Maana ya ndoa
Ndoa maana yake ni muungano wa hiari kati ya mwanaume na mwanamke unaokusudiwa kudumu kwa muda wa maisha yao yote (Kifungu cha 9 cha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971). Ili ndoa hiyo iwe halali hapa nchini inapaswa kufuata matwaka ya Sheria za Tanzania kama:
Muungano lazima uwe wa hiari, muungano uwe ni kati ya mwanamke na mwanaume, muungano huo uwe unakusudiwa kuwa wa kudumu, wafunga ndoa wawe wametimiza umri unaokubalika kisheria, wafunga ndoa wasiwe maharimu (wasiwe watu wenye mahusiano ya karibu ya damu au kindugu), kusiwe na kipingamizi na mfungishaji ndoa awe na mamlaka ya kufungisha ndoa.
Aina za ndoa
Kulingana na Sheria ya Ndoa kuna aina kuu mbili za ndoa; ndoa ya mke mmoja na ndoa ya zaidi ya mke mmoja. (Ifahamike kwa Sheria ya Tanzania mke anapaswa kuwa na mme mmoja tu).
(a)Ndoa ya mke mmoja
Huu ni muungano unaoruhusu mwanamme kuoa si zaidi ya mke mmoja. Mfano, ndoa ya Kikristo.
(b) Ndoa ya zaidi ya mke mmoja
Huu ni muungano unaoruhusu mwanamume kuoa mke zaidi ya mmoja. Mfano, ndoa za Kiislamu na ndoa za kimila.
Sheria ya Ndoa inatambua aina tatu za ufungaji ndoa yaani kiserikali, kidini na kimila. Pamoja na aina za ndoa zilizotajwa hapo juu sheria ya ndoa inatambua dhana ya kuchukulia ndoa hii ni kwamba iwapo itathibitishwa kwamba mwanamume na mwanamke wameishi pamoja kwa muda wa miaka miwili au zaidi na kupata heshima ya mume na mke basi itakuwepo dhana inayokanushika kwamba watu hao walioana ipasavyo. Madhumuni ya dhana hii ni kumwezesha mwanamke na watoto kupata masurufu pale ambapo ndoa inavunjwa.
HAKI NA WAJIBU WA MUME AU MKE KATIKA NDOA
Baada ya kufunga ndoa na ikaonekana haina kasoro yoyote, mke na mume aana haki mbalimbali kisheria anazostahili kuzipata kisheria. Haki hizi ni kama;
Matunzo
Mke au wake wana haki ya kutunzwa na mume wao kwa kuwapatia mahitaji muhimu kama chakula, malazi, mavazi, matibabu, n.k kulingana na uwezo alionao mume. Hivyo katika ndoa mume anao wajibu wa kumkimu mkewe kwa kumpatia malazi, Nguo na chakula. Mke mwenye kipato vile vile anao wajibu wa kumkimu mumewe ikiwa tu mume huyo:
· Hajimudu kabisa.
· Hawezi kupata chumo la Maisha yake kwa sababu ya athari ya akili au afya mbaya
(hii ni kwa mujibu wa Sheria ya ndoaSura ya 29 ya sheria kifungu 63).
Hivyo basi kisheria mume ndio mwenye wajibu wa kwanza wa kumtunza mkewe. Mke anaweza kumtunza/kumkimu mume ikiwa mume hajimudu i.e hawezi kufanya kazi au shughuli kwa sababu mbalimbali kutokana na athari ya akili au akiwa na afya mbaya. Ikumbukwe mke anaweza kudai kwenye vyombo vya kisheria ikiwemo mahakama kama mume hatampa matunzo.
kutunza watoto
Mume na mke wana wajibu wa kumtunza na kumhudumia mtoto wao na kumpatia mahitaji muhimu kama chakula, nguo, malazi, elimu na mahitaji muhimu. Ni kosa kisheria kutokumuhudumia mtoto wakati ukiwa na uwezo wa kumhudumia. Makosa hayo ni:
Kutelekeza Watoto
Kwamba mtu yeyote ambaye, ni mzazi au mlezi au mtu mwingine mwenye uangalizi au utunzaji halali wa mtoto yeyote mwenye umri usiozidi miaka kumi na nane, hali ana uwezo, wa kumuhudumia mtoto, kwa kuamua au kinyume cha sheria, au bila ya sababu za msingi atakataa kumhudumia, na akamtelekeza mtoto bila msaada, atakuwa ametenda kosa. Kifungu cha 166 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ya sheria za Tanzania pamoja na kifungu cha 188 cha Sheria ya Mtoto ya 2009.
Kosa la Kupuuza kumpa chakula mtoto n.k
Mtu yeyote ambaye, ni mzazi au mlezi au mtu mwingine mwenye uangalizi au utunzaji halali wa mtoto yeyote mwenye umri usiozidi miaka kumi na nne na asiyejiweza, akakataa au kupuuza (hali ya kuwa anaweza kufanya) kumpa chakula cha kutosha, nguo, malazi na mahitaji mengine ya lazima kwa maisha ya mtoto kiasi cha kumdhuru kiafya mtoto huyo, atakuwa ametenda kosa. Kifungu cha 167 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ya sheria za Tanzania pamoja na kifungu cha 189 cha Sheria ya Mtoto ya 2009.
Umiliki wa pamoja wa mali na mahusiano baina ya wanandoa
Mali ya mke au mume iliyopatikana kutokana na jasho lao wote wawili ni mali yao kwa pamoja hata kama juhudi zao au jasho lao katika kupata mali hizi si sawasawa. Lakini pamoja na hayo kuna dhana inayokanushika kuwa kama mali hii imeandikishwa kwa jina la mmoja wao basi ni mali yake. Ni wajibu wa yule anayedai kuthibitisha kuwa pamoja na kwamba mali pamoja na kwamba mali imeandikishwa kwa jina la mwenzake, ni mali yao kwa pamoja. Mwanandoa huyo anaweza kuthibitisha kwa kuonyesha kwamba amechangia jasho lake mfano kwa kuendeleza, kuzalisha au kuboresha mali hiyo. yule mwanandoa aliyechangia atakuwa amepata haki ya kumiliki ile mali kwa hisa ya pamoja (occupancy in common) na yule mwenye haki ya kumiliki ardhi.
Mke au mume ana haki ya kumiliki mali aliyoipata kabla ya ndoa kama aliipata kwa fedha yake mwenyewe ingawa mwenza (mume/mke) ana haki kama ilivyoelezwa hapo juu akonyesha kuwa amekuwa akichangia kuiendeleza au kuitunza. Pia Mke ana haki ya kuingia mikataba, kushitaki na kushitakiwa kwa jina lake mwenyewe
Jivunie kuwa mwana ludewa
Blogger Comment
Facebook Comment