FILIKUNJOMBE AVITAKA VYAMA VYA SIASA LUDEWA KUFANYA KAMPENI ZA KISTAARABU CHAGUZI ZA SERIKALI ZA MITAA.
Mbunge wa jimbo la Ludewa katika mkoa wa Njombe Mh.Deo Filikunjombe amevitaka vyama vya siasa wilayani hapa kufanya kampeni za kistaarabu ambazo hazitaambatana na matusi,kejeli na vijembe katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za mitaa ili kuonesha ukomavu wa siasa na kujenga dhana sahihi ya kampeni kwa vijana na watoto wa Ludewa.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara Katibu wa mbunge huyo Bw.Stanley Gowele ambaye alimuwakilisha katika ziara ya Mbunge ndani ya kata mbili za mwambao wa ziwa Nyasa ambazo ni kata ya Makonde na kata ya Lifuma alisema jamii ya Ludewa haijazoea na haina utamaduni wa kuona wanasiasa wakitoa Lugha chafua wawapo majukwaani,hivyo ni vyema zikafanyika kampeni za kistaarabu.
Lengo la ziara hiyo ikiwa ni kufanya mikutano ya hadhara ili kusikiliza changamoto zinazo wakabili wananchi katika masuala mazima ya kimaendeleo ambapo kila mkutano wananchi ndio walikuwa waongeaji wakuu katika kuuliza maswali na kueleza kelo zao ikiwa pamoja na kukumbushia ahadi ambazo zilikuwa bado hazijatekelewa na Mbunge wa jimbo la Ludewa.
Bw.Gowele alisema kuwa katika mikutano ya hadhara wakati wa kampeni wanaokusanyika kusikiliza sera za wakombea ni watu wenye rika mbalimbali hususani watoto hivyo ni lazima wanasiasa kuangalia Lugha za kutumia ili kukijenga kizazi kijacho kuona siasa si matusi wala vijembe bali ni hoja za msingi zinazoweza kushawishi wananchi kumchagua wampendaye.
Alisema imekuwa ni kawaida ya baadhi ya wanasiasa wasio na ukomavu wakisiasa kutumia muda wa kampeni kwaajili ya kuwatukana wagomvi wao kwa kuwatangaza hadi siri za chumbani kitu ambacho si sawa katika kuwajenga vijana ambao wanatarajia kuwa wanasiasa na viongozi wa kesho hivyo kila chama kina mipango yake ni vyema kuwaeleza wananchi wakuchague ili kuwaletea maendeleo na si kukashifiana wawapo majukwaani.
“Mimi nimetumwa na mbunge wenu Filikunjombe katika ziara licha ya mambo mengine lakini niwaeleze viongozi na wafuasi wa vyama vya siasa kuwa katika kampeni za kuwachagua viongozi wa vijiji na mitaa tufanye kampeni za kistaarabu ambazo zitajenga taswira ya ukomavu wa kisiasa kwa watoto wenu na sio Lugha za kukashifiana kwa visa,pia haipendezi kutukanana wakati wote tunaishi kijiji kimoja naomba vyama visitugawe nduguzangu”,alisema Bw.Gowele.
Katika ziara hiyo Bw.Gowele aliweza kutoa kiasi cha shilingi Laki tano kwa waathirika wa mapolomoko katika kijiji cha Lifuma ambayo yalisababisha uharibifu wa mali za wananchi na watu watatu kupoteza maisha ambapo wananchi hao waliipokea pole hiyo kwa kuimba nyimbo za kumsifu Filikunjombe kwa mambo mengi anayoshirikiana nao.
Vifaa vingine ambavyo alivitoa ni bati 100 katika zahanati ya kijiji cha Nsisi ambayo iko katika hatua ya ujenzi,shilingi laki moja katika mchango wa ujenzi wa majengo ya maabala shule ya Sekondari Makonde vinanda viwili katika kanisa Katoloki la Lifuma na Anglikana kijiji cha Nsisi.
Aidha katibu wa itikadi na uenezi CCM wilaya ya Ludewa Bw.Felix Haule aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uandikishaji kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wametimiza haki ya kikatiba ya kumchagua kiongozi wamtakaye.
Bw.Haule alisema wananchi wengi hasa vijana wamekuwa na ushabiki wa kisiasa lakini wakijisahau suala la kujiandikisha na kukosa sifa za kupiga kura hivyo ni vyema kila matanzania akatambua umuhimu wa kijiandikisha ili kuweza kufanya maamuzi yaliyo sahihi wakati wa kuwachagua viongozi ambao wataweza kuongoza katika maendeleo yanayolalamikiwa na wananchi siku zote.
Alisema kumekuwa na makosa makubwa katika kuchagua viongozi ambao ndio taa ya maendeleo,hivyo inapofuka wakati viongozi hao wakashindwa kutekeleza majukumu yao lawama huelekezwa katika Serikali suala ambalo si sahihi,kinachotakiwa ni kuwapendekeza viongozi wanaofaa na kuwachagua ili kuisaidia Serikali kuu katika kuleta maendeleo kwa wananchi.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment