BABA APIGA MTOTO WAKE KWA STULI HADI AKAMUUA KISA KALA ANDAZI MOJA
BIWI la simanzi lilitanda katika mtaa wa Mutirithia, mjini Molo baada ya mwanamume mwenye umri wa makamo kumpiga mwanawe hadi kufa kwa madai ya kula andazi maarufu kama kangumu bila ruhusa.
Kulingana na jirani yake, Bw Stephen Ngugi, jamaa huyo ambaye ni mlevi kupindukia alifika nyumbani kwake majira ya usiku na baada ya kuarifiwa kwamba mtoto huyo alikula andazi ili kupunguza makali ya njaa, alimpiga hadi akazirai kabla ya kumgonga kichwani kwa kutumia stuli, pigo ambalo lilipelekea mtoto kuvuja damu nyingi.
“Nimemjua mtu huyu kwa zaidi ya miaka kumi na amekuwa mlevi kupindukia. Na niliposikia mayowe nyumbani kwake nikafikiria pengine ashalowa maji ndio maana kapiga kelele,” Ngugi alisema. Ngugi alielezea kuwa jamaa huyo vile vile huvuta bangi na kwamba huenda ndio chanzo cha kutekeleza mauaji hayo. Bi Phylis Wangui ambaye ni shangazi ya watoto hao alisema mtoto huyo, ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya wavulana ya Mt Mary’s mjini Molo amekuwa mtiifu hata ingawa babake amekuwa akiwatesa haswa baada ya kutalakiana na mama yao. Aidha, Bi Wangui alielezea Taifa Leo kwamba baada ya jamaa huyo kutekeleza mauaji hayo ya kikatili, alizitupa baadhi ya nguo alizovaa mtoto huyo na ambazo zilikuwa zimelowa damu kwenye choo ili kuficha ushahidi wa unyama aliomtendea mwanawe. Hata hivyo, jamaa alisahau kulikuwa na alama za damu zilizotapakaa kila mahali, na hata kwenye ukuta na pia kwenye godoro. Wangui amesema baba huyo mlevi na ambaye pia hutumia bangi wamekuwa wakizozana mara kwa mara na mkewe kabla ya kutalakiana kwa muda wa miezi mitatu kwa sasa. Hatua za kisheria Bw Sammy Karanja, ambaye ni babuye marehemu ameitaka serikali kumchukulia hatua za kisheria mshukiwa na pia kuwapa ushauri nasaha watoto wawili ambao walishuhudia baba yao akimtendea ukatili ndugu yao. “Nina huzuni tele kufuatia kifo cha kijana huyu mdogo na ningeomba hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya mshukiwa,” alisema babu huyo. Wakazi wa mtaa huo wameelezea kusitika kwao kufuatia mauaji hayo ya kikatili huku wengi wakitiririkwa na machozi kuona maovu na uhayawani ambao umetekelezwa na baba dhidi ya mwanawe. Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Molo huku mshukiwa akiwa katika kituo cha polisi akisubiri kufunguliwa mashtaka
0 comments:
Post a Comment