SAMATTA: NINA MOTO WA HATARI, WAALGERIA LAZIMA WANIONGEZEE HESHIMA



MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amesema ana moto wa kufanya vizuri kumalizia mwaka ili ashinde Tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika.
Samatta ameingia kwenye orodha ya wachezaji 10 wanaowania Tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika mwaka 2015 na mwezi huu atakuwa na mechi tatu muhimu ambazo akifanya vizuri atajiweka katika mazingira mazuri ya kushinda.
Akizungumza na kwa simu jana kutoka Lubumbashi, Samatta amesema uteuzi huo ni heshima kwake na kwa taifa lake.
Mbwana Samatta ni tegemeo la Tanzania na TP Mazembe kwa sasa 

“Najisikia furaha sana kuingia kwenye 10 Bora hii ya Mchezaji Bora Anayecheza Afrika. Najisikia furaha kama binafsi na pia kwa taifa langu,”amesema mshambuliaji huyo wa TP Mazembe ya DRC.
Na Samatta aliyetua Mazembe akitokea Simba SC mwaka 2011 ameongeza; “Kwa kweli uteuzi huu unanifanya nikusudie kufanya kitu kikubwa ili nimalizie vizuri mwaka,”.
Mwishoni mwaka wiki, Samatta ataiongoza Mazembe katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya USM Alger Uwanja wa TP Mazembe mjini Lubumbashi.
Mchezo wa kwanza Jumamosi, Mazembe ilishinda 2-1 Algiers na Samatta ndiye aliyefunga bao la pili kwa penalti, baada ya yeye mwenyewe kuangushwa kwenye boksi kufuatia pasi ya Mtanzania mwenzake, Thomas Ulimwengu.
Baada ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Samatta atajiunga na kambi ya timu yake ya taifa, Taifa Stars kwa ajili ya michezo dhidi ya Algeria itakayochezwa Novemba 14 na 17 kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 Urusi, Tanzania wakianzia nyumbani.
Samatta aliifungia Mazembe bao la pili dhidi ya USM Alger Jumamosi katika ushindi wa 2-1

Katika orodha iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) juzi, Samatta ni kati ya wachezaji watatu wa TP Mazembe walioingia 10 Bora, wengine wakiwa ni kipa Robert Kidiaba Muteba wa DRC na kiungo Roger Assale wa Ivory Coast.
Watatu hao wanachuana na Abdeladim Khadrouf wa Morocco na Moghreb Tetouan, Baghdad Bounedjah wa Algeria na Etoile du Sahel, Felipe Ovono wa Equatorial Guinea na Orlando Pirates, Kermit Erasmus wa Afrika Kusini na Orlando Pirates, Mohamed Meftah wa Algeria na USM Alger, Mudather Eltaib Ibrahim ‘Karika’ wa Sudan na El Hilal na Zineddine Ferhat wa Algeria na USM Alger.
Katika orodha ya wachezaji wa 10 wanaowania tuzo ya jumla ya Mwanasoka Bora wa Afrika, Yaya Toure wa Ivory Coast na Manchester City ataitetea tuzo hiyo dhidi ya Andre Ayew wa Ghana na Swansea, Aymen Abdennour wa Tunisia na Valencia na Mudather Eltaib Ibrahim ‘Karika’ wa Sudan na El Hilal.
Wengine ni Mohamed Salah wa Misri na Roma, Pierre-Emerick Aubameyang wa Gabon na Borussia Dortmund, Sadio Mane wa Senegal na Southampton, Serge Aurier wa Ivory Coast na Paris Saint Germain, Sofiane Feghouli wa Algeria na Valencia na Yacine Brahimi wa Algeria na Porto.
Washindi watatokana na kura za makocha wa timu za taifa barani na Wakurugenzi wa Ufundi wa Vyama vya Soka vya nchi wanachama wa CAF.
Sherehe za tuzo zinatarajiwa kufanyika Alhamisi ya Januari 7 mwaka 2016 mjini Abuja, Nigeria


Ludewa yetu na maendeleo yetu
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: