Na Njenje ze ropo
Ludewa
Akizungumza katika hafla maalum ya utoaji wa vyeti na barua za shukrani kwa wachangiaji, Mhe. Thomas alisema kuwa ushirikiano mkubwa uliooneshwa na jamii umekuwa nguzo muhimu katika kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
> "Tunawashukuru sana wadau wote na wananchi kwa moyo wao wa kizalendo. Ushirikiano huu umeleta mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu, na tutaendelea kushirikiana katika kuhakikisha kila mtoto wa Ludewa anasoma katika mazingira bora," alisema Mhe. Thomas.
Aidha, Mkuu huyo wa wilaya alihimiza wananchi kuendeleza mshikamano na ushirikiano katika juhudi za kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika wilaya hiyo. Alibainisha kuwa, licha ya mafanikio yaliyopatikana, bado kuna uhitaji wa takribani madawati 3,000.
> "Michango iliyopatikana ni hatua kubwa, lakini bado hatujafikia lengo. Tunawaomba wadau waendelee kujitokeza ili tufikie mahitaji halisi ya madawati kwa shule zetu," aliongeza.
Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi, Bi. Munawara Swai, alieleza kuwa harambee hiyo ilifanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi milioni 49.791,500 kutoka kwa wadau 89. Fedha hizo zilitumika kutengeneza madawati 1,041 pamoja na viti na meza kwa shule za sekondari.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Ndugu Castor Kibasa, alisema mafanikio hayo ni ushahidi tosha wa mshikamano wa wananchi wa Ludewa.
> "Tunaona wazi kuwa wananchi wetu wana uzalendo wa dhati. Umoja huu ni chachu ya maendeleo endelevu, hasa katika sekta ya elimu," alisema Kibasa.
Harambee hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali kwa kushirikiana na jamii katika kuhakikisha sekta ya elimu inaboreshwa kwa kuwapatia wanafunzi mazingira rafiki na salama ya kujifunzia, sambamba na kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya msingi ya elimu.
0 comments:
Post a Comment