fence-hayangaUkuta wa uzio wa kiwanja cha Lulu Saccoss ukionekana kujengwa kwa kuziba barabara ya Mtaa wa Hayanga ambao unalalamikiwa na wananchi.
WAKAZI wa Mtaa wa Hayanga Kata ya Ilomba jijini Mbeya wamemuomba Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuwasaidia kutatua mgogoro wao na Chama cha Akiba na Mikopo cha Lulu (Lulu Saccoss) kutokana na Jiji kushindwa kutoa msaada.
Wakizungumza na www.mbeyayetu.co.tz, Wakazi hao wanailalamikia Lulu Saccoss kwa kujenga uzio uliopelekea kuziba barabara ya Mtaa na kuwaletea usumbufu watumiaji wengine wa barabara hiyo kutokana na kushindwa kupita na pikipiki pamoja na magari.
Aidha wamesema kutokana na kuzibwa kwa barabara hiyo imepelekea kushindwa kupata msaada wa haraka kutoka kwenye vikosi vya uokoaji kama kutatokea janga lolote kama vile Moto.
Akizungumza kwa niaba ya wenzie,Geofrey Mackenzi,Veronica Mlowe na Juma Legembo,  Mkazi wa Hayanga anayepakana na eneo lililojengwa na Lulu Saccoss,Lena Anyandwile Kila alisema wamelazimika kutoa kilio chao kwa Waandishi wa habari ili Waziri asikie kutokana na kukosa majibu ya kueleweka kutoka kwenye Uongozi wa Jiji la Mbeya ambao pia umepuuza maagizo ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla.
Killa alisema mgogoro huo ulianza wiki tatu zilizopita ambapo Lulu saccoss wamejenga uzio katika kiwanja namba 15 Block c na kuziba barabara ya Mtaa tofauti na ramani ambayo inaonesha sehemu hiyo kuwa inapaswa kuwa na barabara kwa ajili ya magari.
Alisema suala hilo waliripoti kwenye uongozi wa Mtaa, Kata na Jiji mara baada ya kuwaona mafundi wa Lulu saccosi wakichimba msingi wa kuanza Ujenzi huku wakiwa wamepitiliza kwenye mipaka yao na kuziba barabara ya Mtaa lakini wakashangaa hakuna hatua zilizochukuliwa hadi ukuta umekamilika.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Hayanga, Esther Mizeck alipoulizwa kuhusiana na mgogoro huo alikiri kuufahamu na kuongeza kuwa alipata taarifa kutoka kwa majirani wakilalamikia kufungwa kwa njia na ndipo alipoanza kufuatilia kujua kinachoendelea.
Mizeck alisema alifanikiwa kufika eneo la tukio na kuwakuta mafundi wakiendelea na ujenzi lakini alipowauliza kuhusu kibali mafundi hao walijibu kuwa kipo kwa viongozi wa Lulu ndipo alipotoa hati ya kusimamisha ujenzi lakini mafundi walikaidi hadi alipotishia kuita jeshi la Polisi.
Alisema baada ya kuwasimamisha akashangaa kesho asubuhi ukuta umejengwa bila kibali na ndipo alipowasiliana na uongozi wa Lulu ambao walimpelekea nakala ya kibali kikiwa kimetolewa Septemba 30,2015 chenye namba 1832 kwa ajili ya ujenzi wa ukuta kikiwa kimetolewa na Mhandisi wa Jiji la Mbeya.
Alisema ili Jiji litoe kibali cha ujenzi ni lazima muombaji aanzie ofisi ya Mtendaji wa Mtaa ambaye hutoa barua kwa mwombaji ili apelike Jiji wampatie kibali lakini Kwa Lulu haikufanyika hivyo kwa kile alichodai kwenye Faili hakuna nakala ya barua ya kuruhusu kupewa kibali cha ujenzi huo.
Aliongeza kuwa taarifa alizonazo ni kwamba Lulu wanahaki ya Uwanja huo kwa muda mrefu lakini wanapaswa kuacha eneo kwa ajili ya njia ili huduma muhimu ziweze kupatikana ikiwemo wenye magari kuweza kupita na kwamba wakati wa upimaji Jiji hawakushirikisha majirani.
Naye Mwenyekiti wa Lulu Saccoss, Vitus Lubulle,alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo aligoma kuongelea na kudai kuwa wanaopaswa kuzungumza Ofisi ya Mipango miji ambao walienda kupima kwani wao hawahusiki na chochote.
Kwa upande wake Afisa ardhi wa Jiji la Mbeya, Patrick Mwakilili, alipoulizwa kuhusiana mgogoro huo alisema ni kweli Lulu wameziba barabara na walipofuatilia waligundua kuwa kuna tatizo kubwa na kuamua kumzuia Lulu asiendelee na ujenzi wowote hadi tatizo litatuliwe.
“Tumegundua kuwa kuna tatizo Mtaa mzima na Lulu tulimzuia asiendelee na Ujenzi lakini hivi sasa ratiba zimetubana nadhani wiki ijayo tutaweza kulifanyia kazi ili kutatua mgogoro huo” alisema Mwakilili.