KESI YA SHEHE PONDA BADO HALI NI TETE
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa Morogoro jana ilishindwa kuanza kusikiliza kesi ya Katibu wa Jumuiya ya Waislamu Tanzania, Shehe Ponda Issa Ponda kutokana na mgongano wa kiutawala na kukosekana kwa nakala ya hukumu ya rufaa iliyompa ushindi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.
Kesi ya Ponda ilishindwa kuanza kusikilizwa mahakamani hapo kufuatia kushindwa kufikishwa kwake kulikosababishwa na kusigana kwa tarehe iliyopangwa kwenye jalada la kesi hiyo ambayo ni Desemba 8, mwaka huu, na ile ya amri ya kutolewa rumande ya Gereza la Morogoro kwa uongozi wa Jeshi la Magereza ikiwa imeandikwa akitakiwa kuondolewa Desemba 10, mwaka huu ili kufikishwa Mahakamani.
Katika kikao hicho, upande wa mashikata ukiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Sunday Hyera, sambamba na maofisa wa Mashikata wa Polisi, wakati kwa upande wa utetezi wa Ponda, uliwakilishwa na Wakili Bartholomew Tarimo.
Hata hivyo baada ya kumaliza majadiliano hayo mafupi Mahakamani hapo, Wakili Tarimo, aliwaambia waandishi wa habari kuwa kumetokea tofauti ambayo imesababishwa Ponda kushindwa kufikishwa mahakamani hapo.
Kwa mujibu wa Wakili huyo wa utetezi, kusigana huko ni kwa tarehe ya hati iliyotolewa kwa Jeshi la Magereza kuhusu kuletwa Ponda Mahakamani hapo ikiwa ni tofauti na uliyopo katika jalada la kesi yake.
Hivyo alisema kuwa, jalada la kesi hiyo limeandikwa siku ya Desemba 8, mwaka huu kuwa mshikatiwa afikishwe mahahakamani, ikiwa ni tofauti na waliyopelekewa Magereza ya kuletwa kwake mahakamani kuwa ni Desemba 10, mwaka huu.
Pia alisema upande wa utetezi sambamba na wa Jamhuri pamoja ulifikia uamuzi wa kuahirishwa kwa kesi hiyo hadi Desemba 22, mwaka huu kutokana na kutokuwepo mahakamani hapo nakala ya hukumu ya rufaa ya kesi aliyoshinda Shehe Ponda iliyotoka Mahakama Kuu ya Kanda ya Dar es Salaam iliyompa ushindi akipinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu.
0 comments:
Post a Comment