MFANYABIASHARA AJIUA KWA KUJIPIGA RISASI KWENYE BAA JIJINI ARUSHA

MFANYABIASHARA wa Arusha anayemiliki kampuni ya Tanzania Bush Camp yenye kambi za watalii katika hifadhi za Serengeti mkoani Mara na Manyara iliyopo katika mikoa ya Arusha na Manyara, Timoth Mroki (36) amejiua kwa kujipiga risasi tatu kifuani akiwa katika baa maarufu ya Arusha Raha iliyopo eneo la Shams, jijini hapa. Kisa cha kujiua kwake kimetajwa ni kusababisha ajali, baada ya kuligonga gari lingine katika eneo la Mbauda wakati akitoka katika makazi yake yaliyopo eneo la Kwa Mrombo, jijini hapa. Alifikwa na mauti katika tukio lililotokea kati ya saa 1:30 na saa 2:00 usiku, ndani ya baa hiyo. Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Mroki alifika katika baa hiyo baada ya kufanikiwa kuwatishia kwa risasi waendesha bodaboda waliokuwa wamemzingira katika eneo la ajali na kisha kuondoka kwa kasi kwa gari lake aina ya Nissan Navara. “Alipiga risasi mbili hewani waliokuwa wamemzunguka wakanywea, akatumia mwanya huo kukimbia na moja kwa moja akafika Arusha Raha pengine kwa lengo la kujificha, na hapo akaanza kunywa… “Ingawa inaonekana alikotoka alikunywa kidogo, alipofika Arusha Raha alikunywa haraka pombe mbili kali aina ya Valuu (Valeur) na wakati anamalizia ya tatu, akajikuta anazingirwa tena na wale waendesha bodaboda,” anasema mtoa habari huyo na kuongeza kuwa, baada ya kufyatua tena risasi mbili nyingine hewani, lakini bila ya dalili ya watu hao kutishika, ndipo akaamua kujimiminia risasi. Habari zaidi zinasema wakati anazingirwa, naye akijihami kwa risasi wasamaria wakiwa katika harakati za kupiga simu Polisi walishtukia wakiingia katika eneo la tukio lakini tayari Mroki alikuwa ameshajitoa uhai baada ya kujimiminia risasi kifuani. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatusa Sabas hakupatikana kuzungumzia tukio hilo, ingawa Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi ya wilaya ya Arusha imekiri kuwepo kwa tukio hilo, lakini chanzo chetu kikikataa kutajwa jina gazetini kwa kuwa si wasemaji wa matukio ya polisi mkoani Arusha. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru.
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: