moyo, yanaongezeka kasi yake. Ninashusha pumzi ndefu. Ninaukabili mlango wa chumba, ninagonga kwa adabu.
Simu mfukoni mwangu, inaanza kuita. Ninaitoa na kuitazama namba inayopiga, ninaiona ni hii, hii inayofanya niwe pahala hapa muda huu.
“Halow, nimeshafika.”
“Najua, nimekuona tangu unaegesha gari. Hapo chini ya maegesho”
“Sawa nifungulie, mlango kwani hii milango inafunguliwa na Kadi, nami sinayo.”
“Natambua Dobe, ndani ya dakika sifuri utafunguliwa huo mlango.”
Simu inakatwa ninabaki namaswali yasiyojibika. Nitafunguliwa mlango, ina maana siyo yeye anifungulie?
Nikiwa bado natafakari, mara lifti inafunguliwa na dada mmoja amevaa sare mithili ya yule alienipokea mapokezi. Anatoka ndani yake, akiwa na Kadi mkononi. Ananisalimu kisha anaionesha ile Kadi katika mlango upande wa kulia, mlio mdogo ninausikia kuonesha kuwa Kadi imesomwa.
Anaushika mlango anaufungua, lakini haingii ndani. Ila ananikabidhi Kadi, ananiashiria nipite ndani.
Ninaingia chumbani, ninapokelewa na harufu nzuri ya uturi.
Ninaufunga mlango, nakielekea kitanda lakini ninapofika kitandani, ninasita kidogo. Ninasita kwa sababu kuna kitu kimenifanya nisite. Hakuna katika hoteli zote Duniani zinazoweza, kufanyika kitu hiki. Au niseme katika kutembea kwangu, sijawahi kukutana navyo.
Ninatupa macho huku na kule. chumba ninakiona kitupu hamna mtu.
Macho yangu ninayarejesha, kwenye kitanda, ninatizama nakujikuta ninasoma kimoyomoyo.
WELCOME AGAIN DOBE BOY
Maandishi hayo yameandikwa kwa herufi kubwa,
kwa Mashada ya asumini juu ya kitanda.
Chumba kipo tulivu, shuka na mazingira yapo safi. Nikiwa katika kushangaa, ninasikia mlio wa mlango wa kioo ndani ya chumba unafunguliwa.
Ni mlango wa sehemu ya kupungia hewa, ambayo ipo nje ikiwa imeachanishwa kwa aluminium na kioo kikubwa ndani ya chumba hicho. lakini kwa uzito wa mapazia, siyo rahisi kutambua kama kuna mlango. Ninakuwa makini zaidi kuona nani anaeingia, mara ninauona mguu wake ukiingia ndani, mara nusu ya mwili wake unaonekana, hatimae wote ninamuona ameingia.
Ninapotazamana nae, nashindwa kuamini macho yangu. Moyo wangu ninauhisi kushindwa kufanya kazi sawasawa. Miguu inanisha nguvu, kitete kinanipata, fahamu nazo ninazihisi kwa mbali zikinitupa mkono. Kizunguzungu kimenivamba, macho yanitanda kiza, siwezi kutazama sawasawa, ninajihisi kuupiga mweleka wa chali. Kwa mbali sana ninahisi mikono laini ikinidaka, lakini siwezi kusikia anachokiongea, ninapoteza fahamu.
DOBE KAPATA AU KAPATWA?!
MAJIBU YAKE KESHO KATIKA MUDA WAKE, USIKOSE MDAU.
Ludewa yetu na maendeleo yetu posted by barnabas njenjema, kutoka Ludewa
0 comments:
Post a Comment