JINSI FEDHA ZINAVYOATHIRI MAPENZI



Kila mtu anatumia fedha, sisi sote tunataka fedha na tunafanya kazi kutafuta pesa zaidi na mara nyingi tunafikiri juu ya fedha na matumizi yake. Hebu fikiria kama kungekuwa hakuna fedha duniani maisha yangekuwaje leo. Hebu fikiria umefika dukani na unataka kununua kitu lakini mfukoni huna fedha ya aina yoyote ungefanya nini? Labda ungeweza kumuomba mwenye duka akupe kazi ya kupanga mabox na ufanye usafi dukani ili akupe kilo moja ya mchele. Fedha ina kazi kubwa mbili:-

(1)        Ni kitu ambacho kinakuwezesha kubadilishana na mtu mwingine vitu au huduma kama vile kununua chakula au muda wa maongezi kwa simu yako.

(2)        Ni ghala la thamani, fedha inakuhifadhia thamani ambayo unaweza kuitumia baadae utakapohitaji kitu au huduma fulani ambayo itasaidia katika kukufanya ufurahie maisha yako.

Fedha hainunui penzi lakini penzi haliwezi kununua zawadi ya valentine, fedha haziwezi kununua penzi lakini hurahisisha kazi ya kupendana sikiliza kesi hii.

Mimi ni dada wa miaka 27 nimekuwa na uhusiano na kaka mwenye uwezo mkubwa wa kifedha kwa zaidi ya mwaka mmoja la ajabu ni kwamba anajipendelea sana yeye mwenyeywe na haangalii kipato change kidogo, atanunua simu mpya, laptop mpya japo anazo za zamani zinazofanya kazi na kwa upande wa nguo usiseme makabati hayatoshi. Inaniumiza kuona anaishi maisha ya fahari na haoni ninavyohangaika. Naogopa kuzungumza nae juu ya hilo kuogopa kuonekana napenda pesa zake zaidi na inaniumiza moyo wangu.

Ningependa nitoe angalizo kwa wanaume ambao wana wapenzi ambao wana uwezo mkubwa wa kifedha zaidi yao. Kwa mwanaume ni muhimu ukumbuke kuwa haijalishi mwanamke ana uwezo mkubwa wa kifedha kiasi gani angependa aendelee kuchukuliwa kama mwanamke na unapaswa kuhakikisha kuwa unampa mahaba sahihi na ya kutosha nje na ndani ya chumba cha kulala. Onyesha shukrani za kutosha juu ya mchango wake mkubwa kifedha japokuwa mwanamke huyo ana uwezo mkubwa kifedha. Kumbuka kuwa  mwanamke huyo bado anatarajia zawadi utakayomchagulia wewe kuonyesha jinsi gani unamuona ni wa kipekee.Kwa kufanya hivyo utamzuia asione uwezo wako mdogo wa kifedha kutokana na ukubwa wa penzi lako.

Mwanamke ambaye anajikuta ana fedha nyingi kuliko mwanaume ajitahidi kuepuka kuonekana yeye ndie dereva wa uhusiano wao, tambua mwanaume hatavumilia aina yoyote ya dharau au kupewa nafasi ya chini kwako. Hivyo kuwa mwangalifu katika maneno na mwenendo wako.  Kama mwanamke lazima ukumbuke kuwa mpenzi wako angependa akulipie huduma fulani japokuwa uwezo wake wa kifedha ni mdogo hivyo aonyeshapo nia ya kufanya hivyo usimzuie.

Mwisho kwa wote wawili pale mnapotoka kwenda hotelini kwa chakula na vinywaji ni muhimu mjadiliane kuwa ni nani atakaelipa ili isijetokea hali itakayomuaibisha yule mwenye kipato  kidogo na kuleta maumivu kwake.   

Wataalamu wa sayansi ya mapenzi katika tafiti zao wanasema asilimia 35 ya wapendanao hugombana juu ya mambo yanayohusu fedha kila wiki na asilimia 10 ya wapendanao hukwazana juu ya mambo yanayohusu pesa karibu kila siku. Takwimu hizo zinakupa mwanga juu ya umuhimu wa kuangalia kwa makini juu ya eneo hili. Na kama takwimu hizo tungezibadilisha sura yake itatutisha na kuweza kufanya bidii katika mwenendo wetu juu ya pesa na tukasema asilimia 35 ya wapendanao huachana kila wiki kutokana na mambo ya pesa bado tungekuwa tunasema ukweli kwa asilimia fulani kwani ni kweli kwamba wapo watu ambao wameharibu ndoa zao kwa sababu ya pesa kidogo kuwepo kati yao au kuwepo kwa pesa kupita kiasi na mgogoro ukazuka juu ya nani atumie nyingi zaidi ya mwenzie na zitumikeje pesa hizo. Mara nyingi kutokana na kushindwa kupanga matumizi mazuri ya fedha watu wengine wamejikuta wakinunua penzi nje ya ndoa zao kuziba mapungufu yaliyomo katika ndoa zao.

Tafiti ya hivi karibuni inasema kuwa ni rahisi kutabiri ndoa itakayovunjika uonapo mke na mume ambao hawaelewani au kugombana katika mambo yanayohusisha fedha. Kiongozi wa utafiti huo Dr. Jeffrey Dew anasema kwa kuwa kila mtu ana mtazamo wake juu ya maeneo muhimu ya matumizi ya fedha .Na kutokana na umuhimu wa fedha  katika maisha yetu ni rahisi sana watu kushindwa kuelewana katika eneo hilo. Mshiriki mwingine katika utafiti huo Dr. Sonya Britt anasema sio tendo la ndoa, watoto au wakwe vinavyoongoza katika kuleta msukumo wa watu kuachana bali ni fedha na mambo yahusuyo fedha. Kwa wanaume imeonekana kuwa walijikuta wanataka kuachana na kuvunja ndoa juu ya masuala yahusuyo fedha pekee na kwa wanawake ilikuwa masuala ya fedha na tendo la ndoa jambo linalothibitisha hali ya wanawake walioolewa na wanaume wenye fedha nyingi kwenda nje ya ndoa. Pamoja na hayo bado ilionekana ili kuwa pale inapotokea ugomvi juu ya pesa watu hutumia maneno makali zaidi kuliko katika maeneo mengine. Jambo linaloweza kutengeneza uhasama kati ya wapendanao. Dr Jeffrey Dew anasema kuwa utafiti wao unaonyesha hoja ya wapendanao kutumia akili yao vizuri katika mambo yahusuyo fedha na umuhimu wa kukagua hisia na mitazamo tuliyonayo juu ya fedha na matumizi yake.
    
Labda nitoe mifano michache hapa,mwanaume anaombwa fedha ya maziwa ya mtoto wao wa mwaka mmoja na kwa kuwa anajua mke wake anafanya kazi anasema hana fedha akijua maziwa hayatakosekana kwani mke wake anao uwezo wa kununua.Inatokea jioni hiyo hiyo mwanaume huyo anaona watembeza viatu ananunua viatu vizuri sana ,je hapo mwanamke hatakasirika?Akikasirika na hasemi kitu na hapohapo sayansi inasema wanawake wengine wakikasirika hupatwa na hamu ya tendo la ndoa na mwanamke huyo akivamiwana hamu ya tendo la ndoa na akakumbuka JOHN alikuwa anamtaka kwa muda mrefu  si ataenda kwa JOHN na kumpa kuchikuchi? usaliti una vyanzo vingi na pesa inaweza kuwa kianzishi.Na angalia mwanamke anaemwambia mchumba wake kuwa hana pesa kabisa na anaomba msaada kwa mchumba wake lakini baadae anaonekana na gauni jipya kabisa na ni la bei mbaya huoni mchumba wake atafikiria vibaya? kuna mambo mengi yanayofanana na hayo kama vile mwenzio anakuomnba fedha na ukasema huna na akatokea ndugu yako akakuomba pesa ukampa hayo yote huleta maumivu makali kwani mtu anajiona kuwa hapendwi.

Ni kweli kuwa fedha haziwezi kununua penzi lakini huwezi kusema kuwa fedha sio muhimu katika ujenzi wa penzi. Katika historia ya wanadamu imeonekana wazi kuwa mara nyingi ukiwa na uwezo mkubwa wa kifedha imesaida mtu kupendwa na wengi zaidi. Ni vigumu kwa mtu kukubali kuwa hatojali kuwa na mtu asiekuwa na pesa lakini wengi wangefurahia kuwepo na pesa za kutosha katika penzi lao.

Utafiti uliofanyika na Chuo kikuu cha TEXAS huko Marekani unaonyesha kuwa kupungua kwa fedha katika uhusiano ulioanza katika mazingira ya kuwepo pesa nyingi husababisha watu wawili waliopendana kipindi cha kwanza kuachana kutokana na pesa kupungua. Hivyo inatokana kuwa pale ambapo inaonekana kuwa fedha hazitoshi kwa mahitaji yaliozoeleka au mahitaji yanayotamaniwa mikwaruzano kati ya watu wawili wapendanao huongezeka na kusababisha kutoridhika na uhusiano huo.Kutoridhika huko kutasababisha mikwaruzano na usaliti wa chini kwa chini.

Daktari mwingine aliefanya utafiti katika eneo Dr. Terri Orbuch anasema haijalishi watu wanapendana kiasi gani marumbano yanayohusu pesa hutingisha sana mahusinao hayo. Tafiti hiyo ya muda mrefu inaonyesha kuwa katika ndoa 10 ndoa 7 lazima zitakuwa na mizozo na mvutano katika eneo hilo na Dr. Terri anasema ndio maana watu wengi hukwepa kuzungumzia hisia zao juu ya jambo hilo. Pamoja na hilo pia imeonekana kutokana na ugumu wa kuzungumzia hisia za mtu juu ya swala hilo mtu anajikuta anamchukia mwenzie bila kumweleza kwani anamuona kama mzigo au anaona anatumiwa kama ATM ya Benki.

Haijalishi mtu ana fedha nyingi kiasi gani lazima atakuwa anafikiria juu ya kupungua na kuongezeka kwa fedha zake na zaidi  ya hayo angependelea kuwa fedha zake zinaongezeka hivyo atokeapo mtu ambae anasababisha zipungue lazima ataonekana kama tishio kwake.Hofu ya kupungua kwa fedha na aibu ya kutokuwa na fedha za kutosha zitasababisha misuguano ya hapa na pale.

Hisia juu ya fedha unaweza kuziona zinajitokeza kama ifuatavyo, iwapo unaogopa kuishiwa fedha hapo hapo unakuwa unaogopa kudharauliwa na kuachwa na hivyo hatua zako za kutaka kujilinda na hayo lazima zitaleta migongano.

Iwapo unajikuta huna fedha za kutosha kukidhi mahitaji ya mpenzi wako unajiona kuwa hufai kwani humtoshelezi mahitaji yake, hali hiyo huleta uchungu nafsini. Kwa kuwa hupendi uchungu huo ujulikana utajikuta unajawa na hasira wakati wowote pale fedha inapohitajika kwa matumizi Fulani na hasira hiyo italeta chachu kati yenu.

Utafiti uliofanywa na gazeti moja la SELF magazini miongoni mwa wanandoa 23,000 ilionekana kuwa asilimia 40 yao walisema uongo juu ya matumizi ya fedha zao. Kati ya wanandoa  hao asilimia 60 wanasema kuwa kushindwa kuwa mwaminifu kwenye matumizi ya fedha ni sawa na mtu kushindwa kuwa mwaminifu na kufanya mapenzi nje ya ndoa. Na kati ya watu hao 1/3 wamesema kuwa kutokuwa mwaminifu katika matumizi ya fedha humfanya mtu kuhalalisha uzinzi nje ya ndoa.

Fedha hazifanyi kazi ya kununua vitu au huduma peke yake, pesa zinaweza kusaidia mtu kuoneysha mapenzi, ubabe na uhuru pia jinsi gani mtu anapenda pesa zake zitumike ni uamuzi wake binafsi na hivyo pale ambapo mtu mwingine ana shiriki matumizi ya pesa zake uhuru wake kwa kutumia fedha hizo unaingiliwa na hivyo kama penzi la watu wawili halina mizizi mizito lazima mvutano wa aina fulani utatokea na isipotumika hekima migogoro itachipua kwa urahisi.

Kwa mfano  mpenzi wako anaomba umtumie shilingi 20,000 na yeye hajui umepangia nini fedha zako na wewe ili usionekana huna pesa unatoa kwa shingo upande. Angalia hivi juzi umempa shilingi 20,000 leo  unamwambia aje alale kwako unatoa visingizio hali hazuiliwi na wazazi  au mtu yeyote. Sisemi kuwa kwa kutoa shilingi 20,000 ndio amenunua penzi na lazima alipwe nasema angalia hisia za mtu huyu, na mfano huo huo ukigeuza utaona jinsi gani migogoro hutokea.

Ugeuze hivi leo mchumba wako wa kike kwa hiari yake mwenyewe kajitolea kuja kulala kwako akisema ana hamu na wewe na wewe ukafurahi sana lakini siku tatu zijazo akakuomba Tshs. 20,000 ulioipangia jambo fulani muhimu na ukamwambia sina dada huyo ataumia sana kwani anaona humpendi. Na kama utatoa pesa hiyo kwa shingo upande tayari umeathirika kisaikolojia.

Shida iliopo inatokana mtazamo wa mambo ya kifedha kati yenu. Unaweza kuona mtu analipia chakula hotel, chumba na hata kukupa hela ya nauli lakini ukimuomba Tshs 20,000 akakunyima unaona hakujali kikamilifu. Huoni kiasi gani anatumia   kwa starehe zenu na mawasiliano yenu pia hujui mipango mikubwa aliyonayo. Hebu angalia mfano huu huyu dada kabla hajapata kazi mchumba wake alijitolea gharama zake zote za saluni na chumba anachoishi na sasa dada huyo amepata kazi bado anataka mchumba wake aendelee kumlipia chumba alichopanga na gharama za saluni eti kw akuwa kaka huyo ana kipato kikubwa. 


Ludewa yetu na maendeleo yetu posted by barnabas njenjema, kutoka Ludewa
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: