AZAM kukaa kileleni leo?
Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, amesema kuwa ushindi ni lazima katika mchezo wa leo wa Ligi Kuu Tanzania bara dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa leo kwenye dimba la Azam Complex Chamazi. Azam inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 32, inashuka dimbani kwenye mchezo huo ambao ni wa kiporo.
Iwapo itashinda mchezo huo, Azam itapaa kileleni na kuishusha Yanga yenye pointi 33, kwani wanarambaramba hao watakuwa wamefikisha pointi 35. Na iwapo watatoka sare, watakuwa na pointi sawa na Yanga, yaani 33.
Kwa upande wa Mtibwa inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 27, iwapo itashinda mchezo huo itafikisha pointi 30, huku ikiendelea kuwepo katika nafasi hiyo hiyo. Ushindi kwa kila timu ni muhimu ili kuwa katika mbio za kugombea taji la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania.
Akizungumza jana, Hall alisema mipango yao ni kushinda mchezo huo, huku akikiri kuwa utakuwa mgumu, lakini akidai wamejipanga kukabiliana na changamoto zote kutoka kwa wapinzani wao.
“Tumejipanga kushinda na lazima tufanye hivyo, tunataka kurejea namba moja kwenye msimamo, najua mchezo utakuwa mgumu kama ulivyokuwa kwa Kagera Sugar, lakini tumejipanga kwa changamoto zozote uwanjani,” alisema.
Hall aliongeza kuwa atawakosa wachezaji watatu walio majeruhi, ambao ni mabeki, Aggrey Morris na Erasto Nyoni aliyeumia nyama za juu ya paja katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar, mshambuliaji Ame Ally ‘Zungu’, huku pia beki David Mwantika naye akikosekana baada ya kufiwa na mdogo wake mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mara ya mwisho Azam kucheza na Mtibwa kwenye Uwanja huo, ilikuwa ni Februari mwaka huu walipoichapa mabao 5-2 na ziliporudiana Uwanja wa Manungu, zilitoka sare ya bao 1-1. Kwa upande wa Mtibwa, msemaji wake, Thobias Kifaru ameutabiria mchezo huo kuwa mgumu, lakini aki ahidi kuwa kikosi chake kimejipanga kushinda.
Wakati huo huo, Simba wanatarajia kuondoka leo kuwafuata Ndanda FC kwa ajili ya mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara. Akizungumza na waandishi wa habari jana, msemaji wa Simba, Haji Manara alisema kikosi hicho kina mategemeo ya kupata pointi tatu za ugenini.
“Baada ya maandalizi yetu tunategemea kwenda kutafuta ushindi katika mchezo huo na tukirudi tutaelekea moja kwa moja Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi,” alisema.
Wakati huo huo, Manara aliwatakia heri ya mwaka mpya wanachama wote wa Simba huku pia akisema kuwa Rais wa Klabu hiyo, Evans Aveva anatarajia kuzungumza na wazee wa timu hiyo Jumapili ya wiki hii makao makuu ya klabu hiyo.
“Lengo ni kubadilisha mawazo lakini kuzungumzia mpira. Ili tutoe matokeo mazuri wazee watakuwa na maoni yao, ushauri wao, tutapiga dua ya kuwakilisha mwaka mpya,” alisema Manara.
Klabu hiyo pia, ilizungumzia malalamiko yake juu ya waamuzi waliochezesha mchezo dhidi ya Mwadui FC mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo walilazimishwa sare ya bao 1-1 katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.
Alisema tayari wameiandikia barua Bodi ya Ligi kulalamikia uchezeshaji mbovu wa waamuzi hao ambao wanadai uliwagharimu.
Manara alisema malalamiko hayo yanamlenga mwamuzi wa kati na msaidizi namba mbili. Waamuzi waliochezesha siku hiyo ni Ngole Mwangole wa Mbeya, Joseph Masija wa Mwanza na Abdallah Rashid wa Pwani.
Alisema waamuzi hao waliwanyima penalti lakini pia walikataa nafasi mbili za mabao na kwamba ulalamikaji wao juu ya waamuzi hao sio kwamba wanahitaji pointi isipokuwa wanataka rekodi ikae sawa na waamuzi hao wasichezeshe tena mchezo dhidi ya Simba.
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment