MTOTO AJIFUNGUA PACHA WAKE
Ama kwa hakika, ‘ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni.’ Huko Huaxi, nchini China, mtoto wa miaka miwili amefanyiwa upasuaji wa kutoa kifusi mwilini mwake. Hii ni baada ya madaktari kugundua kuwa kifusi hicho kilipaswa kuwa pacha wake aliyeshindwa kukua ipasavyo. Xiao Feng alipelekwa hospitali baada ya tumbo lake kuwa kubwa kiasi cha kuwa alijikuta akishindwa kupumua. Alipolazwa, madaktari walichukua picha za ‘X-ray’ na ‘MRI’ na kugundua kuwa Feng alikuwa amebeba mimba isiyokua na hivyo kuamua kumfanyia upasuaji. Walikiondoa kifusi hicho changa kilichokuwa na ukubwa wa inchi 10 na tayari kilikuwa kimeanza kuwa na uti wa mgongo na vidole. Mimba hiyo ilitakiwa kuwa pacha wa mtoto huyo (yaani mmoja alikulia tumboni mwa mwenzie). Pacha huyo wa sponji angekua na kuwa mtoto wa kiume. Mapacha wanaofanana hutokea pale yai linapojigawa wakati wa urutubishaji na mapacha walioungana hutokea pale yai linaposhindwa kujigawa kikamilifu. Kwa kesi ya Feng, baada urutubishaji, yai lilishindwa kujigawa na upande mmoja ukamezwa na upande wa pili.
MTOTO AMEZALIWA AKIWA NA MIKONO NA MIGUU MINNE MTOTO
wa kiume wa maajabu amezaliwa akiwa na mikono minne na miguu minne jambo ambalo liliwashangaza watu wengi pamoja na familia yake. Mtoto huyo kwa sasa anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji wa saa 3 katika hospitali ya Mulago nchini Uganda. Paul Mukisa alizaliwa Septemba mwaka huu na mwanamke aitwaye Margaret Awino mwenye umri wa miaka 28. Mama huyo baada ya kuona hali ya mtoto wake huyo kuwa ya kushangaza, alishirikiana na familia yake na kuamua kumkimbiza hospitali iliyo karibu na kijiji chao cha Nabigingo. Baada ya mtoto huyo hali kuendelea kubadilika, walimhamishia kwenye hospitali ya Mulago iliyopo Kampala kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Baada ya kufika hospitalini mtoto Paulo alifanyiwa upasuaji na kutolewa kiumbe kiingine kwenye mwili wake chenye miguu miwili na mikono miwili lakini hakina kichwa wala moyo. Iwapo kiumbe hiki hakingejiunganisha na mwili wa Paulo na kikue vizuri, kingekuwa pach wa Paulo. Dkt. Nasser Kakembo aliyeshiriki kwenye upasuaji huo, alikiambia kituo cha runinga cha CNN kwamba walitoa pia mbavu kutoka kwa kiumbe kilichoungana na mtoto huyo. “Tulitoa mbavu zake za kulia na kushoto zilizokuwa zimeungana, tulizuia damu na kuziba vidonda,” alisema Dkt. Nasser. Wataalam hao wa afya wanasema ni nadra sana mtoto kama huyo kuzaliwa ingawaje kuna uwezekano mkubwa wa kuzaliwa mtoto kama huyo. Ndiyo maajabu hayo ya dunia, kile ambacho hufikiri kutokea katika dunia hii huwa kinatokea katika hali yoyote muda wowote na mahali popote.
KIAZI CHAMEA NDANI YA KIZAZI
Ama kweli kua ujionee. Huko nchini Colombia, msichana mmoja mwenye umri wa miaka 22 aliwashangaza madaktari kutokana na kuwa na kiazi ambacho kilikuwa kikimea kila siku ndani ya kizazi chake. Mh! Ujana maji ya moto! Msichana huyo ambaye jina lake halikutajwa alikuwa anajaribu kukitumia kiaza hicho kama kifaa au njia mojawapo ya kuzuia mimba. Hali ilipoanza kubadilika, baada ya kulalamika kuhusu maumivu ya tumbo, aliamua kumuona daktari na baada ya uchunguzi aligunduliwa kuwa ana kiazi ambacho kilikuwa kimeota mizizi ambayo ilianza kumea ndani ya kizazi chake. Kulingana na gazeti la Nation nchini Kenya, msichana huyo amedai kuwa mamake alimshauri kwamba iwapo angependelea kuzuia mimba basi alifaa kuweka kiazi ndani ya kizazi chake. Licha ya hatari aliyokumbana nayo mwanamke huyo hakuathirika huku kiazi hicho kikitolewa bila kufanyiwa upasuaji.
MFAHAMU MTOTO MREFU DUNIANI
Ama kweli ya Mungu mengi. Huko nchini India msemo huu wa Waswahili ulidhihirika baada ya kuzaliwa mtoto mwenye uzito wa kilo saba na urefu wa zaidi ya futi mbili na kupewa jina la Karan Singh. Baba wa mtoto huyo mwenye umri wa miaka 35 alisema kuwa, “wakati anazaliwa, alikuwa na urefu na uzito usio wa kawaida. Tulifikiria kwamba huenda akawa ana matatizo fulani ya kiafya. Lakini madaktari walituambia kuwa ni mzima na mwenye afya tele.” “Urefu na uzito wake uliwashtua madaktari, hatimaye kuingizwa kwenye kitabu cha ‘Guinness Book of World Records’ ambapo anatambulika kama mtoto aliyezaliwa mrefu zaidi na uzito mkubwa zaidi duniani kwa watoto waliowahi kuzaliwa. Cha kushangaza ni kwamba kwa sasa Karan ana umri wa miaka mitano na urefu wa futi tano na inchi saba. Hii inamfanya kuwa mtoto mrefu zaidi duniani kwa watoto walio na umri wa miaka mitano. Babake Karan ana urefu wa futi sita na inchi saba huku mama yake Shweatlana Signh, wa umri wa miaka 26, ni mrefu zaidi kwa kuwa na urefu wa futi saba na inchi tatu. Kuna kipindi alitambulika kama mwanamke mrefu zaidi India na kuendelea kufahamika kuwa ni miongoni mwa wanawake warefu zaidi kusini mwa Asia. Baba yake Sanjay aliongeza kuwa, “Sisi ni familia ya watu warefu. Kama nikienda mahali fulani, najikuta kuwa ni mtu mrefu zaidi katika eneo hilo. Lakini ninaporejea nyumbani ninakuwa mfupi ukinilinganisha na mke wangu.” Naye Shweatlana alisema kuwa, “kila mwaka Karan anaongezeka futi moja na inchi tano kila mwaka.” Hii ni kutokana na kuzidi kwa homoni za ukuaji. Hata hivyo, mama yake alisema kuwa anapata wakati mgumu sana kwenye kutafuta mavazi ambayo yatamtosha.
Ludewa yetu na maendeleo yetu posted by barnabas njenjema, kutoka Ludewa
0 comments:
Post a Comment