CUF yaijia juu China kuhusu Zanzibar



Siku moja baada ya Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing kusema kuwa nchi yake inaamini kuwa uchaguzi wa marudio uliofanyika Zanzibar hivi karibuni ulikuwa huru na haki, chama cha CUF kimejitokeza na kupinga kauli hiyo kikieleza ni ukandamizaji wa demokrasia.

Chama hicho kimeionya China kuacha siasa na kufumbia macho ukiukwaji wa demokrasia nchini kwa masilahi yao na kuitumia Tanzania kujinufaisha na rasilimali zilizopo bila kujali amani itakapovunjika hapo baadaye.

Juzi, Dk Youqing alipokuwa anazungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba alimhakikishia kuwa nchi yake itaendelea kutoa misaada kwa Tanzania hata baada ya Shirika la Marekani la Maendeleo ya Milenia (MCC) kusitisha misaada.

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Abdalah Mtolea alisema China inahalalisha uchaguzi wa marudio uliofanyika Zanzibar kwa sababu ya masilahi yao ya kiuchumi kwa taifa lao na raia wa China waliopo nchini.

“CUF tunaelewa kwamba kwa nchi yoyote inayofahamu demokrasia, uhuru na haki ni nini, hawezi kusema uchaguzi wa marudio Zanzibar ulikuwa huru na haki,” alisema.

Alisema chama kikongwe kinachotawala China CCP na CCM vimekuwa na uswahiba wa muda mrefu jambo linaloifanya nchi hiyo kutoaana mambo mbalimbali ya ukiukwaji wa demokrasia na haki za binadamu wakihofia kuharibu uhusiano wao.

Alisema Serikali ya Tanzania inapaswa kuwa makini na uhusiano na misaada inayotolewa na nchi hiyo ili kubaini  ina malengo gani yaliyofichika kwa Taifa letu.

Mtolea ambaye pia ni Mbunge wa Temeke alisema China imeamua kuunga mkono kukandamizwa kwa demokrasia nchini Tanzania ili kujikomba kwa Serikali ya CCM waendelee kupata hisani zaidi kwa masilahi ya taifa lao.

Alisema: “China inapata tenda kubwa za ujenzi nchini Tanzania mfano ujenzi wa barabara ambazo nyingine zishaanza kuharibika, madaraja na majengo makubwa nchini.

"Hata mradi wa kusafirisha gesi, kana kwamba hiyo haitoshi, kumekuwa na ongezeko la Wachina wakifanya biashara zinazofanywa na Watanzania huku wengine wakiishi nchini bila vibali."

Katika mazungumzo yake na Waziri Makamba, Balozi Youqing alisema China ina mipango mingi ya ushirikiano na Tanzania, ikiwamo kwenye sekta ya umeme na itaendelea kutoa ushirikiano kupitia kampuni zake.

Kwa upande wake, Makamba alimshukuru Balozi Youqing pamoja na Serikali ya China kwa ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili.

“Ujumbe na salamu ulizotoa leo umetupa faraja Watanzania. Urafiki baina ya nchi zetu, na baina ya vyama vyetu vya CCM na CCP, ni wa muda mrefu, ni wa majira yote na umejengwa kwenye misingi ya kuheshimiana na hauna budi kuendelezwa”, alisema Makamba.

Pia Waziri Makamba na Balozi Youqing walikubaliana kutembelea Pemba na Unguja kwa pamoja ili kukagua na kutengeneza miradi ya maendeleo kati ya China na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar


Ludewa yetu na maendeleo yetu
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: