HABARI MBALIMBALI


KATAVI
MKAZI wa Kijiji cha Kapalala Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi , Mele Seni (60) ameuawa kikatili kwa kukatwa mapanga kichwani na mgongoni na watu wasiofahamika wakati akiwa nyumbani kwake akiota moto, sababu kubwa ikielezwa kuwa mzee huyo alikuwa anatuhumiwa kwa ushirikina.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea jana saa moja na nusu usiku wakati Seni akiwa anaota moto nyumbani kijijini hapo.
Alisema siku hiyo ya tukio Seni akiwa nyumbani kwake amejipumzisha akiota moto ghafla walitokea watu wasiofahamika na kupiga hodi nyumbani kwa Seni ambapo aliwakaribisha akidhani ni watu wema.

Inadaiwa ndipo watu hao wakiwa na mapanga walipoanza kumshambulia Seni kwa kumkata kwa panga kwenye kichwa na mgongoni huku akipiga mayowe kuomba msaada kwa majirani zake.


MBEYA

SERIKALI mkoani Mbeya, inakusudia kuzichukulia hatua za kisheria kampuni zote za ulinzi zitakazotoa ajira kwa vijana wasio na sifa, ikiwa ni pamoja na kupata mafunzo maalumu ya ulinzi.
Aidha, zimetakiwa kuanzia sasa ziwaondoe kazini wote waliojiriwa bila kupitia mafunzo ya ulinzi. Hayo yalisemwa juzi mjini hapa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Chrispin Meela wakati wa kufunga Mafunzo ya Mgambo katika Kituo cha Sabasaba, Tarafa ya Iyumba jijini hapa.
Meela ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, alisema kuendelea kutoa ajira kwa watu wasio na sifa imekuwa chanzo cha walinzi wengi kukiuka maadili ya kazi yao na kushirikiana na majambazi kufanya uhalifu katika maeneo wanayopangiwa kufanya kazi.
Aliwataka pia wamiliki wa kampuni za ulinzi kuhakikisha wanaongeza mishahara ya wafanyakazi wao ili kuwafanya wasiwe na mioyo ya kutamani kushirikiana na wahalifu wakiamini watapata chochote wakifanikiwa kufanikisha uhalifu.
Wakati Mkuu huyo wa Wilaya akiyasema hayo, baadhi ya wanamgambo waliohitimu mafunzo hayo wakitokea kazini, wamewalalamikia waajiri kwa kutojali maslahi ya askari wao, huku wale wa kike wakidai hawajaliwi kabisa wanapokuwa wajawazito na hata wakijifungua.
Hali hiyo ilibainishwa katika risala ya wahitimu 112 waliohitimu mafunzo hayo, 27 kati yao wakiwa wa kike.

SHINYANGA
WATUMISHI wa Serikali wametakiwa kuwa na utaratibu wa kutunza siri za Serikali pamoja na kusimamia misingi, sheria na taratibu zilizowekwa kwa lengo la kuleta ufanisi katika maeneo yao husika ya kazi.
Hayo yalibainishwa juzi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Halmashauri ya Msalala, Patrick Kalangwa katika semina ya siku moja iliyojumuisha wafanyakazi wa Idara ya Uhamiaji mkoani Shinyanga.
Kalangwa aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kahama Benson Mpesya katika semina hiyo, alisema kwa sasa ni wajibu wa watumishi wa umma kufuata sheria na taratibu ili utendaji wa kazi uweze kufanyika kwa ufanisi.
Aidha, alisema watumishi hao wa Serikali hususani wa Idara ya Uhamiaji lazima wajenge imani ya kuaminika na wateja wao wanaowatumikia hali ambayo itaepusha malalamiko katika idara husika.
Awali Naibu Kamishna wa Uhamiaji mkoani Shinyanga, Anna- Maria Yondani alisema lengo la semina hiyo ni kukumbushana juu ya maadili ya Utumishi wa Umma pamoja na utunzaji wa nyaraka mbalimbali za Serikali.
Alisema Semina hizo za mara kwa mara zinalenga kuwakumbusha watumishi wa Uhamiaji juu ya maadili ya kazi na mambo mengine yanayohusu idara hiyo.
MOROGORO
MKUU wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Anthony Mtaka amewataka madiwani na viongozi wengine kuacha kuingiza masuala ya siasa kwenye mgogoro wa wafugaji na wakulima kwani hakutaleta suluhisho la kudumu.
Hivyo amewasihi wasianze kutafuta kura za kisiasa kwa kutumia migogoro ya wakulima na wafugaji ya muda mrefu iliyomo wilayani humo kwa kuwawekea chuki za siasa katika migogoro inayojitokeza kwa vile migogoro mingi kiini chake na sababu zake ni ardhi.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema hayo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero juzi, mara baada ya kupewa fursa ya kutoa hotuba yake mbele ya madiwani ikiwa ni siku chache tangu kutokea mapigano baina ya pande hizo ambayo yalisababisha vifo vya watu sita na kujeruhi 36 katika Kata ya Hembeti, wilayani humo.
“Tusianze kutafuta kura za kisiasa kwa kutumia migogoro ya wakulima na wafugaji na tusiweke siasa katika migogoro ya wafugaji na wakulima ...yapo maneno ya ukakasi juu ya mgogoro huu , mimi naona kama mtu hana maneno mazuri ya kuyasema mbele ya wananchi wake ni bora waache kufanya hivyo,” alisema Mkuu wa Wilaya.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya , hotuba za wanasiasa zinazotolewa mbele ya wananchi katika maeneo hayo zinakera jamii na kuwa na dalili ya kuendeleza chuki na uhasama jambo ambalo linaweza kuhatarisha amani na utulivu iliyorejea.
Hivyo aliwakumbusha madiwani na viongozi wengine wa kisiasa katika mikutano yao kutambua wajibu wao wa kuhubiri amani na pamoja na kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuheshimu sheria na vyombo vya dola pele vinapofanya majukumu ya kulinda amani ya raia.
Mkuu huyo wa Wilaya pia alitumia fursa hiyo kupiga marufuku vikundi vya ulinzi wa jadi ‘ Umwano’ kushiriki kwenye masuala ya ulinzi na ukamataji wa mifugo kwa vile vimebainika vinatumiwa vibaya na shughuli zote za ulinzi zinataendelea kufanyika chini ya askari Polisi, mgambo na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Jonas Van Zeeland, alisema Baraza linalaani mauaji yaliyotokea ya wakulima na wafugaji na kuwasihi madiwani ambao ni wanasiasa wasikubali mambo hayo yajirudie kwa mara nyingine tena.









Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: