Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Servacius Likwelile
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Servacius Likwelile amesema Jiji la Mwanza ni miongoni mwa miji yenye wakwepaji wengi wa kodi, huku akitoa mfano wa hoteli aliyolala kuwa, alilazimika kudai stakabadhi ya malipo kama deni.
Akizungumza na wafanyabiashara jijini Mwanza jana, Dk Likwelile alisema wafanyabiashara wengi ni wepesi kukwepa kodi, hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.
“Nimeligundua hili, hivyo nimeweka watu wangu kila sehemu walifuatilie kwa undani zaidi,” alisema.
Dk Likwelile alisema maendeleo ya nchi yanagharamiwa na Watanzania wenyewe na wafanyabiashara lazima walipe kodi kwa hiari ili kupunguza utegemezi wa wafadhili wa nje.
Alisema Serikali imefanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kupunguza misamaha mikubwa ya kodi kwa lengo la kutengeneza mazingira mazuri ya ulipaji bila vikwazo.
“Matokeo yake tumepanda kwa kiwango kikubwa katika makusanyo ya kodi, Desemba mwaka jana tulikusanya Sh1.592 trilioni, Januari tumekusanya Sh1.1 trilioni, wakati kipindi cha nyuma tulikuwa tukikusanya Sh850 bilioni utaona kwa kiwango gani watu wasivyolipa kodi,” alisema.
Aliongeza kuwa Serikali inalipa madeni takriban Sh350 hadi 450 bilioni kila mwezi ili kulinda heshima ya nchi na Sh535 bilioni kila za mishahara ya watumishi wa umma.
Baadhi ya wafanyabiashara walisema elimu ya mlipa kodi inahitajika badala ya kutumia vitisho, huku wakitaka kodi zinazolipwa na viongozi wa Serikali ziwe na uwiano na zinazolipwa na watu wengine.
“Kuna vitisho vingi vya kufungiwa biashara, lakini elimu ni nzuri kuliko kuvutana. Tuache mazoea, tupeane elimu vizuri inatosha kufikia malengo yetu,” alisema mfanyabiashara Abubakar Seif.
Tausi Ariri aliomba uwapo ushindanishwaji wa kukusanya kodi kila mkoa na ule utakaoongoza upewe kipaumbele cha kuendelezwa ili kuinua mwamko wa ukusanyaji.
“Uwapo uhusiano mzuri kati ya walipaji na wakusanyaji kodi, pia mipango na bajeti za mwaka tuwe tunashirikishwa hata sisi wafanyabiashara,” alisisitiza.
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment