KWANINI HATUFANIKIWI?
Kuna sababu nyingi ambazo huwafanya watu wasifanikiwe, zifuatazo ni baadhi tu;
· Kufuata mkumbo, watu wengi hawafanyi maamuzi yao na badala yake wanafuata maamuzi ya wengine na hivyo kutofanikiwa kwa mfano, mara nyingi tunasikia matangazo juu ya semina mbalimbali zenye fursa cha ajabu, mtu akishapewa mwaliko wa kuhudhuria, kwanza anauliza marafiki zake na ushauri anaopewa ni kuacha na hivyo kwenda disko. Je, disko na semina kipi kinaleta maendeleo katika maisha ya mtu?
· Kudharau fursa, kuna fursa nyingi sana ambazo kila kukicha zinatangazwa na zingine zinasogezwa kabisa kwa watu lakini watu hawashiriki wala kwenda kujifunza na bado wanalalamika hakuna ajira umaskini umezidi na hali ngumu ya maisha inazidi. Hata siku moja huwezi kufanikiwa kwa miujiza bila kufungua macho yako na kuona fursa na kuzifuatilia bila kuzidharau. Hii itakusaidia kujua faida na hasara zinazopatikana katika fursa husika.
· Ukosefu wa ndoto kubwa ya maisha, maisha yanayoongozwa na ndoto ndio yenye mafanikio kwani ni bora kufuata kile unachokiona kuliko kufuata usichokiona, ndoto ni kama picha iliyoakisiwa kutoka katika kitu halisi hivyo, ukiota unamiliki gari aina ya hammer au benz, na baada ya kutoka usingizini utatamani kukuta ndoto ni ya ukweli. Ukishatamani kumiliki gari ni rahisi sana kujituma ili kusudi kutimiza ndoto hiyo. Kuna watu hata siku moja hawajawahi kuwa na ndoto na wengine wanashindwa kufuatilia ndoto zao ili kuzifanya zitimie, mtu asiye na ndoto ni sawa na mwalimu anayeingia darasani kufundisha akiwa hajui anachotakiwa kufundisha.
· Uchaguzi usio sahihi wa njia ya utafutaji. Watu hawafanikiwi kwa sababu njia waliochagua kuitumia katika utafutaji inawanyonya na hivyo kuambulia hasara kila kukicha kwa mfano, utakuta mtu anaamua kufanya shughuli fulani kwa sababu tu amekosa cha kufanya. Watu wengi wanashindwa kufanikiwa kwa sababu kile wanachokifanya hawakiamini na hawakukichagua kwa malengo ya kuwaletea mafanikio bali kwa kusogezea siku tu kwa mategemeo ya kupata wanachokitaka siku zijazo na matokeo yake utakuta mtu amefanya shughuli fulani kwa miaka mingi pasipokuwa na mafanikio, hii ni kwa sababu kazi au shughuli ile inafanywa kwa malengo ya kusogeza siku tu.
· Utegemezi, watu wengi hasa vijana wanashindwa kujishughulisha na shughuli za utafutaji kwa sababu mategemeo yao au mahitaji yao yanapatikana kutoka kwa watu wengine kwa mfano, kuna vijana wenye umri taikribani 28 hajaoa na bado analishwa na wazazi na wengine wanaolea pale kwa wazazi na kuwategemea wazazi kwa kila kitu, kwa ujumla hajui shida na mawazo yake yote anadhani ataishi na wazazi miaka yote na wengine mawazo yao huenda mbali na kuwaza juu ya urithi wa mali za familia na kutamani wazazi wafariki ili wamiliki magari, mashamba , nyumba na mali zote za familia na matokeo yake tunasikia na kuona ndugu wanauana kwa kugombania mali za urithi. Hii hupelekea ndugu hao kufa masikini.
· Kukata tamaa, watu wengi hukata tamaa katika shughuli zao changa, hii hutokea pale mtu anapoanza shughuli au biashara fulani na kupata hasara au kukosa faida katik siku za mwanzo. Tulio wengi tunataka tukianza biashara leo asubuhi tupate faida leo jioni. Kwa jinsi mtoto anapozaliwa akiwa hawezi kukaa ndivyo biashara changa inavyokuwa, kadri mtoto anavyokua ndivyo anavyozidi kuchangamka vivyo hivyo biashara inavyozidi kukua ndivyo inavyochangamka na wateja wanaongezeka. Kukata tamaa ni dalili za kushindwa, amini kuwa usiku unapoingia, asubuhi inakuja.
· Kukosa imani katika shughuli, ukishaamua kufanya kazi au biashara fulani, ninaamini kuwa ni imani yako iliyokufanya uamue kuifanya, cha kujiuliza, ni nini hasa inachokufanya ukate tamaa? Imani yako inakuwa imekufa, inauawa na nini wakati mwanzo uliamini ni fursa ya kukuinua? Kufaulu na kushindwa ni matokeo yako mwenyewe na watu walisema, mchawi wa mafanikio yako ni wewe mwenyewe. Tunza imani yako juu ya kile unachokifanya.
· Kufanya shughuli bila malengo, malengo ni jambo muhimu sana katika harakati za kutafuta mafanikio kwani ni dira ya kukuonesha pale unapotaka kufika. Watu wengi wanafanya mambo yao kwa kuangalia wakati uliopo bila kufikiria baada ya muda fulani unataka shughuli yako iwe imefikia wapi. Kwa mfano, ukiwa unafanya kazi hotelini, jaribu kuweka malengo kuwa baada ya miaka miwili utakuwa unamiliki mgahawa wako ambapo pia utaweka malengo kuwa baada ya kumiliki mgahawa na hatimaye utamiliki na hotel yako baada ya miaka kadhaa, na hayo ndiyo matokeo ya kuwa na malengo. Ukweli ni kwamba, hadi mtu anakuwa tajiri mkubwa, kuna njia nyingi na magumu mengi anakuwa amepitia. Cha kushangaza wengi tunatamani kuwa kama wao pasipokuwa tayari kujishughulisha na fursa mbalimbali tuzipatazo, kwani ni wazi kabisa kila kukicha tunaona/ tunapata fursa nzuri za kutufanya matajiri lakini zinaonekana ngumu kwetu kutokana na kutobadilisha namna ya kufikiri kwetu (MTAZAMO).
Ludewa yetu na maendeleo yetu posted by barnabas njenjema, kutoka Ludewa
0 comments:
Post a Comment