Kura ya maoni yapingwa kila kona.



Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva.
Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva, kusema wanajiandaa kuanza mchakato wa kura ya maoni ya Katiba Mpya, wanasiasa na wadau wengine wamempinga wakisema anaingilia mamlaka ya Rais.
 
Jaji Lubuva alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na gazeti hili, huku kukiwa na kundi kubwa lililokuwa likimtaka Rais John Magufuli, kutoendela na kura ya maoni na badala yake, mchakato uanze na mambo yaliyokuwa kwenye Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, yaingizwe.
 
“Tulikuwa tunangoja tumalize uchaguzi, kama vile ambavyo Mnyamwezi anavyobeba mzigo, unamaliza mmoja unaenda mwingine, Sasa tumemaliza uchaguzi mkuu, tunaenda na kura ya maoni,” Alisema Lubuva alipozungumza na Nipashe.
 
APINGWA
Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu, alisema Jaji Lubuva anapaswa kutambua mipaka yake ya utendaji kazi. Alisema Lubuva aliwahi kutoa tamko la hali ya Zanzibar kuwa Rais Magufuli hana mamlaka ya kuingilia suala hilo.
 
Aliongeza kuwa Jaji Lubuva ni mwenyekiti wa NEC, hivyo mipaka yake ya uongozi inaishia katika masuala ya uchaguzi na kwamba hahusiki na uendeshaji wak ura ya maoni ya katiba. 
 
Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, alisema Jaji Lubuva aliwahi kueleza kuwa kura ya maoni haiwezi kufanyika bila kubadilisha sheria ya kura ya maoni kwa kuwa inahitajita kufanyika marekebisho.
 
Alipoulizwa endapo mchakato wa kura za maoni utaanza, alisema  upinzani wataendelea na mapambano kuikataa kwa kuwa mchakato huo utakuwa hauna uhalali wa Watanzania.
 
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Imelda Urio, alisema kulingana na sheria za mabadiliko ya katiba na kura za maoni, mchakato huo unatakiwa kuendeshwa kwa kuzingatia maoni ya wadau wote.
 
Alisema kilio na maoni ya wananchi waliyoyatoa yanatakiwa kuzingatiwa ili kutimiza lengo la katiba hiyo.
 
Alisema mchakato huo wa katiba unakabiliwa na changamoto kubwa ya wajumbe wake kutoka nje wakati wa kujadili namna ya kuipitisha hali ambayo tayari imeleta mkanganyiko.
 
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, alisema ni jambo la kushangaza upande mmoja wa serikali unatumbua jipu na upande mwingine unayaotesha.
 
Alisema katiba hiyo ina upungufu mwingi na kwamba serikali haiwezi kubadilika kama imeshindwa kufanya marekebisho katika upungufu ambao ulikuwa unapigiwa kelele na wadau.
 
Alisema jambo watakalolifanya ni kuomba kukutana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ili kuzungumza naye suala hilo.
 
Nao wanasheria na wanasiasa Zanzibar wamesema Katiba Mpya  inayosubiriwa kupigiwa kura ya maoni haina ubavu wa kumaliza kero za Muungano. 
 
Wamesema mfumo wa Muungano wa serikali mbili uliopitishwa na wajumbe Bunge Maalum la Katiba na kuandikwa kwenye  rasimu ya katiba hiyo ndiyo hauna uwezo wa kuondoa kero za Muungano zilizodumu kwa Zaidi ya miaka 50.
 
Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Omar Said Shaban, alisema katiba inayopendekezwa haikutokana na maoni ya wananchi kama walivyokuwa wamependekeza kupitia Tume ya Warioba. 
 
Alisema Wazanzibari wegi wanataka mfumo wa Muungano wa Serikali tatu ili kuondoa kero za Muungano lakini wabunge wa CCM wamelazimisha kubaki na muundo wa serikali mbili kwa kuangalia maslahi ya kisiasa.
 
Wakili wa Mahakama Kuu, Awadhi Ali Said, kwa upande wake alisema katiba inayopendekezwa iwapo itapitishwa, haitasaidia kubadili hali za watu wa Zanzibar bila kudai Muungano wa haki au kuvunja.
 
Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Zanzibar, Hamid Mbwezereni, alisema kabla ya kura ya maoni kufanyika ni muhimu wananchi wapatiwe elimu ya kutosha Tanzania Bara na Zanzibar.
 
Alisema kwa mtazamo wake katiba hiyo haitasadia kuondoa kero nyingi na kufungua fursa mbalimbali kwa Zanzibar ikiwamo za kukopa nje pamoja na mambo ya mafuta na gesi kuondolewa rasmi katika orodha ya mambo ya Muungano.
 
Mchakato wa Katiba Mpya uliingia dosari baada ya baadhi ya viongozi wa CCM, kupinga mfumo wa serikali tatu uliokuwa umependekezwa na Tume ya Jaji Warioba, iliyokusanya maoni nchi nzima na matokeo yake kuzaa kundi lililojiita Ukawa.
 
Mbali na muundo wa serikali tatu, baadhi ya mambo ambayo Ukawa walitaka yawe kwenye Katiba Mpya ni Mamlaka ya Rais kupunguzwa, Ushindi wa Rais uwe zaidi ya asilimia 50, Tume Huru ya Uchaguzi, matokeo ya rais kupingwa mahakamani, mgombea binafsi, mawaziri wasitokane na wabunge na muundo mpya wa Bunge la Muungano.
 
Oktoba 2, mwaka juzi, Bunge Maalumu chini ya aliyekuwa mwenyekiti wake, Samuel Sitta, lilipitisha Katiba inayopendekezwa na kuiwasilisha kwa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Oktoba 8, ili mchakato wa kura ya maoni uendelee.
 
Imeandaliwa na Gwamaka Alipipi, Mary Geofrey (Dar), Marco Maduhu (Mwanza), na Mwinyi Sadallah (Zanzibar)
CHANZO: NIPASHE



Ludewa yetu na maendeleo yetu
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: