MWENYEKITI WA CHADEMA IRINGA MJINI AINGIA MATATANI
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Iringa Mjini, Frank Nyalusi ameingia matatani baada ya kudaiwa kutoa tuhuma zisizo za kweli dhidi ya Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Iringa, Salim Asas,kwa lengo la kujipatia umaarufu.
Katika mkutano wa hadhara uliofanywa na Chadema hivikaribuni kwenye uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa, Nyalusi ambaye pia ni diwani wa kata ya Mivinjeni mjini Iringa, anadaiwa kutoa tuhuma zinazowahusisha vijana watatu ambao hata hivyo hakuwataja majina; kwamba walitumwa na Kamanda huyo wa UVCCM kwenda kumdhuru.
Taarifa za uhakika zilizoufikia mtandao huu zimedai Asas kwa kupitia wakili wake, Alfred Kingwe amekwisha mkabidhi Nyalusi hati ya madai (Demand Note) inayomtaka kukanusha tuhuma hizo ndani ya siku 14 vinginevyo atafikishwa mahakamani.
Kwa kupitia hati hiyo ya madai Nyalusi anatakiwa kuitisha mkutano katika eneo lile lile alilotolea tuhuma hizo na kukanusha madai hayo yanayoelezwa kupikwa kwa lengo la kuchafua wasifu wa Asas na kumuongezea Nyalusi umaarufu.
Katika kumnurusu Nyalusi dhidi ya mkono wa sheria endapo atashindwa kuitisha mkutano huo, baadhi ya viongozi wa chama hicho wanadaiwa kumpigia magoti Bwana Asas ili suala hilo limalizwe kiungwana.
Mmoja wa viongozi wa chama hicho, Abou Changawa alisema; “tunamtafuta Bwana Salim, tunajua ni muungwana, tunataka suala hili tulimaze kiungwana; kama itashindikana kuitisha mkutano wa hadhara basi tutafanya mkutano na waandishi wa habari ili kuiweka sawa taarifa hiyo.”
Mtandao huu utaendelea kukujuza kinachoendelea kuhusiana na habari hii.....
CHANZO:BONGO LEAKS
0 comments:
Post a Comment