TIBAIJUKA: BWANA ALITOA, BWANA AMETWAA

Siku moja baada ya kufukuzwa uwaziri, Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka amewasili jimboni kwake na kusema, “Bwana alitoa na Bwana ametwaa.” Profesa Tibaijuka alivuliwa uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Rais Jakaya Kikwete juzi kutokana na kuhusika kupokea fedha katika akaunti binafsi. Baada ya kuwasili na kupokewa kwa maandamano, Profesa Tibaijuka aliwaomba wananchi kukaa kimya kwa dakika moja ili kumkumbuka katibu wake wa jimbo aliyefariki dunia wakati sakata hilo likijadiliwa bungeni. Profesa Tibaijuka aliyepokewa kwa msafara wa magari kutoka Uwanja wa Ndege wa Bukoba, aliwaeleza wananchi kuwa ilikuwa ni lazima kutafuta msaada kwa watu wengi ili aweze kuwasomesha watoto anaowasaidia kielimu. “Kuna suala la escrow, zamani kulikuwa na aspro ambayo ilikuwa ni dawa ya kweli, sasa suala hili limefikia tamati hamkunichagua ili nikawe waziri, ni sawa na kusema Bwana alitoa na Bwana ametwaa,” alisema Profesa Tibaijuka. Aliambatana na mtoto wa kike akisema ni mmoja wapo wa wanafunzi wasio na uwezo anaowasomesha katika Shule ya Babro Johanson, inayotajwa kuwa ndiyo iliyopokea Sh1.6 bilioni alizoingiziwa katika akaunti yake binafsi, katika Benki ya Mkombozi. Profesa Tibaijuka alitumia muda mfupi kuelezea suala la kuhusishwa katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow akisema Taifa lina changamoto ya kupata elimu bora na wapo viongozi wachache kama yeye wenye moyo wa kusaidia masuala ya elimu. “Teknolojia sasa imekua, naamini mlikuwa mnafuatilia mambo yalivyokuwa yanakwenda, yalikuwa ni mambo makubwa, kazi ya uwaziri nisingeipata bila nyinyi wananchi. Nilikuwa na majukumu mengi, sasa nitapata muda wa kukaa jimboni. “Taifa bado lina changamoto ya kupata elimu bora, hiyo shule mnayoisikia ada yake kwa mwaka ni zaidi ya Sh4 milioni, hivyo lazima nitafute mtu wa kunisaidia. Hakuna mtoto wangu hata mmoja anayesoma kwenye shule hizo,” alisema Tibaijuka. Huku hotuba yake ikikatizwa na watu waliokuwa wakishangilia, Profesa Tibaijuka aliwaonya wanaotaka kulinyemelea jimbo hilo kuwa yuko ‘fiti’ na anawasubiri kukutana nao ulingoni. Alisema atakuwa tayari kufanya kazi katika maeneo yanayoongozwa na vyama vya upinzani jimboni kwake akiamini kuwa pia wapo wanachama wa CCM. >>>Mwananchi
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: