Mwenyekiti wa Baraza ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mbangala Ibrahim Sambila akihutubia Baraza
Mkuu wa Wilaya ya Songwe Jeremiah Samwel akihutubia Baraza la Madiwani Wilaya ya Songwe

Baraza la Madiwani Wilaya ya Songwe Mkoa wa Songwe limeazimia kuwafikisha mahakamani wanafunzi wanaopewa mimba kutokana na kushindwa kutoa ushirikiano pindi wanapotakiwa kutoa ushahidi mahakamani kwa sababu za ujauzito. Azimio hilo limefikiwa katika kikao cha kwanza cha Baraza hilo kilichoyanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Bomani kikao kilichohudhuriwa pia na mkuu wa Wilaya ya Songwe Jeremiah Samwel. Wakiongea kwa uchungu Madiwani walisikitishwa na kitendo cha wanafunzi kushindwa kuwabainisha wahalifu kwa kutaja jina moja tu au wakidai waliowapa mimba walikutana nao mnadani hivyo kesi kukosa ushahidi. Aidha mazungumzo yanayofanywa na pande mbili nje ya Mahakama yamekuwa yakikwamisha kesi hizo kutokana na makubaliano ya kuoana hivyo kupelekea wanafunzi na wahalifu kutotokea mahakamani. Matukio mbalimbali yaliyoripotiwa Polisi yamekuwa yakikosa ushahidi kutokana na mahudhurio hafifu Polisi na Mahamani. Mwenyekiti wa Baraza ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mbangala Ibrahim Sambila amesema hayupo tayari kuona watoto wanakatishwa masomo kwa mimba hivyo hatua ya wanafunzi kufikishwa mahakamani kuwasaidia kukomesha vitendo hivyo. Pia Sambila amekerwa na baadhi ya wazazi kushindwa kuwapeleka watoto bweni bila sababu za msingi hali inayosababisha kuongezeka kwa mimba katika Halmashauri ya Songwe. Baadhi ya madiwani wamekerwa na wazazi wa Galula kutokana na wazazi hao kushindwa kuwapeleka watoto bweni kwani licha ya kukamilika kwa mabweni shule ya sekondari ya Galula ni wanafunzi 28 tu ndiyo wanaoishi bweni. Mpaka sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kutokana na kuwapa mimba wanafunzi ambapo tatizo hilo limeonekana kuwa kubwa Wilaya ya Songwe na kuongezeka kwa mimba za utotoni  na kuwakosesha watoto wa kike haki ya kupata elimu.
Na Ezekiel  Kamanga