MTO Ruaha Mkuu ni mto wa pili kwa kwa Urefu nchini Tanzania  ambao una urefu wa km 475, muonekano na uzuri wa mto huo huonekana vizuri sana katika uwanda wa Bonde la Usangu na katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha
Asili ya jina la Ruaha mkuu ninatokana na Lugha ya Kihehe yani RUVAHA yenye maana mto mkubwa na mto huo kwa wenyeji wa  bonge la Usangu (Wasangu) hufahamika kwajina la (MNYINAVANA) kwa maana ya mto mkubwa ni moja ya mito yenye kona na mzunguko wa wajabu sana  na pia humwaga maji kwa kiwango kikubwa  katika eneo chepechepe  la Ihefu (Ihefu Swamp) kabla ya kuunganika  na kuendelea.
Ukubwa wa mto Ruaha Mkuu ni Km za Mraba 83,970 na  muda mrefu mto huo umekuwa ukitumika kwajili ya shughuri za kilimo cha umwagiliaji,uvuvi na kunyweshea mifugo, matumizi ya wanyama wa porini katika eneo la hifadhi ya Taifa ya  Ruaha na pia mto huo umekuwa ukitumika kama chanzo cha umeme katika mabwawa ya Mtera  na Kidatu.
Chanzo cha Mto Ruaha mkuu ni safu za Milima ya Kipengere na huunganika na mito mbalimbali ikiwemo ya Lukosi, Yovi, Kitete, Sanje,Kimbi,Nyamalela, Ruaha-mdogo, Kisigo, Mbarali(Barali),Kimani na Chimala pamoja na mito modogo ya Umrobo, Mkoji, Lunwa, Mlomboji, Ipatagwa, Mambi na  Mswiswi na kuambaa  katika uwanda wa bonde la Usangu wilayani Mbarali Mkoani Mbeya.
Maajabu ya mto Ruaha Mkuu ni kuwa una aina 38 za  samaki wakiwemo Kitoga,kolokolo na kambale  na pia ni mazalia ya wanyama wakiwemo viboko, Mamba na kenge wakubwa,hata hivyo mto huo umekuwa ukiathiliwa na shughuri za kibinadamu  na mwanzoni mwa miaka ya 1990 hadi mwaka 1994  mto huo ulianza kukauka nyakati za kiangazi na kubakiza madibwi tu ingawa kumekuwa na jitihada za makusudi za kuhifadhi asili ya mto huo.

Na mto wa kwanza kwa urefu nchini Tanzania ni Mto Rufiji ambao ambao unakadiliwa kuwa na  urefu wa Km 600 na chanzo cha mto huo ni mito ya kilombero na Luwegu na umekuwa ukimwaga maji katika bahari ya hindi katika mkondo wa eneo la Kisiwa cha mafia.
muonekano wa Mto Ruaha mkuu katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha
Imeandaliwa na Ng’oko Innocent