KOCHA Mkuu wa Simba Jackson Mayanja ametenga silaha tatu muhimu za kuimaliza Yanga kuelekea kwenye mchezo baina ya timu hizo Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Achana na mkali wa mabao Hamisi Kiiza na Ibrahim Ajib, Mayanja ameamua kuwapa kazi maalumu mastraika Dany Lyanga, Hija Ugando na beki Hassan Ramadhani Kessy kutengeneza upacha wa kulishambulia lango la Yanga kama nyuki kwa muda wote wa dakika 90 za mchezo.
Simba ipo kambini mji Kasoro Bahari, Mkoani Morogoro ikijiwinda na mchezo ambapo kocha huyo ametamba kwamba Lyanga, Ugando na Kessy ameshawapa majukumu mazito ya namna kuitikisa ngome ya Yanga ili kuwapa urahisi wa kufunga Kiiza na Ajib.
Alisema, anaifahamu Yanga ni timu nzuri na anaiheshimu lakini atapambana kuhakikisha wanaendeleza rekodi yao ya ushindi katika mechi hiyo inayovuta hisia za mashabiki wengi.
"Yanga ni timu nzuri, tunawaheshimu kutokana na rekodi yao, lakini tunajiandaa kwa ajili ya mchezo huo, kwani dhamira yetu ni kuhakikisha tunapata ushindi ili kujiweka kwenye mazingira bora ya kuelekea kwenye ubingwa," alisema.
Mayanja alisema Yanga haimuumizi kichwa kwani aliwahi kukutana na kikosi cha timu hiyo kabla ya kukabidhiwa Simba, hali hiyo haimuumizi kichwa juu ya mechi yao.
“Yanga hainipi tabu kabisa niliwahi kuwafunga nikiwa na Kagera Sugar na kugawana pointi, hivyo kwa sasa sina wasiwasi na wachezaji wangu iwapo watayafanyia kazi maelekezo yangu,” alisema
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment