PARACHICHI: Huukinga mwili dhidi ya sumu, hukimbiza uzee

PARACHICHI ni tunda linaloupatia mwili vitamini C. Tunda hili hupatikana kwa wingi katika mikoa ya Kilimanjaro, Tanga na Mbeya.
Pamoja na umuhimu wake tunda hili pia limekuwa likitumiwa na wanawake wengi kama nyenzo mojawapo ya urembo kwa kupaka usoni, au nywele.
Parachichi lina faida nyingi kiafya, hususan kuukinga mwili dhidi ya kemikali hatari pamoja na kumfanya mtu kuonekana kijana.
Wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Michoacana de San Nicolas de Hidalgo cha nchini Mexico wanaeleza kwamba tunda hilo husaidia katika kuukinga mwili dhidi ya kemikali hatari (free radicals), hivyo kuweka kinga dhidi ya magonjwa mengi pamoja na kumfanya mtu kuonekana kijana.
Wanasayansi hao wanaeleza kuwa mafuta yanayopatikana katika parachichi yana uwezo wa kupenya hadi ndani ya injini inayotengeneza nishati mwilini inayopatikana katika seli inayojulikana kama mitochondria.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, free radicals ni kemikali zinazosababisha magonjwa mengi yakiwamo baadhi ya saratani, kuharibu mishipa ya damu ya ateri arteries, pamoja na kumfanya mtu kuzeeka haraka.

Wanaeleza kuwa mafuta yanayopatikana katika baadhi ya mboga za majani, matunda na nyanya/tungule yana uwezo wa kupambana na kemikali hizo hatari lakini mafuta haya hushindwa kuingia ndani ya mitochondria ambako ndiko kuna kemikali hizo hatari kwa wingi.
Naye Mtafiti Christian Cortes-Rojo kutoka Chuo Kikuu hicho cha Mexico ambaye ndiye alifanya utafiti huo, anasema anti –oxidants zinazopatikana katika mboga za majani na matunda mengi haziwezi kupenya ndani ya mitochondria, hivyo kushindwa kudhibiti kemikali hatari ndani ya mitochondria hizo.
Hatua hiyo huelezwa kusababisha kemikali hizo hatari kuendelea kushambulia mitochondria na kuziharibu na matokeo yake ni kuwa nishati haitolewi tena kutoka kwenye mitochondria na seli hushindwa kufanya kazi na kufa.
Matokeo ya utafiti huu yalitolewa katika kongamano la kila mwaka la chama cha wataalamu wa mambo ya biochemistry na bayolojia ya viumbe hai kutoka nchini Marekani (American society of biochemistry and molecular biology annual conference).
Kemikali hizi hatari ni uchafu na zinatolewa na mwili wakati wa kusaga chakula na huweza kutolewa kwa wingi kwa mtu anayevuta sigara, mtu anapokumbana na mionzi na hata wakati kukiwa na uchafuzi wa mazingira.
Kemikali hizi uharibu mpangilio wa protini katika muundo wa vinasaba.
Wanasayansi hao wakati wanafanya utafiti waliweza kuona ya kwamba mafuta ya parachichi yaliwezesha seli za ‘yeast’ kuishi kwa muda mrefu kwenye madini chuma licha ya kuwekewa kiwango kikubwa cha madini hayo ambayo ndiyo hutoa kemikali hizi hatari kwa wingi.
Katika tafiti ambazo ziliwahi kufanyika huko nyuma nchini Mexico, ambayo inaongoza kwa uzalishaji wa parachichi duniani, zilionesha ya kwamba parachichi hupunguza kiwango cha rehemu mwilini na pia hupunguza baadhi ya mafuta yanayohusishwa na ugonjwa wa kisukari.
Mafuta ya parachichi yana virutubisho sawa na mafuta ya olive oil yanayohusishwa kwa kusaidia kupunguza lehemu mwilini pamoja na kinga dhidhi ya magonjwa mengi sugu kama inavyoonekana kwa watu wanaoishi katika nchi za mediteranean ambao ni watumiaji wazuri wa mafuta haya ya olive.
Kwa muda mrefu wanasayansi wamekuwa wakiita parachichi kama mfalme wa matunda kutokana na kuwa na virutubisho vingi kuliko tunda jingine lolote duniani.
Kutokana na umuhimu wa parachichi, kuna haja kwa kila mwanajamii popote alipo kuhakikisha anazingatia somo hili, ikiwamo kulitumia kwa wingi tunda hili kwa manufaa yake.
Pamoja na mtu mmoja mmoja kuhakikisha anatumia tunda hili ni muhimu pia kwa serikali na hata wakulima kutilia mkazo kilimo cha matunda haya ili kuboresha afya.
Imeandikwa na Hellen Ngoromera

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari. Kwa maoni na ushauri, niandikie kupitia helenpendo@yahoo.com au 0754 886 749.
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: