Vitendo vya ubakaji, kulawiti watoto vyaongezeka Zanzibar

Chama cha Waandishi Habari Wanawake (Tamwa) Vitendo vya ubakaji na ulawiti kwa watoto vimeongezeka kisiwani Zanzibar huku jumla ya matukio 340 yakiripotiwa. Kauli hiyo imetolewa na Afisa Mratibu wa Chama cha Waandishi Habari Wanawake (Tamwa) anayesimamia mradi wa jinsi na kuwawezesha wanawake (GEWEP), Shifaa Ibuni, mjini Unguja jana. Ibuni alikuwa akielezea maadhimisho ya siku 16 ya kupinga vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake. Mradi huo unaondeshwa na Tamwa kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Care, una lengo la kutoa elimu na kuwawezesha wanawake kutambua haki zao. Alisema Tamwa katika shughuli za utekelezaji ilibaini idadi hiyo ya matukio yaliyoripotiwa katika mahakama mbalimbali ikiwamo Mahakama Kuu ya Vuga, Makahama za wilaya ya Mwera na Mfenesini kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka huu. “Kulingana na ukubwa wa tatizo, tumegundua idadi hiyo ni ndogo kulinganisha na hali halisi ndani ya jamii, baada ya watu wengi kushindwa kusema ukweli kutokana na hofu na unyanyapaa dhidi ya waathirika,” alisema Ibuni. Hata hivyo, alieleza kuwa watuhumiwa wengi hawachukuliwi hatua stahili kutokana na kesi zao kufutwa baada ya shinikizo kutoka kwa ndugu na jamaa wa familia au kwa viongozi wa kijamii. “Ndani ya maadhimisho haya kwa kupitia mradi wa GEWEP, tutaendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuona unyanyasaji huu ufike mwisho, hasa kwa jamii kutambua ubaya pamoja na mtuhumiwa kuadhibiwa vikali,” aliongeza. Aidha, alisema vitendo hivyo vinachangiwa na mambo mbalimbali ikiwamo migogoro ya ndoa, utandawazi, umasikini na tamaa ya watoto kutaka kumiliki vitu vya anasa. Ibuni alieleza jumla ya talaka 1,919 zilitolewa katika kipindi hicho na kusababisha wanawake kutopatiwa mali walizozichuma na waume zao, hivyo matokeo yake watoto wanatelekezwa na kuishi katika hali ya umasikini. Mratibu wa mradi huo kutoka Care, Pamela Rwezaura, alisema shirika lake linashirikiana na Tamwa kuendesha mradi huo kwa lengo la kuwafanya wanawake kujiamini katika kuzalisha mali kwa ajili ya kuongeza kipato pamoja na kutumia ardhi kama nyenzo muhimu katika kufanikisha malengo yao.
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: