WAHANGA WA ESCROW!! TUNASUBIRI NENO LA RAIS,TUACHIE NGAZI BAADA YA HUKUMU YA BUNGE"

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, wamesema baada ya hukumu ya Bunge sasa wanasubiri neno la Rais. Viongozi hao waliyasema hayo jana, ikiwa ni siku chache tangu Bunge kupendekeza mamlaka za uteuzi ziwavue madaraka. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyowasilishwa bungeni na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ilionyesha viongozi hao walifanya makosa kadhaa na kusababisha uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Viongozi wengine ambao mamlaka zao za uteuzi zilitakiwa kuwavua nyadhifa zao ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye aliingiziwa Sh bilioni 1.6, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, Sh bilioni 1.6 na Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja Sh milioni 40. Profesa Muhongo alisema: “Sina maoni, sasa wewe unataka kujua nini… kwani wewe umeonaje na ni lazima nikujibu au unataka nikujibu porojo… sasa nakujibu kwamba kaulize Bunge kuhusu hilo suala la Escrow na kama una maswali kuhusu mambo ya umeme nenda Tanesco watakujibu.” Jaji Werema: Siwezi kubishana na Bunge Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, alisema hana kauli wala maoni yoyote na hawezi kubishana na Bunge. “Siwezi kubishana na Bunge kwa sababu wenye mamlaka wamepewa kazi kuchukua hatua, acha wafanye kazi, au unataka nisemeje tena?” alihoji Jaji Werema. Hatima ya Askofu Kilaini, Nzigilwa Kanisa Katoliki nchini limesema haliwezi kuwaadhibu maaskofu wake waliotajwa kuingiziwa fedha zilizotokana na kashfa hiyo kwa sababu wanawajibika kwa kiongozi wa kanisa hilo duniani, Papa Francis. Maaskofu wa kanisa hilo waliotajwa kwenye kashfa hiyo ni Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini aliyedaiwa kupewa Sh milioni 80.5 na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa, Sh milioni 40.4. Akizungumza na waandishi wa habari hizi jana, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki (TEC), Askofu Severin Niwemugizi, alisema hadi sasa hawajataarifiwa kama kuna kosa limefanyika, hivyo hawawezi kukutana. “Kama kungekuwa na kosa angetaarifiwa rais wa baraza… kwakuwa hakuna kosa hakuna dharura yoyote ya kusema tukutane. “Kama kanisa hatuna sababu ya kusema tuhamaki tuwaadhibu kwa sababu askofu yuko chini ya baba mtakatifu,” alisema Askofu Niwemugizi. Hata hivyo, alisema kama vyombo vya dola vikifanya uchunguzi na kubaini kuna makosa ya kinidhamu au kijinai, hapo ndipo wanaweza kuchukua hatua. “’Unless’ uchunguzi ukifanywa wakasema kuna makosa ya kijinai na kinidhamu taratibu nyingine zinaweza zikachukuliwa. “Jambo hili linazungumzwa kisiasa zaidi na ukweli haukusemwa bungeni… hizi ni mbio za urais, sasa wanataka kuwaingiza na wengine ambao hawahusiki,” alisema. Kuhusu Benki ya Biashara ya Mkombozi ambayo ilihusika kupitisha fedha hizo, Askofu Niwemugizi alisema ilifuata taratibu zinazotakiwa ndiyo maana walienda Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kujiridhisha. “Benki inafanya biashara, na mteja anapoleta fedha wanafuata taratibu zinazotakiwa, benki nyingine ziliona wivu kwa kukosa hizo fedha na ndio wanaochochea,” alisema. CAG mpya kuipitia Ripoti ya IPTL Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Musa Juma Asaad, amesema kazi yake ya kwanza ni kuipitia tena ripoti ya ofisi yake juu ya Akaunti ya Tegeta Escrow iliyojadiliwa bungeni hivi karibuni.
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: