MAANA YA UPENDO NA KUWA NA UPENDO


UPENDO unatofautiana kutoka moyo mmoja na mwingine, unaweza kuwa mzuri au mbaya. Kupenda na kupendwa ni viungo kamili vya furaha katika maisha, lakini inapotokea unampenda mtu asiyekupenda, hali hiyo itakuletea shida katika nafsi yako. Kwani kuwa ndani ya upendo ni sawa na tone la maji baada ya ukame wa miaka mingi.
Kijana Bright anasema kuwa, upendo hauchoshi, upendo ni mwema, hauna husuda, hauwazii mambo yako mwenyewe, hauna hasira ya haraka, hauhesabu makosa, upendo una nguvu kwa mambo yote yaliyofichika, una kuaminiana katika kila jambo, huamini yote na hauna mwisho.
Upendo hauelezeki tangu mwanadamu alipoumbwa, kwa hiyo tunatumia mioyo yetu na akili zetu katika maamuzi. Husababisha kupata hisia na msisimko katika mwili wako umwonapo mtu unayempenda. Katika upendo ni hali ya kawaida kuvutiwa kimaumbile na mwenzako awe mwanamke au mwanamume. Ni hali ya kawaida kwa kuwa suala la mahusiano linaanzia hapo. Upendo una heshima, hukufanya kumsaidia mtu katika hali zote za maisha yake, kumhifadhi kutoka kwa maadui, na kujua kuwa akili ya kila moja kati ya wapendanao ipo hapo kwa asilimia mia moja, kujisikia salama kwake, kujivuna unapokuwa naye, kushirikishana katika matarajio na ndoto za kila mmoja na mambo yote mazuri pamoja na kujihisi kama ni mshindi katika dunia.
Unapompenda rafiki yako hutasita kumwambia ukweli pale anapokosea. Pia kupatana naye pale mnapotofautiana. Ikitokea mmetofautiana kauli, mawazo au jambo lolote, ni vizuri kukaa pamoja na kuangalia chanzo cha tatizo ili muweze kutatua.
Mtu anayesema kuwa anawapenda wengine na kuwajali kuliko kujijali yeye mwenyewe, huo ni upendo. Unampenda mtu na kujaribu kumfanya awe na furaha, pia katika nafsi yako utakuwa na furaha. Upendo unaweza kuelezwa hivyo.
Kijana Julius anasema kuwa, anaamini upendo unaelezeka kwa njia nyingi na pia ana uhakika kuwa kuna aina mbalimbali za upendo unaouhisi kwa mtu. Inapotokea ukashindwa kula au kulala kutokana na mawazo unayomuazia mtu aliye maalumu kwako, ni hakika unakuwa na upendo halisi. Unapokaa kwenye kochi kwa ajili ya kupumzika wakati ukisoma kitabu au kitu kingine chochote na kuangalia chini, unaweza ukawa ukurasa wa kumi wa kitabu chako lakini kwa sababu akili yako inafikiri kuhusu mtu ambaye hujamwona ili kuondoa mawazo hayo unajikuta unarudia rudia kufungua kurasa mbalimbali za kitabu chako, au kama una miadi na huyo mtu unayemuwaza na kama mmeonana kwa mara ya kwanza, usiku huo tumbo lako litakuwa linakusumbua na ghafla utajikuta unaumwa kwa sababu ya hisia za upendo.
Julius anauelezea upendo kuwa ni ile hali ambayo huwezi kusubiri kumwona yule unayempenda kwa mara nyingine na kutafuta njia ya kuwasiliana naye, kama kuondoka nyumbani na kwenda kutafuta kibanda cha kupigia simu au kununua kadi ya simu ilimradi tu usikie sauti ya yule unayempenda kwa mara nyingine tena, na wakati mwingine mnapokuwa wote, unadiriki kumpa kitu chochote cha kula ili uendelee kuwa naye kwa dakika nyingine tano.
Unamwamini kwa moyo wako wote, una kuwa na uhuru naye ukiamini kuwa unaweza kuongea neno lolote mbele yake. Mnakuwepo pale kwa jambo lolote, bila kujali kama ni la kufurahisha au la huzuni. Jambo lingine ni kumshirikisha mambo muhimu ambayo siku moja unaamini itakuwa kumbukumbu ya kushangaza katika maisha yenu.
Kwa maelezo mengine upendo wa kweli ni pale mmoja anapomjali mwingine. Kumfanya mwenzako awe na furaha ni jambo la muhimu, upendo wa kweli unasimama katika usawa na ulinganifu katika jambo lolote linalohitaji uaminifu.
Upendo ni hisia, ambayo haiwezi kuelezeka. uhitaji uvumilivu. Ni mzuri. hauna husuda, haujivuni, haukosi adabu, hauchoki katika kufanya shughuli za kujitegemea. Hauna hasira, hauweki kumbukumbu mbaya. Upendo mara zote unahifadhi, unaamini, unatumaini. Mara zote upendo unahifadhi, unasema ukweli, unaamini na haushindwi.
Nini maana ya upendo na kuwa katika upendo? James anasema hafikirii kama yeyote anaweza kulijibu swali hilo. Bila shaka unaweza kuelezeka lakini kuuelezea vizuri ni vigumu kwa sababu upendo wa kila mmoja ni tofauti na wa mwingine. Upendo ni hisia ambao ni kwa watu wawili wanaohusika wanaelewa, na kama huelewi, yakupasa uendelee kusubiri. Usijaribu kutafuta maana ya kitu ambacho hukielewi. Upendo upo kila mahali, ni kitu kinachotafutwa na kueleweka, hakielezeki.
Kuna baadhi ya vitabu vinaeleza kuwa wasichana hawataki kuwa wajasiri tu, bali kuwa sehemu ya ujasiri huo ambao kwa wapendanao unakuwa na hisia za kuthaminiana. Wasichana wengi wanakuwa na mawazo mazuri ya kile wanachokitaka na inakuwa mara kwa mara.
Lakini inaonekana kwa nadharia kuwa upendo unawafanya wasichana wengi kukubali mabadiliko na mara nyingi wanakuwa imara kujifunza kwa mtu anayetaka kumwongoza, hali hii inakuwa tofauti kwa wanaume. Hali hii inawafanya kubadili kwa haraka tabia mbaya walizokuwa nazo awali na kuwa na uwezo mzuri wa kuishi na waume zao. Inafikiriwa kuwa wasichana wengi au wanawake wanakuwa na maisha ya kuvunjwa moyo kama hawajui njia yoyote, wanajikuta wanalazimika kutafuta njia ya kuwafanya waishi, kusimamia kila kitu katika maisha ya wapendanao, kwa mfano kwa mwanamume ambaye husababisha hali hiyo. Kwa hiyo wanakuwa wakarimu, wanajitoa ili kuwaridhisha wenzi wao, na kuonyesha uthamani wa upendo.
Lilly anasema anafanya kazi ya uuguzi, ambapo miaka yote ameona upendo umekuwa ukihitajika. Kwa mfano, amekuwa akifanya kazi nyumbani kwa mwanamke mwenye miaka 87, ambaye alikuwa haongei ila mara zote anatabasamu kwa kila mtu siku nzima anapokuwa pale. Mume wake, amekuwa mtu wa kelele, huenda mara chache kukaa naye na kwenda naye matembezi. Kutokana na kelele hizo si rahisi kwa mtu kukaa na mwanamke huyo, ila kutokana na upendo ndiyo maana yeye ameweza kukaa naye.
Wakati mwingine kwa wapendanao, busu moja linaondoa migongano iliyokuwepo baina yao. Inavunja kila kitu na kinyongo chochote ulichokuwa nacho, unajikuta katika dakika chache unasahau mahali ulipo, na wewe ni nani. Kwa dakika chache unajihisi vizuri kuliko ulivyowahi kusikia, migongano uliyokuwa nayo huisikii tena, wasiwasi unaoandoka. Kutokana na mguso mmoja wa hisia ulioupata kwenye kichwa chako, utajikuta imara, mwenye furaha kubwa na ya kudumu siku nzima.
Tukutane Alhamisi ijayo.



Ludewa yetu na maendeleo yetu posted by barnabas njenjema, kutoka Ludewa
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: