Na Baraka Mbolembole
Mwaka 2009, mchezaji wa nafasi ya kiungo Haruna Moshi ‘ Boban’ alijiunga na klabu ya ligi kuu Sweden, Gefle IF. Haruna ni kati ya wachezaji wenye vipaji vya aina yake kutokea katika mpira wa miguu Tanzania katika kipindi cha miaka 15 hii ya ‘ Karne Mpya’.
Alianza kutamba akiwa Simba SC mwaka 2004. Msimu wake wa kwanza katika klabu hiyo ya Dar es Salaam ( 2003) ulifunikwa na vipaji kabambe kama, Suleimani Matola, Christopher Alex ( marehemu), Patrick Betwel, Primus Kasonso, Aman Mbarouk, Ulimboka Mwakingwe, Steven Mapunda, Yusuph Macho ‘Musso’ ambao waliaminiwa na kufanya vizuri katika nafasi ambazo kimsingi hucheza Haruna.
Akiwa ‘mvivu’ wa kukaba, Boban kwangu alikuwa ni namba 10 hasa. Aliweza kufunga ‘magoli ya video’ akiwa hata nje ya eneo la mita 18, akiwa upande wa kulia au ule wa kushoto. Popote pale, Boban angeweza kufunga goli zuri lisilotarajiwa. Mkenya, James Siang’a ambaye ni kocha wa kwanza kufanya kazi na Boban katika klabu ya Simba alimtumia zaidi kama kiungo wa pembeni.
Haruna alianza kupenya latika kikosi cha Simba akicheza kama wing wa kulia. Tofauti na Mapunda ambaye alicheza wing ya kizamani ambayo ilitegemea zaidi mfumo wa 4-4-2. Mapunda alikuwa na kasi, uwezo wa kukimbia na mpira na kupiga krosi ambazo nyingi zilifika kwa walengwa.
Alicheza zaidi pembeni ya uwanja, lakini Boban aliingiza stahili mpya ya kiungo wa pembeni. Wakati, Ulimboka alikuwa mbunifu katika wing ya kushoto kwa stahili yake ya kuichezesha timu kwa krosi fupi fupi, Boban akawa anaingia na mpira hadi katikati ya uwanja na kufanya Simba ionekane ikichezeshwa na viungo watatu.
Matola, Kasonso na Boban upande wangu ilikuwa safu ya kwanza ya kiungo ambayo nilishuhudia ikiitawala Yanga vile walivyotaka. Hata alipokuja, Mzambia, Patrick Phiri nafasi ya Boban iliendelea kuwepo kikosini. Ndani ya Simba alijijengea jina kutokana na uchezaji wake wa utulivu, kupiga pasi angavu, kufunga magoli ya kuvutia na pengine stahili yake ya uchezaji makini iliyoambatana na ubabe.
NIDHAMU IMEMUANGUSHA MAPEMA?
Boban ni kati ya wachezaji maarufu wenye tabia mbaya kiuchezaji. Alipata kadi nyekundu mara kadhaa akiwa klabuni Simba. Ni kati ya wachezaji nyota ambao nidhamu yao ya nje ya uwanja imewafanya washindwe kuichezea timu ya Taifa ( Taifa Stars) kwa kiwango cha kuridhisha.
Boban ni kati ya wachezaji maarufu wenye tabia mbaya kiuchezaji. Alipata kadi nyekundu mara kadhaa akiwa klabuni Simba. Ni kati ya wachezaji nyota ambao nidhamu yao ya nje ya uwanja imewafanya washindwe kuichezea timu ya Taifa ( Taifa Stars) kwa kiwango cha kuridhisha.
Amewahi kujibishana na makocha wa Stars, Marcio Maximo kiasi cha kumuacha nje ya Taifa Stars kwa mwaka mmoja( 2007-2008). Alipoomba radhi na kurudishwa kikosini,
Boban alichangia kwa kiasi kikubwa timu ya Taifa kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani, 2009 ( CHAN). Lakini alitimuliwa kikosi mara baada ya kumdharau, Maximo ambaye alimfanyia mabadiliko dakika chini ya 25 katika mchezo wa kwanza wa fainali hizo dhidi yb Senegal. Stars ilichapwa 1-0.
Hakuitwa tena timu ya Taifa hadi Charles Boniface Mkwassa na Jamhuri Kiwhelo ‘ Julio’ walipomjumuhisha katika kikosi cha Tanzania Bara ( Kilimanjaro Stars) kilichoshiriki kama wenyeji na kufanya vibaya katika michuano ya Cecafa Senior Challenge Cup, 2011.
Boban ambaye alicheza kwa kiwango cha chini katika mchezo dhidi ya Malawi alifanyiwa mabadiliko, na alipotoka tu uwanjani kaitupa chini jezi ya timu ya Taifa na kuondoka zake uwanjani. Si matukio hayo tu, Boban amewahi kuonekana akiwa na makopo mengi ya pombe katika mifuko ya jinsi yake aliyokuwa amevaa.
Alikuwa amelewa sana na aliingia uwanjani kuitazama Simba kama sijakosea katika mchezo wa kirafiki dhidi ya URA ya Uganda kabla ya kuanza kwa msimu wa 2008/09. Hakika nyuma ya kipaji hiki kuna matukio mengi ya utovu wa nidhamu ambayo yamepelekea kwa sasa kuwa katika klabu isiyo na malengo ya kutwaa ubingwa ( Mbeya City FC)
Ikumbukwe Simba ilimsaini Boban kutoka klabu ya Moro na aliichezea Simba kwa miaka 6 mfululizo kati ya 2003 hadi 2009, alipokwenda Uarabuni na kucheza kwa miezi mitatu kisha akaichezea Simba kwa muda mfupi na kujiunga na Gefle IF. Alicheza mechi Tano tu katika timu hiyo ya Sweden kisha akafanya vitendo vya utovu wa nidhamu kwa wachezaji wenzake na kulazimisha kurejea nyumbani Tanzania.
Watu wengi walimlaumu, Haruna baada ya kufanikiwa kulamisha kurudi nyumbani na kuicha timu hiyo ambayo kwa muda mfupi alitokea kukubalika sana kuanzia kwa benchi la ufundi, wachezaji hadi mashabiki wa timu yake. Aliwatemea mate Mate baadhi ya wachezaji wa kizungu mazoezini na kutoa lugha chafu.
Baadhi ya watu akiwemo, Damas Ndumbaro aliyekuwa wakala wake alinukuliwa akisema kuwa sababu kubwa ya Haruna kulazimisha kurejea nyumbani si kiwango kidogo cha mshahara kama alivyodai mchezaji huyo bali ni utovu wa nidhamu. Haruna alikuwa akilipwa zaidi ya milioni 4 za Kitanzania kwa mwezi baada ya kukatwa kodi. Kilikuwa ni kiwango kikubwa cha mshahara ambacho hakuna klabu ya Tanzania ilikuwa ikilipa wakati ule.
Mapenzi yake kwa Simba, na mapenzi ya mashabiki wa klabu hiyo kwa mchezaji huyo yalifanya mchezaji huyo kurejea Simba SC na kuichezea kwa misimu miwili na kushinda ubingwa wake wan ne wa ligi kuu msimu wa 2011/12. Baada ya mwenendo mbaya wa timu hiyo kuanzia mwanzo wa msimu wa 2012/13 uliambatana na maneno mengi kwamba baadhi ya wachezaji wanahusika kuifanya timu hiyo iingie katika kipindi kigumu.
Baada ya kushindwa kuelewana na aliyekuwa kocha mkuu, Milovan Curkovic, wengi walifikiri ujio wa Patrick Liewig ungerudisha kiwango cha mchezaji huyo. Lakini haraka, Liewig aliingia katika mzozo na baadhi ya waliokuwa wachezaji mastaa kama Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu huku Haruna pia akihusika. Sunzu na Mwinyi walimaliza tofauti zao na Liewig na kurudishwa kikosini lakini Haruna hakurejea tena hadi sasa.
Alijiunga na timu ya Coastal Union kwa ajili ya msimu wa 2013/14 lakini baada ya kuanza vizuri ndani ya timu hiyo, mwisho wake haukuwa wa kueleweka sana. Mara nyingi alikuwa akifanya mazoezi na wachezaji wa zamani pale uwanja wa Muhimbili wakati Coastal ikicheza mechi za ligi kuu. Baadaye ‘ Ukata’ ulitajwa sababu ya mchezaji huyo ‘ kuwasusa’ Coastal lakini taarifa za utovu wa nidhamu mara baaada ya Coastal kufungwa 4-0 na Azam FC zilitajwa pia.
Kwa nusu msimu wa 2014/15 aliichezea klabu ya daraja la kwanza ya Friends Rangers ya jijini, Dar es Salaam. Rangers ni timu ambayo ina mwalimu rafiki/ndugu/kaka kwa wachezaji wengi wenye majini nchini, Herry Mzozo. Pia ina wachezaji wengfi ‘ maswahiba’ wa Haruna kama Yusuph Mgwao, Amir Maftah, Credo Mwaipopo. Haruna alikuwa akicheza bure katika timu hiyo ili kuisaidia kuipandisha daraja la ligi kuu lakini timu haikupanda.
Wakati wa usajili wa kiangazi katikati ya mwaka huu, Haruna alisajiliwa na Mbeya City FC lakini alisafiri kwanza kwenda Qatar kujaribu bahati ya kucheza soka la kulipwa na baada ya kushindwa kwa kile kilichosemwa kuchelewa muda wa usajili, Haruna alijiunga na Mbeya City na amecheza gemu nne hadi sasa.
Akiwa na miaka 28 hivi sasa, Haruna si kipaji kilichopotea, Bali alijiuangusha mwenyewe kwa kushindwa kucheza ulaya kutokana na nidhamu yake mbaya. Aliichezea Tanzania mechi 24 kati ya mwaka 2007 hadi 2011. Alishinda VPL ( 2003, 2004, 2007, 2011/12) na mataji mengine ya Tusker Cup, Ngao ya Jamii. Je, anaweza kufufuka sasa akiwa Mbeya City FC? Ni jambo la kusubiri na kuona.
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment