MAMBO HAYA KUMI(10) YANAWEZA KUOKOA MAHUSIANO AU NDOA YAKO




Katika pitapita nimekutana na hii mada hapa nikaona niwashirikishe na mwenzangu karibu upata hii elimu nawe hata kama wajua si mbaya kurudia.

Mahusiano sio jambo rahisi. Haishangazi kuona kwamba eneo la mahusiano ya binadamu, iwe ni kwenye ndoa, mapenzi, kazi, biashara na jamii ni mojawapo ya eneo linalopewa kipaumbele cha kila aina. Wataalamu wa saikolojia kila siku wanakesha wakijaribu kugundua mbinu mpya za kuboresha mahusiano ya binadamu.

Pamoja na “ugumu” wa mahusiano ya kibinadamu, yapo mambo kadhaa ambayo yanakubalika miongoni mwa wengi wetu kwamba yakifanyika kwa uwazi,upendo na bila hila, yanaweza kusaidia sana katika kuboresha mahusiano hayo. Haya hapa ni mambo 10 ambayo yanaweza sio tu kuboresha bali hata kuokoa mahusiano yako hususani mahusiano ya kimapenzi au ndoa.


1.Kuomba Msamaha (Samahani)- hakuna binadamu aliye kamili. Sote tuna mapungufu. Mapungufu hayo huja au kuwa dhahiri kwenye mahusiano na hata kwenye ndoa. Kuna kukosea. Kuna kumkosea mwenzako. Na mara nyingine unaweza kukosea kwa bahati mbaya tu bila kukusudia. Ukigundua kwamba mwenzako hajafurahishwa na ulichofanya au kutofanya, omba msamaha. Hata kama huelewi kwa undani kwanini mwenzako kakasirika au hata kama wewe unaona ni jambo dogo tu, omba msamaha.

2.Tumia Neno Tafadhali- Unapoomba kufanyiwa au kusaidiwa kitu, tumia neno tafadhali au naomba. Badala ya kusema Baba Nanihii, niletee maji ya kunywa,sema, “Baba nanihii tafadhali naomba niletee maji ya kunywa”. Ni maneno madogo tu lakini yanatosha kuonyesha heshima na upendo kwa mwenzako.

3. Sema Asante(Shukuru)- Kila unapopewa kitu, kufanyiwa jambo, kusifiwa nk onyesha upendo wako kwa kusema “Asante”. Usiposema asante usishangae siku nyingine usipopewa au kufanyiwa kitu fulani.

4. Mwambie mwenzako Unampenda- Anajua kwamba unampenda na pengine ndio maana yupo na wewe. Lakini hakikisha unamkumbusha. Usimchukulie poa tu. Hapana. Haya mwambie mwenzako unampenda sasa hivi.

5. Samehe na Sahau- Kama nilivyosema hapo juu, binadamu hatupo kamili. Tunakosea. Mara nyingine tunakosea kila mara na kwa jambo lile lile. Jifunze kusamehe na kusahau. Usisamehe kwa minajili ya kuzuga amani ili ulipize kisasi. Samehe na sahau. Usikumbushe yaliyopita. Jifunze kutokana na yaliyopita ila samehe na muombe Mungu usahau.

6 Ongea Lugha Ya Umoja Badala ya Umimi- Binadamu tu-wabinafsi. Ni hulka. Tunajiangalia sisi kwanza kabla ya kumwangalia mtu mwingine hata akiwa mpenzi, mume au mke. Lakini ukitaka mahusiano yadumu, ni muhimu kubadili “lugha”. Badala ya kuongelea mambo katika umimi, ongea katika wingi(sisi). Kwa mfano badala ya kusema,’ nyumba yangu au gari langu” (hususani kwa walio kwenye mahusiano ya ndoa) sema, “nyumba yetu na gari letu”. Hutopungukiwa kitu ila utaijaza akaunti yako ya mahusiano mema.

7. Muite kwa Jina Lake- Ushakwenda mahali kama benki vile ukasoma jina la mhudumu aliyepo mbele yako kupitia kitambulisho chake kisha ukamuita kwa jina? Uliona jinsi alivyokupa huduma nzuri zaidi? Binadamu (hususani wanaume) tunapenda kusikia majina yetu yakitajwa. Ni hulka. Hakikisha unamuita mwenzako kwa jina lake. Litumie katika mazungumzo ya kila siku na kila mara.

8. Sikiliza- Kuna nyakati mpenzi wako anachotaka ni sikio lako tu. Sikiliza kwa makini anachokuambia. Onyesha wazi kwamba unasikiliza. Epuka na tabia ya “kumsikiliza” mwenzako huku unachezea simu yako au unakodolea macho televisheni.

9. Mheshimu- Hili linaonekana kuwa la wazi, si ndio? Kwa bahati mbaya mahusiano mengi yanavunjika huku wanaoachana wakisema “kutoheshimiwa” ndio sababu kubwa ya wao kuamua kujitoa. Kila mtu ana jinsi yake ya kuona anaheshimiwa au kudhauraliwa. Kwa makini jaribu kujua mambo yanayomfanya mwenzako aone umemdharau au kutomheshimu. Ikiwezakana muulize. Msome. Kisha yaepuke kama ukoma.

10 Msaidie Mwenzako- Ni muhimu sana kusaidiana. Hata pale ambapo mwenzako hajaomba msaada, fikiria kama Ingekuwa wewe ungehitaji msaada? Kama ni ndio, basi msaidie. Kwa mfano, msaidie kupika, kufua, kusafisha gari, kununua mahitaji ya Nyumbani, kusafisha nyumba, kuvalisha watoto. Kila inapowezekana (na mara nyingi inawezekana) msaidie.
KILA LA KHERI WOTE


Ludewa yetu na maendeleo yetu
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: