Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya ziara yake ya kwanza nje ya nchi leo tarehe 06 April, 2016 kwa kutembelea nchi jirani ya Rwanda, ambapo yeye na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mheshimiwa Paul Kagame wamefungua Kituo cha Pamoja cha Utoaji wa Huduma za Mpakani (One Stop Border Post) na Daraja la Kimataifa la Mto Rusumo katika Mpaka wa Tanzania na Rwanda.
Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, ameingia nchini Rwanda kwa usafiri wa magari akitokea nyumbani kwake Lubambangwe, katika kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita ambako alikuwa mapumziko tangu tarehe 29 Machi, 2016.
Katika eneo la Rusumo, Rais Magufuli na Rais Kagame kwanza wamefungua majengo ya Kituo cha Pamoja cha Utoaji wa Huduma za Mpakani kilichopo upande wa Tanzania, kisha wakafungua daraja la mto Rusumo, na baadaye wakafungua Majengo ya Kituo cha Pamoja cha Utoaji wa Huduma za Mpakani kilichopo upande wa Rwanda.
Mradi huu wa ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha utoaji wa Huduma za Mpakani cha Rusumo, umehusisha ujenzi wa majengo ya mamlaka ya Mapato katika pande zote mbili na daraja lenye urefu wa mita 80 na upana wa mita 9.5, na umegharimu shilingi Bilioni 61.4 zilizotolewa kwa ufadhili wa serikali ya Japan kupitia shirika lake la JICA.
Akizungumza katika sherehe ya ufunguzi wa mradi huo Rais Magufuli ameishukuru Japan kwa kutoa fedha za kuwezesha utekelezaji wa mradi huo na ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Rwanda kupitisha mizigo yao Tanzania kupitia mpaka huo, pamoja na kuitumia bandari ya Dar es salaam.
Dkt. Magufuli amewasihi wananchi wa Rwanda na wanajumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla, kushirikiana kibiashara kwa kutumia fursa zilizopo huku akibainisha kuwa Tanzania imeanza juhudi za kuimarisha miundombinu yake ya barabara na kujenga reli ya kati, ambayo tayari washirika 13 wameonesha nia ya kufanikisha ujenzi huo.
Aidha, Rais Magufuli amewaonya maafisa forodha na vituo vya ukaguzi kuacha mara moja tabia ya ucheleweshaji wa upitishaji wa mizigo, na amesema serikali imeshaamua kuwa barabara ya Rusumo hadi Dar es salaam itakuwa na vituo vitatu ambavyo ni Rusahunga, Singida na Vigwaza ili magari yatumie muda wa siku 3 badala ya kutumia siku zaidi ya 10,
Kwa upande wake Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye ameongozana na mkewe Mama Janeth Kagame, pamoja na kuishukuru Japan kwa kufadhili mradi huo amesema Tanzania na Rwanda zina kila sababu ya kushirikiana kiuchumi na ameongeza kuwa ni matumaini yake kujengwa kituo hicho kutaongeza biashara na idadi ya watu wanaovuka daraja kutoka 2,000 wa sasa hadi watu zaidi ya 15,000 kwa siku.
Akiwa Rwanda Rais, Magufuli amefanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Paul Kagame na hapo Kesho Rais Magufuli atashiriki maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 22 ya mauaji wa Kimbari yaliyotokea mwaka 1994 ambapo watu takribani milioni 1,000,000 waliuawa.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Kigali
06 April, 2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame wakikata utepe kwa pamoja kuashiria uzinduzi rasmi wa daraja
la kimataifa la Rusumo na Kituo cha Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP)
cha Rusumo. Tukio hilo limehudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu
serkalini kutoka Nchi zote mbili, Mabalozi, na Viongozi wa Taasisi
mbambali za Kitaifa na Kimataifa.
Ujenzi
wa Daraja la Kimataifa la Rusumo na Kituo cha huduma Pamoja Mpakani
Rusumo ni moja ya miradi inayotekelezwa kwa msaada kutoka Serikali ya
Japan kwa Nchi za Tanzania na Rwanda kupitia shirika lake la maendeleo
la JICA.
Mradi huu kwa upande wa Tanzania umegharimu takribani kiasi cha TShs. 33,206,508,072.07 hadi kukamilika. Miradi mingine inayotekelezwa kwa kushirikiana na Serikali ya Japan kupitia JICA ni pamoja na ujenzi wa Barabara ya Arusha – Namanga, Iringa – Dodoma, Namtumbo – Kilimasera – Matemanga – Tunduru pamoja na barabara ya Masasi - Mangaka.
Mradi huu kwa upande wa Tanzania umegharimu takribani kiasi cha TShs. 33,206,508,072.07 hadi kukamilika. Miradi mingine inayotekelezwa kwa kushirikiana na Serikali ya Japan kupitia JICA ni pamoja na ujenzi wa Barabara ya Arusha – Namanga, Iringa – Dodoma, Namtumbo – Kilimasera – Matemanga – Tunduru pamoja na barabara ya Masasi - Mangaka.
Muonekano wa sehemu ya Daraja hilo la Rusumo
Jiwe la msingi lililowekwa baada ya uzinduzi wa daraja hilo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame wakipita kwenye Daraja hilo la Rusumo mara baada ya uzinduzi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame wakikata utepe kwa pamoja kuashiria uzinduzi
wa Kituo cha Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Rusumo. Tukio hilo
limehudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu serkalini kutoka Nchi zote
mbili, Mabalozi, na Viongozi wa Taasisi mbambali za Kitaifa na
Kimataifa.
Picha ya pamoja mara baada ya uzinduzi wa huo
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment