MBUNGE SUGU KUSOMESHA WALIOKOSA ADA

MBUNGE wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi(Sugu),amesema kuwa, hakuna mwanafunzi atakayefaulu na kukosa ada kisha kushindwa kuendelea na masomo ya elimu ya sekondari na chuo kikuu katika jimbo lake. Hayo aliyasema juzi alipokuwa akiwanadi wagombea wa nafasi za serikali za mitaa, katika mitaa ya Muungano, Makanisa, Magorofani na Forest Mpya, katika mkutano wa kampeni uliofanyika jana katika kata ya Forest karibu na chuo kikuu cha Mzumbe tawi la Mbeya. Alisema kazi ya kusomesha wahitaji ni ya jamii, hivyo atatumia mfuko wa jimbo kuwasomesha wale wote watakaofaulu na kukosa uwezo wa kulipiwa karo na kwamba hata kama mfuko huo utakosa fedha, atahamasisha wananchi wawachangie wahitaji hao. Kabla hajawanadi wagombea wa nafasi hizo, alisema anajivunia kusimamia vema mfuko wa jimbo na kutekeleza ahadi zake alizoahidi na kwamba kwa sasa anaanzisha maabara za kompyuta mashuleni ili wanafunzi wakihitimu kidato cha nne, wawe wanatoka na vyeti vya ufaulu wa somo la kompyuta badala ya kwenda kutafuta ujuzi wa matumizi ya kompyuta shule za ufundi. “Tumesimamia vema ujenzi wa barabara za lami za mitaa yetu, ambapo kwa kiwango cha lami zimejengwa kilomita 40 na kiwango cha changalawe pia zimejengwa kilomita 40”alisema Mbunge huyo. Alisema anawashangaa baadhi ya viongozi wa CCM wanaoeneza uvumi kuwa barabara hizo siyo utekelezaji wa ahadi zake kwasababu zimejengwa chini ya ufadhili wa benki ya dunia, jambo ambalo alisema kuwa barabara hizo hata zingejengwa kwa ufadhili wa vikoba, bado zimetekelezwa chini ya utawala wake. Akiwanadi wagombea wa serikali za mitaa, aliwaambia wapiga kura wa Jimbo hilo kuwa, kashfa ya sakata la Escrow lililoisha hivi karibuni Bungeni mjini Dodoma, inatosha kuwa kigezo cha kuwanyima kura wagombea wa nafasi za serikali za mitaa kupitia CCM. Wagombea hao na mitaa wanayowania nafasi za uenyekiti kwenye mabano ni Andrew Mwamakamba, (Muungano), Kwame Elly Anangisye(Makanisani),Habibu Mwangoka (Magorofani) na Ben Mwang’ombola(Forest mpya). Jiji la Mbeya, lina mitaa 181, ambapo Chama Cha Mapinduzi kimepita bila kupingwa katika mitaa 28 na uchaguzi unatarajiwa kufanyika nchi nzima Desemba 14, mwaka huu.
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: