Hivi Ndivyo Unavyoamua Kuharibu Maisha Yako Mwenyewe Bila Ya Kujua.


Tumekuwa tukipoteza maisha yetu sisi wenyewe, na mbaya zaidi hatujui hilo wakati tunafanya. Baadaye ndiyo tunakuja kujua kwamba tuliharibu maisha yetu wenyewe. Na kwa bahati mbaya siyo watu wote wanakuja kujua kwamba walipoteza maisha yao, na hata wakishajua wanakuwa hawana tena uwezo wa kubadili hali ya mambo.
Leo hii nataka tujadili kwa pamoja ili uweze kuchukua hatua mapema, kabla haujafika wakati ambao utasema kama ningejua. Utajua leo na kama utaendelea kufanya yale ambayo yanaharibu maisha yako basi unakuwa umechagua mwenyewe.
Kitu kikubwa sana ninachoamini ni kwamba kama unaweza kusoma hapa, na umesoma basi unayo nafasi kubwa sana ya kuweza kuyabadili maisha yako na kuyaboresha zaidi. Ni wewe uamue kuchukua hatua na usikubali kurudi nyuma.
Unaharibuje maisha yako wewe mwenyewe?
Ndiyo, wewe mwenyewe umekuwa ni mharibifu mkubwa sana wa maisha yako wewe mwenyewe. Na umekuwa unayaharibu maisha yako kwa kuyapoteza. Unajiuliza unapotezaje maisha yako? wacha nikupe kwanza mfano.
Je umewahi kufanya kitu ambacho hakina manufaa yoyote kwako lakini kitu hiko kinakuchukulia muda wako? Mtu alipokuuliza ulijibu nini? Mara nyingi umekuwa unajibu NAPOTEZA POTEZA MUDA HAPA. Sasa hili ndiyo jibu la jinsi gani unapoteza maisha yako.
Unapoteza maisha yako pale unapopoteza muda wako. Na hii ndiyo changamoto kubwa sana kwa kizazi chetu hiki, muda umekuwa adimu kuliko wakati mwingine wowote kuwahi kutokea hapa duniani. Na muda huu umekuwa adimu siyo kwa sababu masaa yamepunguzwa, bali kwa sababu mambo yameongezeka wakati muda ni ule ule.
Unapochagua kupoteza muda, umechagua kupoteza maisha yako. Na kwenye hili hakuna hata mmoja wetu ambaye anaweza kusema hajawahi kupoteza maisha yake. Tunachotofautiana ni kiasi tulichopoteza na ni wakati gani tulijua hilo na kuamua kuchukua hatua.
http://www.amkamtanzania.com/p/kuwa-tajiri.html 
Lakini pia muda umekuwa haupotei tu wenyewe, bali tunaupoteza kwa kuchagua kufanya vitu ambavyo havina thamani kubwa kwetu.
Na hapa ni vitu vitano ambavyo tunapenda kufanya lakini vinapoteza muda wetu na maisha yetu pia.
1. Kazi au biashara usiyoipenda.
Tafiti nyingi zilizofanywa maeneo ya kazi, karibu asilimia 80 ya watu hawapendi kazi wanazozifanya sasa. Unaelewa maana yake ni nini? Kwamba watu wengi waliopo kwenye kazi wamechagua kupoteza maisha yao, wao wenyewe bila ya kushurutishwa na mtu yeyote.
Kama unafanya kazi au biashara yoyote ambayo huipendi, labda kinachokuweka pale ni kipato unachopewa, unapoteza muda wako na maisha yako pia.
Subiri kidogo, najua hapa unaanza kupata hisia tofauti, kwamba iweje kazi inayokupa kipato cha kuendesha maisha yako ndiyo iwe kitu kinachopoteza maisha yako. Ninachotaka kukuambia ni kwamba kwa sasa unaweza usione hilo, lakini itakapofika wakati maisha yako yanaelekea ukingoni, ukitazama nyuma na kuangalia uliishije maisha yako, utaona giza nene, utaona ni jinsi gani maisha yako yalikuwa matupu. Kwa sababu ulilazimika kufanya kitu usichopenda ili tu upate fedha. Hutaona kitu kikubwa ambacho unajivunia kufanya kwenye maisha yako, kwa sababu kazi au biashara usiyopenda ni kama mzigo.
HATUA; hatua ya kuchukua hapa ni kufanya tathmini ya kazi au biashara yako. Jiulize je ni kweli hiko ndio kitu unachopenda kufanya? Je unaona unaongeza thamani kwenye maisha ya wengine kupitia unachofanya? Kama jibu ni ndiyo basi endelea. Kama jibu ni hapana anza kufanya mabadiliko, anza kutafuta kile unachopenda kufanya na kifanye, anza kwa hatua ndogo ndogo.
SOMA; Jambo Muhimu Kuzingatia Kabla Ya Kuwasaidia Wengine, Ili Msaada Wako Uwe Bora.
2. Mitandao ya kijamii.
Hakuna kitu ambacho kinatafuna muda wa watu wengi, na hasa vijana kama mitandao ya kijamii. Na kwa hapa Tanzania, mitandao miwili imekuwa ndiyo kinara. Facebook na Instagram. Mitandao hii imekuwa inawanasa watu kuiperuzi kila baada ya dakika chache, na wengine kushinda siku nzima kwenye mitandao hii.
Namitandao hii ya kijamii imekuwa kinara wa kupoteza maisha kwa njia tofauti, hapa nitazitaja zile kuu;
2.1 Kupoteza muda, hapa unapoteza muda ambao ungeutumia kwenye kazi zako muhimu kuperuzi mitandao hii.
2.2 Kujilinganisha na wengine. Mitandao hii imekuwa inachochea hali ya kujilinganisha na wengine. Kwa kuwa watu huchagua yale mambo mazuri tu na kuweka kwenye mitandao hii, unaweza kujiona wewe ndiyo huna maisha mazuri. Kwa njia hii unapoteza maisha yako kwa kukazana kujilinganisha na wengine.
2.3 Kukosa muda wa kuishi na kufurahia maisha. Mitandao hii ya kijamii imekuwa inatusukuma kufanya vitu siyo kwa sababu ni muhimu kwetu, ila tuweze kuwaonesha wengine kwamba na sisi tumo. Siku hizi hata vyakula siyo vitamu tena kula mpaka tupige picha na kuweka kwenye mitandao ya kijamii. Watu hawapo tayari kukaa na matatizo yao na kuyatafutia ufumbuzi, badala yake wanayaweka kwenye mitandao ya kijamii.
HATUA; hatua ya kuchukua hapa ni kutumia mitandao ya kijamii kwa akili sana. Hakikisha unatenga muda maalumu na mfupi sana, usizidi saa moja kwa siku kupitia mitandao yote ya kijamii uliyopo. Na kingine muhimu zaidi usikazane kuwa kwenye kila mtandao, kuwa kwenye ile mitandao ambayo ina mchango kwenye maisha yako. kama mtandao wa kijamii hauna mchango kwenye maisha yako basi jitoe.
3. Kufuatilia maisha ya wengine.
Huwezi kuwa unafuatilia maisha ya wengine, na wakati huo huo ukapata muda wa kuishi maisha yako, HAIWEZEKANI. Unapoanza kufuatilia huyu kafanya nini, huyo kaenda wapi na mengine mengi kuhusu wengine, ambayo siyo muhimu kwako, umechagua kupoteza maisha yako.
Na changamoto kubwa kwenye kufuatilia maisha ya watu ni kwamba unakuwa huna taarifa za kutosha, hivyo mara nyingi unatumia maneno ya kusikia. Wakati wenzako wako ‘BIZE’ kufanya maisha yao kuwa bora, wewe unakuwa bize kufuatilia ni kipi wanafanya au kipi hawafanyi. Na huu ndio msingi wa umbeya na majungu ambayo yamejaa kwenye maeneo ya kazi na hata kwenye mitaa tunayoishi.
HATUA; acha mara moja kufuatilia maisha ya wengine. Kuna mengi sana ambayo huwezi kuyajua kuhusu mtu, hivyo acha kujidanganya kwa taarifa chache za watu unazosikia kwa wengine. Weka nguvu kubwa kwenye kuboresha maisha yako, na utayafurahia.
4. Televisheni
Kama kuna kitu kingine kinachomaliza muda wako basi ni tv. Na tv haitofautiani sana na mitandao ya kijamii, kwa sababu kupitia tv unapoteza muda na pia unajilinganisha na wengine.
Ubaya mkubwa sana wa tv ni huu, unalipa gharama kuwaangalia watu ambao wanaishi maisha yao, huku wewe ukishindwa kuishi maisha yako. unapoangalia tv kumbuka kitu hiki kimoja, yule unayemwangalia kwenye tv analipwa, na wewe unayeangalia unalipa huku ukipoteza muda wako.
HATUA; kama unaangalia tv kwa zaidi ya saa moja kwa siku, unapoteza maisha yako, acha mara moja.
SOMA; Mambo Yanayokufanya Ukose Furaha Ya Kweli.
5. Kufuatilia habari.
Ufuatiliaji wa habari ni njia nyingine ya kupoteza muda wako na maisha yako pia. Tatizo la habari ni hili, habari nyingi ni hasi, nyingi ni za uongo au zimeongezwa chumvi na kwa sehemu kubwa sana hazikuhusu wewe.
Lakini utaniambia unataka kujua kila kinachoendelea, ili ujue dunia inaendaje. Na mimi nitakuambia hutajua dunia inaendaje kupitia habari. Bali utajua dunia inaendaje kwa kujifunza yale muhimu.
Sioni na kwa jinsi habari ya mtu aliyejinyonga huko Tabora inavyokusaidia wewe uliyepo dar, au arusha au moshi.
Kama kuna habari muhimu sana inayokuhusu wewe utaipata tu, bila hata ya kuwa mfuatiliaji mkubwa wa habari.
HATUA; epuka habari zote hasi, usipoteze muda wako kufuatilia habari ambazo siyo muhimu kwako.
Chagua sasa kuishi maisha yako rafiki yangu, usikubali tena kuyaharibu maisha yako kwa kufanya yale ambayo yanakupotezea wewe muda.
Nakutakia kila la kheri katika kuboresha maisha yako.

Ludewa yetu na maendeleo yetu
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: