Mbeya,Tanzania.
BAADA ya mapumziko ya wiki moja kupisha wiki ya mechi za timu ya Taifa, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, inatarajia kuendeleza kampeni yake ya kutwaa taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa kukipiga na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya kesho saa 10.30 jioni.
Tayari kikosi cha Azam FC kipo kamili tokea juzi Jumapili kilipwasili jijini hapa kwa ajili ya mchezo huo sambamba na ule wa Jumamosi ijayo (Septemba 10) dhidi ya Mbeya City.
Kwa miaka mingi sasa tokea Azam FC ipande Ligi Kuu Julai 27, 2008, imekuwa ikikutana na upinzani mkali kutoka kwa maafande hao katika mechi zote za nyumbani na ugenini.
Rekodi zao (Head to Head)
Kuelekea mchezo huo wa kwanza wa ugenini wa Azam FC msimu huu, mtandao rasmi wa klabuwww.azamfc.co.tz umekuandalia rekodi muhimu za ligi tokea timu hizo zianze kukutana kwa mara ya kwanza Oktoba 25, 2008, mchezo ulioshuhudiwa ndani ya Uwanja wa Sokoine, Prisons ikishinda 2-0.
Mpaka sasa katika rekodi zao, Azam FC na Tanzania Prisons zimekutana mara 12 ndani ya ligi, huku rekodi zao zikifanana kwenye kila kitu kuanzia mechi za kushinda hadi walizotoka sare.
Rekodi hizo zinaonyesha kuwa, nusu ya mechi hizo 12 (mechi sita) timu hizo zimeenda sare huku pia kila upande ukishinda mara tatu.
Jumla ya mabao 20 yamefungwa na timu hizo katika mechi zote 12 walizokutana, cha kustaajabisha zaidi kila timu imefunga mabao 10 jambo ambalo linaongeza zaidi mvuto kwenye mchezo wa kesho.
Hadi timu hizo zinakutana tena, Azam FC imeonekana kuwa na takwimu nzuri ya ufungaji mabao kuliko Prisons msimu huu, wakati wote wakiwa wamecheza mechi mbili mpaka sasa matajiri hao wamefunga manne huku maafande hao wakitupia mawili tu, lakini wote wameruhusu wavu wao kuguswa mara moja.
Ukiondoa mechi za ligi, pia timu hizo zimewahi kukutana katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) Machi 31 mwaka huu ndani ya Uwanja wa Azam Complex, mchezo ambao uliisha kwa Azam FC kuibuka kidedea kwa kufuzu kwa nusu fainali kwa ushindi wa mabao 3-1, yaliyofungwa na Shomari Kapombe aliyetupia mawili na Khamis Mcha akitupia moja.
Mfanano na msimu uliopita
Pambano hili limeonekana kufanana na lile la msimu uliopita kwenye mzunguko wa pili kwa upande wa Azam FC, ambapo matajiri hao wataingia dimbani wakiwa na lengo kubwa la kuibuka na ushindi ili kurejea kileleni katika msimamo wa ligi.
Vilevile Februari 24 mwaka huu zilipokutana mara ya mwisho ndani ya uwanja huo, Azam FC iliingia dimbani ikiwa na nia ya kuibuka na ushindi ili kurejea kileleni kwa kuishusha Yanga, lakini ilishindwa kufikia malengo hayo kufuatia mchezo kuisha kwa sare ya bila kufungana.
Hivyo, hata kesho ushindi wowote wa zaidi ya bao moja kwa upande wa Azam FC, utaifanya kurejea kileleni kwenye msimamo ikifikisha pointi saba na kuishusha Mbeya City ambayo nayo ina pointi hizo lakini itazidiwa idadi ya tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa (GD) kwani mpaka sasa imefunga mabao manne tu na kufungwa moja.
Bocco kuendelea kucheka na nyavu?
Nahodha wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, ameendelea kuwa mhimili mkubwa kwenye eneo la ushambuliaji la timu hiyo, ambapo hadi sasa msimu huu amefanikiwa kufunga mabao mfululizo katika mechi zilizopita za Azam FC.
Mpaka sasa ameandika rekodi ya kufunga mabao matatu ndani ya mechi mbili, akifunga moja kwenye mechi ya ufunguzi dhidi ya African Lyon iliyoisha kwa sare ya 1-1 na akatupia mawili Azam FC ilipoichabanga Majimaji ya Songea 3-0.
Bocco ambaye pia ni nahodha msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, mpaka sasa katika mechi za mashindano msimu huu, amefunga mabao manne ndani ya mechi tatu.
Mechi nyingine iliyomfungulia rekodi hiyo ni ile dhidi ya Yanga waliyoshinda kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 90 na kutwaa taji la Ngao ya Jamii, ambapo Bocco alifunga bao la pili la kusawazisha dakika ya 89.
Jambo kubwa linalosubiriwa kesho ni Je, Bocco ataendelea na moto wake wa kutupia mabao zaidi na kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa wafungaji bora msimu huu? Ni jambo la kusubiri baada ya dakika 90 kumalizika.
Zeben alonga
Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, amewaambia mashabiki wa timu hiyo kuwa wamekuja na kazi moja tu mkoani Mbeya kusaka pointi sita wakianza na ushindi kwa mchezo wa kesho dhidi ya maaafande hao.
“Lakini izingatiwe ya kuwa ligi sio nyepesi kiasi hicho kutokana na timu zote tulizocheza nazo kujiandaa, kikubwa tumekuja kufanya kazi tutaonyesha uwezo wetu, lakini tunaamini kuwa tutahakikisha tunapata zile pointi ambazo tumekuja huku kuzifuata na baada ya hapo tutarudi nyumbani (Dar es Salaam) kucheza mchezo dhidi ya Simba,” alisema.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji murua kabisa kinachochangamsha koo cha Azam Cola, katika kufanya maandalizi yake mwisho kabla ya kupambana na Prisons, leo Jumanne jioni inatarajia kufanya mazoezi ya mwisho ndani ya uwanja huo ikiwa na kikosi chake kamili
Ludewa yetu na maendeleo yetu posted by barnabas njenjema, kutoka Ludewa
0 comments:
Post a Comment