YONDAN AIPELEKA YANGA NUSU FAINALI




Yondan ameifungia bao la ushindi Yanga leo dhidi ya Ndanda

YANGA imekata tiketi ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) maarufu kama Kombe la Azam Sports Federations Cup baada ya kuilaza 2-1 Ndanda FC ya Mtwara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga walitangulia kupata bao lao dakika ya 27 kupitia kwa mshambuliaji wake, Paul Nonga aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na beki wa kulia Juma Abdul.
Adhabu hiyo ilitolewa baada ya kiungo na Nahodha wa Ndanda, Kiggi Makassy kumchezea faulo mshambuliaji wa Yanga, Mzimbabwe Donald Ngoma nje kidogo ya boksi.
Katika kipindi hicho, Yanga wangeweza kuondoka na mabao zaidi kama washambuliaji wake, wangekuwa makini hususan Nonga mwenyewe na mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, Simon Msuva.
Msuva alipewa pasi nzuri kwenye njia na Kamusoko dakika ya 34, lakini akagongesha mwamba wa juu, wakati Nonga naye alipewa pasi nzuri na Mzimbabwe huyo na wakati anajivuta kupiga shuti ndani ya boksi beki wa Ndanda, Paul Ngalema akaupitia mpira na kuondosha kwenye hatari.
Kipindi cha pili, Ndanda walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 56 kupitia kwa Nahodha wake, Kiggi Makassy kwa shuti la nje ya boksi baada ya kuwatoka mabeki wa Yanga.
Baada ya bao hilo, Yanga walicharuka na kufanikiwa kupata bao la ushindi lililofungwa na beki Kevin Patrick Yondan kwa penalti dakika ya 69, baada ya beki wa Ndanda, Paul Ngalema kumkwatua winga Simon Msuva ndani ya boksi.
Ngalema alionyeshwa kadi ya pili ya njano na refa Jimmy Fanuel kwa rafu hiyo na kutolewa nje kwa kadi nyekundu. 
Yondan alirudia kitendo cha Januari 27, mwaka huu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara alipofunga bao pekee kwa penalti pia katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Ndanda Uwanja huo huo wa Taifa, akimtungua kipa huyo huyo, Jeremiah Kasubi baada ya awali mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe kukosa penalti.
Yanga imeungana na Azam FC iliyoitoa Prisons ya Mbeya na Mwadui FC iliyoitoa Geota Gold kutinga Nusu Fainali. Nusu Fainali ya mwisho itachezwa Aprili 11, kati ya Simba SC na Coastal Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji Mngwali, Kevin Yondan/Nadir Haroub ‘Cannavaro’ dk84, Vincent Bossou, Pato Ngonyani/Salum Telela dk58, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Paul Nonga na Deus Kaseke/Godfrey Mwashiuya dk66.
Ndanda FC: Jeremiah Kasubi, Aziz Sibo, Paul Ngalema, Cassian Ponera, Salvatory Ntebe/Ahmed Msumi dk73, Hemed Khoja, William Lucian, Bryson Raphael, Omary Mponda/Salum Minely dk88, Atupele Green na Kiggi Makassy



Ludewa yetu na maendeleo yetu
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: