Shule iliyozuia uvaaji wa Yebo yebo shuleni yaonesha matokeo mazuri kitaaluma



HALMASHAURI ya Wilaya ya Nkasi imeipongeza na kuahidi kuizawadia Sh 500,000 Shule ya Msingi Kilambo cha Mkolechi ya mwambao wa Ziwa Tanganyika, Kata ya Kala kwa kushika nafasi ya kwanza mkoani Rukwa katika matokeo ya Taifa ya kuhitimu Darasa la Nne uliofanyika 2015.
Hiyo ni shule ambayo wanafunzi wake wapatao 40 ambao mmoja wa mwalimu wa shule hiyo, aliwapiga marufuku wasivae shuleni hapo wala wasiingie darasani na viatu maarufu ‘yebo yebo’ ambapo viatu hivyo viliteketezwa na moto shuleni hapo.
Kwa mujibu wa matokeo mtihani wa Taifa wa Darasa la Nne yaliyotolewa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) 2015, inaonesha kuwa wanafunzi 33 wa Shule ya Kilambo cha Mkolechi walifanya mtihani huo ambapo kiwilaya shule hiyo iliibuka ya kwanza kati ya shule 97 zilizoko wilayani Nkasi.
Kadhalika, shule hiyo katika matokeo ya mtihani huo imeibuka ‘kidedea’ kwa kushika nafasi ya kwanza kimkoa kati ya shule 358 zilizoko mkoani Rukwa, ambapo kitaifa imeshika nafasi ya 1,250 kati ya shule 16,627 za msingi.
Akizungumza na gazeti hili, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi , Misana Kwangula alilishukuru gazeti hili kwa kuripoti taarifa vinginevyo kisa hicho kingesababisha mvutano kati ya wazazi na walimu wa shuleni hapo.
“Nikushukuru sana kwa hilo ulinisaidia sana … isitoshe tulimwagiza mwalimu huyo aliyehusika na mkasa huo (Baraka Mwakasege) ambaye aliwanunulia watoto hao wote ‘yebo yebo’ mpya kwa fedha zake mwenyewe. Cha kufurahisha zaidi Shule ya Msingi Kilambo cha Mkolechi imefanya vizuri sana katika mtihani wa Taifa wa kuhitimu Darasa la Nne ambapo kimkoa imeshika nafasi ya kwanza,” alieleza Kwangula.
Kwangula ambaye pia ni Ofisa Elimu Halmashauri ya Nkasi (Shule za Msingi) alikiri kufurahishwa kwake kwa shule hiyo kufanya vizuri katika mtihani wa Taifa wa kuhitimu Darasa la Nne ambapo halmashauri yake itaizawadia Sh 500,000.










Ludewa yetu na maendeleo yetu
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: