MTUHUMIWA WAUGAIDI ALIYEFIA MIKONONI MWA POLISI HUKO ARUSHA
Hatimaye Abdulkarimu Thabiti Hasia aliyekuwa akituhumiwa kwa ugaidi, amefariki katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru alipokuwa amelazwa kwa miezi sita akiwa mikononi wa polisi.
Taarifa ya kifo cha Hasia aliyekuwa mmoja wa maimamu wa Msikiti wa Geti la Mbao Mbauda, ilitolewa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Arusha wakati kesi ya mtuhumiwa huyo na wenzake saba ilipotajwa.
Hasia aliyekuwa ni mshtakiwa wa pili katika kesi ya kushambulia baa maarufu ya Arusha Naighty Park, alikuwa akikabiliwa na makosa 16 ya ugaidi, amefariki bila kufikishwa mahakamani hata siku moja.
Ilielezwa mahakamani hapo jana, mbele ya Hakimu Hawa Mguruta kuwa mtuhumiwa huyo alifariki Desemba mosi, akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.
Hata hivyo, wakati taarifa hiyo ikitolewa, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Augostino Komba alieleza kutokuwa na taarifa hiyo, hivyo mahakama iliagiza kubadilishwa hati ya mashtaka.
Baadhi ya ndugu wa marehemu walieleza kwamba tangu alipokamatwa na kupata kipigo katika mahojiano na polisi, Hisia alikuwa amelazwa hadi kifo chake.
Kifo cha mtuhumiwa huyo kimekuja wakati kuna malalamiko ya watuhumiwa wengine kupigwa na kujeruhiwa na polisi katika mahojiano na bado wapo gerezani.
Septemba 4 mwaka huu, mtuhumiwa huyo alisomewa mashtaka 16 ya ugaidi akiwa amelazwa hospitalini baada ya kupata fahamu.
Kabla ya kusomewa mashtaka hayo, marehemu alikuwa ameshalazwa hospitalini hapo kwa takriban miezi minne na awali ilishindikana kusomewa mashtaka kutokana na kutokuwa na fahamu.
Kesi ya watuhumiwa wengine wa ugaidi inatarajiwa kutajwa tena Desemba 19 kutokana na kutokamilika kwa upelelezi na watuhumiwa hao walirejeshwa rumande.
0 comments:
Post a Comment