JUZI Watanzania tulipata pigo la kumpoteza Mbunge wa Mbinga
Magharibi, Kapteni John Komba. Alikuwa ni msanii nyota na mwakilishi wa
watu wa Mbinga na kubwa alitetea maslahi ya Watanzania akiwa bungeni.
Taarifa za msiba huo zilienea kwa kasi kwenye mitandao hiyo na kufanya watu wengi kufikiwa na taarifa hizo za kuhuzunisha.
Pamoja na kupeana taarifa hizo za kusikitisha, baadhi ya watu ama kwa
ulimbukeni wa mitandao, ama kwa kutojali heshima ya marehemu, tangu
kupatikana kwa taarifa za kifo chake cha ghafla wamekuwa wakisambaza
picha ya mwili wa marehemu.
Huku katika mazingira ya kawaida ni kukosa maadili, kushindwa
kujiheshimu na pia kukosa ustaarabu wa kuheshimu na kusitiri binadamu
aliyeondoka duniani.
Picha hiyo iliyokuwa imetumwa kwenye makundi ya marafiki kwenye
mitandao ya kijamii, ilinifanya kuumia zaidi, kwani waliopata taarifa
hiyo iliyoambatana na mwili wa marehemu ukiwa umelala kwenye kitanda
katika hali ile sidhani kama walikuwa ni watu stahiki, sembuse kuwa na
uwezo wa kuiondoa akilini.
Ninavyoona haikuwa sahihi kuiweka picha ya marehemu, watoa taarifa
wangeweza hata kutumia picha ya kiongozi huyo akiwa kwenye moja ya
shughuli zake wakati wa uhai wake ambazo ziko nyingi kwenye mitandao
kuliko ile.
Tukio hilo lilinikumbusha matukio mengi na picha nyingi ambazo watu
wamekuwa wakizituma bila kujua kuwa zitaleta ukakasi kwa wale
wanaotumiwa, kama vile picha za ajali, au ile iliyomuonesha mwanamke
aliyeunguzwa na mumewe sehemu za siri au mtoto albino alivyocharangwa
mapanga na nyingine nyingi ambazo naamini hazifuati maadili katika
kupashana habari wala faragha ya mtu.
Ukiangalia kwa undani picha hizi za kiongozi wetu huyo, zinaonesha
kabisa kuwa zimepigwa na watu waliokuwapo karibu na marehemu wakati huo
na hawa pasi shaka ni wauguzi au madaktari au wahudumu, katika hali ya
kawaida hakuna ndugu ambaye atapigapicha kisha aiweke kwenye mitandao.
Jambo la kujiuliza kama waliofanya hivyo ni kati ya madaktari na
wauguzi, maadili ya kazi yao yako wapi. Wote tunajua kuwa siri ya
mgonjwa au marehemu anayefika katika hospitali zetu ziko kwenye mikono
ya watoa huduma hao, sasa iweje pia hiyo isambae kwenye mitandao? Hii
inasikitisha sana kwani huu ni uvunjaji wa maadili ya kazi yao.
Nakumbuka, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilianzisha kampeni
ya Futa Delete Kabisa ambayo kwa kiasi kikubwa imepunguza matumizi
mabaya ya mitandao ingawa bado kuna watu chache ambao bado wanafanya
hivyo.
Ikumbukwe kuwa maendeleo ya teknolojia yana manufaa makubwa kwa wale
wanaotaka kutumia kwa ajili ya manufaa na kupewa taarifa za kuwafanya
wapige hatua za maendeleo, lakini pia zina ubaya wake kwa watu ambao
hawataki kutumia kwa maendeleo.
Hao walioanza kutumia maendeleo ya mitandao kamwe huwezi kuona picha
na maiti zikiwa zinaoneshwa ovyo, mfano mzuri ni kifo cha Michael
Jackson, hakuna mtu anayeweza kutafuta hiyo pia, sasa kwa nini iwe
kwetu?
Kufanya hivyo ni dalili ya ulimbukeni wa watumiaji wa teknolojia hii.
Pamoja na jeshi la Polisi kuwa na jukumu la kupambana na wahalifu wa
mitandao, ikiwa ni pamoja na wanaotumiwa kusambaza taarifa za chuki,
kashfa kwa watu wengine na hata picha zinazokwenda kinyume na maadili ya
watanzania, kazi hii inatakiwa jamii nzima ishirikiane kutokomeza.
Jambo la kwanza kwa jamii ni kuhakikisha unawaambia washirika katika
makundi ya kijamii, kutotuma picha za ajabu, au taarifa zisizo za maana
au zenye kueneza chuki, pili tunaweza kukubaliana kuwaondoa wale
wanaokiuka maadili na tatu kutokuwa mmoja wa watu wanaosambaza vitu kama
hivyo.
Hivyo, Watanzania wakati umefika sasa, kushirikiana katika kukataa
hili la udhalilishaji na kuwa chombo cha kusambaza mambo yasiyo na
msingi, na badala yake tutumie mitandao katika kutafuta taarifa za
kujenga na kuweza kutuletea maendeleo.
0 comments:
Post a Comment