Wivu wa Mapenzi: Mwanaume Amuua Mama Mkwe wake na Mwanaye kwa kuwachoma Visu
MKAZI wa kitongoji cha Ng’anandi kijiji cha Mpinga Kata ya Kigwe wilayani Bahi, Jumanne Ichirile (23) ameua mama mkwe wake na mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili kwa kuwachoma visu.
Pia amemjeruhi mkewe kabla ya kujiua kwa kujichoma na kisu tumboni, kutokana na wivu wa kimapenzi. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema tukio hilo ni la Jumamosi iliyopita.
Waliouawa walitajwa kuwa ni Sarah Mango wa miaka kati ya 60 na 70 na mtoto, Amina Jumanne mwenye umri wa miaka miwili, ambao waliuawa kwa kuchomwa kwa visu sehemu mbalimbali za miili yao.
Akisimulia mkasa huo, mke wa mtu huyo ambaye alijeruhiwa katika tukio hilo, Elizabeth Kulwa (21) , alisema akiwa nyumbani kwa mama yake mzazi Sarah Mango ilipofika majira ya saa 11 jioni alivamiwa na mume huyo huku akiwa ameshika kisu mkononi.
Alisema ghafla alianza kumshambulia na kumchoma kisu tumboni mara mbili na katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Alisema hii si mara ya kwanza kwa mwanaume huyo kumshambulia, kwani hata mwaka jana alifanya hivyo kwa kumkatakata kwa mapanga yeye na mama yake.
Alisema katika shambulio hilo walifanikiwa kuripoti kwenye vyombo vya sheria na kisha kesi ikafunguliwa mahakamani ambapo mumewe alihukumiwa kifungo cha miezi minane gerezani.
Hata hivyo, mama huyo hana kumbukumbu mumewe huyo alitoka gerezani lini lakini anachokumbuka ni miezi ya hivi karibuni.
Kwa sasa Elizabeth amelazwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu kutokana na majeraha aliyoyapata katika titi la kushoto, ubavuni, tumboni na mkononi
0 comments:
Post a Comment