Na.Chikoti Cico.
Siku 35 baada ya David Luiz Moreira Marinho kuumia kwenye mchezo wa nusu fainali ya FA cup kati ya Chelsea vs Tottenham Hotspur, beki huyo anaingia uwanjani tena kucheza mchezo wa fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich huku akiwa bado haamini kama ataweza kucheza.
Baada ya mchezo huo na Chelsea kunyakua ubingwa haya ndiyo yalikuwa maneno ya Luiz “ Ijumaa nilifanyiwa vipimo vya mwisho kuona kama ntaweza kucheza fainali (Jumamosi) lakini hata wakati wa mchezo baada ya dakika 20 nilikuwa najiskia vibaya ila nilijiambia mwenyewe sitaacha maumivu yanisababishe nitoke”
“Nimekuwa nikicheza maisha yangu yote kwaajili ya kombe hili, hii ndiyo ndoto niliyokuwa nayo toka nikiwa mtoto kucheza kwenye mechi kama hii (fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya). Hivyo nilijiambia nitacheza kutumia moyo wangu, sikuhitaji kucheza kupitia mwili wangu wakati moyo wangu ulikuwa jasiri”
Huyo ndiye David Luiz ambaye amesajiliwa na klabu ya Chelsea kwa mara nyingine tena kwa pauni milioni 32 baada ya kuuzwa mwaka 2014 kwenda PSG kwa pauni milioni 50. Kurejea kwa Luiz klabuni hapo kumeleta maswali mbalimbali mengi yakionyesha wasiwasi juu ya beki huyo ambaye wakati flani Gary Neville aliwahi kusema anacheza kama vile “anachezeshwa kwenye “play station”.
Usajili wa Luiz kurejea Chelsea unaweza kuwa usajili wa muhimu chini ya kocha Antonio Conte pamoja na kwamba umekuja dakika za mwisho kabisa kabla dirisha la usajili halijafungwa hapo Agasti 31.
Kwanza kabisa Luiz haitaji muda wa kuzoea mazingira (adaptation) ya ligi ya primia na ndani ya klabu ya Chelsea tofauti na usajili kama wa beki Shkodran Mustafi kwenda Arsenal ama Erick Bailly wa Manchester United ambao wote hawa kwa namna moja ama nyingine watahitaji muda kuzoea ligi ya primia na mazingira ya klabu zao.
Pili Luiz anarejea Chelsea akiwa na miaka 29, umri ambao inategemewa kwamba tayari ameshakuwa na uzoefu wa kutosha kuweza kuondokana na makosa ambayo alikuwa akiyafanya kipindi akiwa klabuni hapo wakati huo akiwa na miaka kati ya 24-27. Ingawa bado atahitaji kukaa vyema na kocha Conte ili kuimarika zaidi katika mambo kama wakati gani wa kumkaba adui na wakati gani wa kukaba nafasi.
Tatu faida nyingine Luiz aliyonayo ni morali na upiganaji wake akiwa uwanjani, kucheza dakika 120 huku akiwa bado hajapona vizuri kwenye mchezo wa fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern unakuonesha namna ambavyo beki huyu huiweka timu mbele kuliko stahiki binafsi. Pamoja na makosa madogo madogo ambayo Luiz hufanya lakini bado ni beki ambaye unaweza kumwamini uwanjani.
Nne Luiz ni beki ambaye ana uwezo mkubwa wa kuutumia mpira miguuni (foot work) jambo ambalo litaweza kumsaidia kocha Antonio Conte kama akitaka kutumia mfumo “aupendao” wa mabeki wa tatu, mfumo ambao huitaji beki mwenye uwezo mzuri wa kupiga pasi kutokea eneo la nyuma.
Kwahiyo unaweza kuona namna ambavyo Luiz atakuwa na faida chini ya Conte ingawa bado atakuwa na changamoto kubwa ya kuonyesha kwanini amestahili kurejeshwa klabuni hapo na kwanini ilikuwa ni kosa kipindi cha mwaka 2014 kuuzwa.
Ludewa yetu na maendeleo yetu posted by barnabas njenjema, kutoka Ludewa
0 comments:
Post a Comment