UNAWEZA KUJILETEA FURAHA MAISHANI KWA NJIA HIZI TATU




Unataka maisha yenye furaha na amani ? Unataka mafanikio ? Je unao mkakati wa kufikia hayo ? Jibu ni rahisi sana kama unavyoenda kusoma makala hii. Tena jibu la maswali hayo lipo karibu kuliko unavyoweza kudhani, hata hivyo lina gharama kubwa, sio ya kifedha bali ya kisaikiolojia. Pengine itakugharimu mambo mengi ambayo ulidhani ni ya msingi. Ni gharama ya mabadiliko.
Kwanza tafakari sahihi ya maisha:
Kwanza kabisa, je na wewe ni mmoja wa watu "wanaotafuta" maisha ? Ni kawaida kuwasikia watu wakisema wanatafuta maisha. Hii ni dhana inayopotosha kufanya watu wengi waamini kuwa maisha ni kama kitu fulani kinachowezekana kufikiwa, yaani maisha ni dhana tofauti na wewe. Hapana, hauhitaji kutafuta maisha. Tayari unayo maisha, wewe ni sehemu ya maisha, kucheka kwako, kula kwako, kufanya kazi, kuwaza kwao, yote hayo ni sehemu ya maisha. Ukiwa na mtazamo wa "kutafuta" maisha unaweza kujikuta mtu usiye na furaha siku zote, mtu usiye makini na ulichonacho, na pia utashindwa kutambua uwezo wako mkubwa ulionao. 
Hivyo basi anza sasa kutambua kuwa tayari unayo maisha. Tafakari na jikumbushe siku zote uwezo ulionao -akili, marafiki, jamaa, mafanikio yako kielimu, mahusiano, biashara, n.k yote hayo ni "maisha" yako.
Faida ya kutambua kuwa tayari unayo "maisha" ni kuwa utaweza kuunganisha nguvu zako katika kufikia mambo mengine ya msingi, pia utatumia 'utajiri' ulionao kuweza kutimiza malengo mengine.

Kuta ulizojiwekea katika maisha:
Pili unatakiwa uondoe "kuta" ulizojiwekea wewe mwenyewe katika kupiga hatua zaidi za kimaisha. Soma vizuri, nimesema katika kupiga HATUA zaidi za KIMAISHA. Sio katika KUTAFUTA maisha. Kuta hizo ni kama vile uwoga wa kushindwa, Uwega wa Maumivu, Uvivu na Kujitegemeza kwa wengine.
Ni kweli ni mara ngapi umeweza kufanikiwa katika jambo ambalo hapo awali ulidhani usingeliweza ? Na je, ni wapi uliona mafanikio yamekuja bila kuwepo na mapungufu katika njia ya kufikia mafanikio hayo? Utajiuliza, sasa ikiwa makosa nitajaribu na kushindwa nitakuwa nimepoteza vingi sana, itakuwaje ? Swali hilo bado linadhibitisha kuwa unao uwoga. Amini kuwa baada ya kushindwa, kutatokea njia mbadala au utakuwa umejifunza zaidi ili usikosee tena. Swala la kuogopa hasara linakupa shida, ila kumbuka nafasi za kushindwa ni chache pia, na hata utakaposhindwa  utakuwa umejikusanyia uzoefu wa kushindana na kushindwa. Hivyo wakati mwingine hautoogopa, na pengine utaweza kupambana vema na kushindwa.
Ukuta wa kuogopa maumivu, inaendana na ukuta wa kuogopa kushindwa. Chukulia maumivu kama sehemu ya mafunzo na matayarisho ya FURAHA.
Uvivu ni adui yako mkubwa, hata hivyo pengine umemkaribisha na amekuwa kama sehemu ya wewe. Unachotakiwa kutambua ni kuwa ili mambo yafanyike ni lazima YAFANYIKE, hakuna cha ziada, hivyo basi FANYA, usiwe mtu wakusema NITAFANYA. Ni vema kuanza kidogo kidogo kuliko kusubiri majuto, ya kujiambia "ningejua".
Jambo lingine ambalo unafanya pengine kila siku ni kujishusha bila kukusudia. Mara ngapi ungeweza kujisomea ili kupata ufahamu fulani hata hivyo ukajiambia 'aah ntamuuliza fulani', mara ngapi ungeweza kujiwekea akiba ili kutimiza kusudio lako la kununua kitu fulani hata hivyo ukajisemea "aah ntamuomba fulani". Yaani hata haupati shida ya kujiuliza kama kweli hayo unayodhani wengine wafanye kwa ajili yako wewe mwenyewe unaweza kufanya. Hali hii ni pacha wa kufikia wa UVIVU.

Miliki Maisha Yako
Tatu jiunge katika ulimwengu wa msemo huu maarufu, yaani ni msemo maarufu katika kusemwa na watu kuliko jinsi wanavyouishi. Msemo huo ni "Miliki Maisha Yako, Ishi Maisha Yako".
Pengine hata wewe umewahi kuutumia tena bila hata kutafakari maana yake hasa ni nini, kwani utaishije maisha yako, wakati upo bize unayatafuta hayo maisha ? Si wewe peke yako, wengi wamekumbwa na hali hii kwakuwa tumefundishwa na kuaminishwa katika jamii zetu kutokuishi maisha yetu. Angalia matangazo ya biashara yanavyokuhamasisha kununua bidhaa fulani fulani. Angalia mfumo wetu wa elimu unavyoandaa watu kuwa wa aina fulani bila kujali kuwa tupo wa aina tofauti tofauti, tuna mahitaji tofauti na hata  uwezo tofauti wa kiakili, n.k
Hivyo unajikuta na wewe umekuwa wa kuiga, umejifunza kujikataa, umejifunza kutokuangalia nini hasa unataka, bali nini haswa marafiki, ndugu na jamaa wanataka au wanategemea wewe uwe vipi. Halafu ukiitafakari hali unaona ni kama vurugu kwani hakuna anayeishi maisha yake. Wewe nawe una mtoto wako au utakuwa na mtoto, tayari unawaza vile unavyotaka mtoto wako awe. Hali hii inakufanya uogope kuwa tofauti. Umetoa kafara mipango yako mingi, umeacha kufanya mengi ambayo pengine una uwezo nayo au ungependa kujifunza.
Ni wakati wako sasa wa kuanza kushinda hofu, kuondoa uvivu, kutambua kuwa unayo maisha, na kuanza kuishi. 
Kumbuka: "Wewe kujibandika Manyoya, hata kama ni mwili mzima, hakukufanyi uwe kuku".

Anza sasa kuondoa manyoya uliyojiweka na kufanya kweli katika maisha yako. UNAWEZA. Mafanikio yanakungoja...




Ludewa yetu na maendeleo yetu posted by barnabas njenjema, kutoka Ludewa
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: