Jambo Muhimu Kuzingatia Kabla Ya Kuwasaidia Wengine, Ili Msaada Wako Uwe Bora.




Unapopanda kwenye chombo cha usafiri kama ndege au meli, unashauriwa kwamba kama itatokea ajali, kabla hujawasaidia wengine ni muhimu ujipe msaada wewe mwenyewe kwanza. Kama kuna hewa ambayo mnataka kuvuta, na kuna mwingine hawezi kuvuta hewa ile yeye mwenyewe bila ya msaada wako, labda ni mtoto au mzee, basi utashauriwa wewe uvute hewa ya kutosha kwanza, ndipo umsaidie na mwingine kuvuta hewa.
Kwa hali ya kawaida unaweza kuona ni ubinafsi, kwa nini usianze na yule asiyeweza ndiyo ukaja kwako? Lakini ukweli ni kwamba ili wewe uweze kutoa msaada mzuri kwa mwingine, ni lazima wewe uwe sawa kwanza. Hivyo kama ni hewa ni vyema wewe ukawa umevuta kwanza, kabla hujamsaidia mwingine kuvuta. Kwa sababu kama hutavuta wewe kwanza, mtakufa wote kwa pamoja.
Sasa huu ndio uhalisia kwenye maisha yetu ya kila siku. Kama unataka kutoa msaada kwa watu wengine, hakikisha ya kwamba wewe tayari umeshajipa msaada muhimu. Hakikisha ya kwamba wewe umeshaweza kusimama na ndiyo uweze kumsimamisha mwingine. Kinyume na hapo wote mtashindwa kusaidiana na mtazidi kuangushana.
Kwenye jambo lolote ambalo ungependa litokee kwa wengine, ili maisha yao yawe bora sana, ni vyema likaanza kutokea kwako kwanza. Kwa sababu kwanza litaonesha mfano mzuri kwamba unajali na inawezekana na pili itatoa hamasa kwamba hata mwingine naye anaweza kufanya.
http://www.amkamtanzania.com/p/kuwa-tajiri.html 
Unataka kuwasaidia wengine kuwa na maisha bora, anza wewe kuwa na maisha bora, anza kujijengea misingi mizuri ya maisha yako na ifanyie kazi. Ona matokeo mazuri kwako na yatumie matokeo hayo kuwasaidia watu wengine na wao kuwa na maisha bora.
Kama unataka kuwasaidia watu waondoke kwenye umasikini, hakikisha kwanza wewe unaondoka kwenye umasikini. Kwa sababu msaada bora kabisa unaoweza kuwapa masikini ni wewe kutokuwa masikini. Kwa sababu hapa utawaonesha mbinu nzuri ambazo umetumia kutoka kwenye umasikini na kama na wao watazifuata basi mambo yao yatakuwa mazuri pia.
Chochote kinachoanzia kwako kinakuwa na nguvu kubwa kwa wengine kwa sababu wao wenyewe wameona ukifanya na hivyo na wao pia wataweza kufanya.
Na ni muhimu sana kujua hili kwa sababu mara nyingi hisia huwa zinatuzuia kufikiria vyema. Kama kwenye hali ya ajali ambapo unaweza kuona kumwokoa mwingine ni muhimu kuliko kujiokoa wewe, unaweza pia kuona kusaidia wengine ni muhimu kuliko kujipa msaada wewe. Unaweza kuwa na nia nzuri lakini nia hii ikapalekea wewe kuanguka kabisa na mwishowe ukashindwa hata kumsaidia yule ambaye ulikuwa na nia ya kumsaidia.
Hivyo unapoamua kuchukua hatua ya kumsaidia mtu mwingine, hakikisha hatua hiyo haikuangushi wewe kabisa, au haikufanyi wewe kuwa kwenye hali mbaya kuliko hata unayemsaidia na mwishowe ukashindwa kabisa kumsaidia. Hakikisha unatoa msaada bora kwako na kwa mwingine pia, hii ikiwa na maana msaada unaotoa haukurudishi wewe nyuma.
KITABU; Kurasa Za Maisha Ya Mafanikio, Toleo La Kwanza 2016.Lakini pia usitumie hiki kama sababu ya kuepuka kuwasaidia wengine. Kwa kujiambia kwamba kwa sababu mambo yangu bado hayajawa mazuri basi siwezi kusaidia mtu mpaka yawe mazuri. Muhimu ni wewe kuwa kwenye njia ya kujikomboa na kisha kuwashirikisha wengine kwenye njia hiyo ya ukombozi. Na kuhakikisha unawasaidia kwa njia ambayo haitakuangusha na wewe pia.
Unaweza kuwa na wakati mgumu kujua ni kiasi gani hasa cha msaada unahitaji kutoa, kwa maana ya kile ambacho kitamsaidia mwingine na wakati huo kutokukurudisha nyuma wewe. Katika wakati kama huu, jaribu kuweka hisia zako pembeni na fikiri kwa kina, kisha chukua hatua ambayo ni sahihi kwako na kwa mwingine pia. Ukiruhusu hisia zikutawale, utafanya maamuzi ambayo yatakuumiza sana wewe, na wakati huo pia kumuumiza yule ambaye ulijitoa kumsaidia.
Naamini umeondoka na kitu cha kwenda kufanyia kazi hapa, fanyia kazi ili uweze kuboresha maisha yako na ya wale wanaokuzunguka pia. Maisha bora yanaanza na wewe na kisha kuwafikia wengine kupitia wewe. Unapokuwa bora wewe, unafungua njia kwa wengine kuwa bora pia.
Nakutakia kila la kheri,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,



Ludewa yetu na maendeleo yetu
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: