A-Z KUHUSU MTOTO ALIYENYONGWA NA BABA WA KAMBO MKOANI MOROGORO!
Abdulrahman Hamis Clemensi enzi za uhai wake.JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia Zamili Shabani kwa madai ya kumnyonga hadi kumuua mtoto wake wa kambo, (mwaka mmoja na nusu) huku mauaji hayo yakihusishwa na wivu wa mapenzi.
Tukio hilo la ajabu lililowaacha vinywa wazi wakazi wa eneo hilo lilijiri saa 6 mchana wa Desemba 2, mwaka huu kwenye nyumba waliopanga wanandoa hao, Zamili na mkewe, Rehema Mustafa (21) iliyopo Kijiji cha Mbogo, Tarafa ya Turiani Wilaya ya Mvomero mkoani hapa.
ALIVYOSEMA SHUHUDA
Kabla ya kuzungumza na mama wa marehemu, Uwazi lilipata mawili-matatu kutoka kwa shuhuda mmoja wa tukio hilo. ”Mimi moja kwa moja namlaumu mama wa mtoto, Bi. Rehema. Awali alikuwa kwenye ndoa na mumewe Hamis, wakabahatika kumzaa Abdulrahman.
“Mwanzoni mwa mwaka huu alifika Zamili akitokea Zanzibar. Kwa taarifa tulizonazo Zamili alikuwa na ishu kubwa kule ndiyo maana akaamua kuja huku. “Unajua vijijini, mtu akitokea mjini wanawake wanamshobokea. Dada yetu Rehema akadanganywa na Zamili akatoka kwenye ndoa yake na kuolewa naye mwezi wa saba mwaka huu.
Rehema Mustafa mama mzazi wa mtoto Abdulrahman Hamis Clemensi. “Toka waoane kila siku ni ugomvi hadi juzi yalipotokea mauaji hayo,” alidai Said Seleman Kindu, mkazi wa kijiji hicho.
MAMA WA MTOTO SASA
Baada ya kuzungumza na Said, Uwazi lilimhoji Rehema ambaye alikuwa na haya ya kusema: “Awali nilifunga ndoa na Hamis Clemensi, tukabahatika kumzaa mtoto mmoja ambaye ni huyo marehemu.
Baada ya kuachana na Hamis nilikaa nyumbani miezi mitatu, nikaja kufunga ndoa na Zamili, Julai 28, mwaka huu. “Tukio zima nahisi kama lilianzia Agosti, mwaka huu kwani nakumbuka siku moja nikiwa sokoni nilikutana na Hamis akamsalimia mwanaye, kumbe kuna mtu alituona akaenda kumwambia Zamili.
“Aliporudi usiku tuligombana sana akitaka nimpeleke mtoto kwa baba yake, nikamwambia mwanangu bado ananyonya siwezi kumpeleka kama vipi asubiri atimize miaka mitatu nitampeleka hata kwa mama yangu mzazi.
“Licha ya kumwambia hivyo, Zamili akagoma, nikamwambia basi anipe talaka nirudi kwetu pia akakataa.” “Siku iliyofuata, usiku alichukua kisu na kuniamuru nimpeleke mtoto kwa baba’ke, tukatoka mimi, yeye na mtoto, lakini baba yake alipotuona alijificha juu ya dari huku akimpigia simu kaka yake anaitwa Kilimo na kumjulisha.
Baba mzazi wa marehemu (kushoto) akiwa na waombolezaji. “Kaka yake alifika, vurugu kubwa ikazuka, baadhi ya vitu vilipotea na kuvunjika kutokana na purukushani hiyo. “Kulipokucha Hamis akaenda kuripoti ofisi ya serikali ya kijiji ambapo mgambo walifika nyumbani na kutuchukua hadi Kituo cha Polisi Mvomero ambapo baada ya kuhojiwa tuliamriwa tumlipe Hamis shilingi laki nne kufidia hasara iliyotokea nyumbani kwake, tulilipa nusu hadi sasa tunadaiwa iliyobaki.”
UGOMVI SIKU YA TUKIO
“Novemba 28, mwaka huu, siku mbili kabla ya mauaji ulizuka ugomvi tena kati yangu na Zamili akipinga kulipa lile deni. Jumamosi tuligomba tena, alikuwa akilalamika kwamba Hamis anamlipisha fedha wakati anamtunzia mwanaye, nikamwambia kama anakereka kumtunza mwanangu anipe talaka, akagoma akidai bado ananipenda.
Hata hivyo, aliahidi kwamba atafanya mauaji.”
SIKU YA TUKIO
“Siku ya tukio Jumanne, saa 5 asubuhi, Zamili alinituma dukani, nikataka kwenda na mwanangu, akasema nimwache atanichelewesha, nikamwacha. “Niliporudi sikumuona mtoto, nikamuuliza Zamili mtoto yuko wapi? Akanijibu kalala, nikaingia jikoni na kusonga ugali, tukala.“Tulipomaliza, mimi nikaenda chumbani kumwamsha mwanangu ili naye ale. Nilishangaa kumuona kalegea. Kwa utoto wangu sikujua kama amekufa, nikaenda kuita wakubwa walipofika wakamuona mtoto kichwa kimegeukia mgongoni, wakaniambia mbona amekufa! “Palepale nikaangua kilio, watu wakajaa, baadaye viongozi wa kijiji wakaja na mgambo wakamkamata Zamili na kumpeleka polisi na mimi nikakodi bodaboda, nikabeba maiti ya mwanangu kuja hapa Mkindo kwa wazazi wangu.
Waombolezaji wakiwa msibani. Mwanangu tumemzika jana (Alhamisi iliyopita),_nimebaki na kumbukumbu ya picha tu,” (akaanza kulia). Rehama alipotakiwa kutoa picha ya Zamili alisema: ”Huyu Zamili hana picha, hata kwenye harusi yetu aligoma kupigwa picha, nadhani alikuwa akitafutwa kule Zanzibar.
Alipoulizwa kama atakuwa tayari kuishi tena na Zamili, alisema: “Siko tayari mimi nataka talaka yangu.”
BABA WA DAMU WA MAREHEMU
Naye baba mzazi wa marehemu, Hamis Clemensi ambaye alikuwepo kwenye msiba huo wa mwanaye alipohojiwa na Uwazi alisema: “Huyu jamaa ni wakuja, tulipata taarifa zake kwamba hakuwa mtu mzuri kule Zanzibar.
Alishataka kuniua mimi baada ya kunivamia kwangu usiku akiwa na mke wangu na mtoto, eti amemleta mtoto wangu, nikapanda kwenye dari na kumpigia simu kaka yangu. Nasikitika kwa kumuua mwanangu.”
0 comments:
Post a Comment