Walimu walivyoandamana Kasulu, Kigoma
Walimu zaidi ya 200 katika wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wameandamana na kumpa wakati mgumu mkurugenzi wa halmashauri ya Kasulu Masalu Mayaya, wakishinikiza kulipwa kwa madai yao mbalimbali yanayofikia zaidi ya shilingi milioni 172.
Viongozi wa chama cha walimu pamoja na walimu hao kutoka shule mbalimbali za sekondari na msingi wamesema kwa muda mrefu wanaidai serikali fedha za likizo, uhamisho, mapunjo ya mishahara, matibabu na hawapandishwi madaraja kwa mujibu wa sheria.
Walimu hao pia wamemshutumu Afisa Elimu wa halmashauri hiyo Kalugutu Zuberi kuwa amekuwa kikwazo kwa maendeleo ya elimu katika wilaya hiyo na kwamba licha ya serikali kukataza uhamisho wa watumishi bila malipo halmashauri hiyo imekuwa ikihamisha walimu bila ya kuwalipa.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Kasulu Masalu Mayaya akizungumza na walimu hao, ameahidi ofisi yake kushughulikia matatizo hayo kwa haraka na kwamba tatizo la kuchelewa kwa malipo linatokana na uhakiki wa viambatanisho na fedha kutoka serikalini.
Katika kikao hicho cha pamoja kati ya mkurugenzi wa Kasulu na walimu, wamekubaliana kupitia upya madai kwa muda wa wiki moja na kuanza kutoa barua za kupanda madaraja mwezi ujao.
0 comments:
Post a Comment