Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Kiukweli nimekuwa nikiwashangaa baadhi ya mashabiki/wadau wa mpira ambao labda kwa kutofahamu vizuri mchezo, ama ni kwa kudharau na kujichukulia ni watu sawa na baadhi ya mastaa wa mpira wa miguu ambao wameshafanya mambo makubwa katika soka la Tanzania.
Unamkumbuka, Emmanuel Gabriel ‘Batistuta’? Huyu ni mshambulizi wa aina yake kuwahi kutokea Tanzania katika kipindi cha miaka hii 15. Kuanzia, Nazareth ya Njombe mwaka 2000, Gabriel alipata kusajiliwa na Simba SC mwaka uliofuata na kujijengea jina kubwa kutokana na uwezo wake wa kufunga magoli.
Akiwa na umbo la ki-straika, Gabriel alitamba nyakati hizo kwa ufungaji ‘stadi’ wa magoli ya vichwa. Hakuwa mzuri sana katika kukokota mpira kutokana na uzito wake katika miguu, lakini katika suala la kutumia nafasi anazotengenezewa bila shaka kwa wale wafuatiliaji wazuri wa mpira wa miguu nchini wakati huo walishuhudia mfungaji aliyekamilika.
Gabriel ndiye mfungaji bora wa muda wote katika mipambano ya ‘Dar es Salaam derby’ ambayo huzikutanisha klabu kubwa zaidi nchini za Simba na Yanga SC. Alifunga jumla ya mabao matano (sawa na Jerry Tegete) katika ushiriki wake wa michezo ya ‘Watani hao wa Jadi’.
Huyu ni mshambulizi ambaye naweza kusema alifuatiliwa sana na wachambuzi wa kimataifa mara baada ya kufunga goli pekee la Simba katika mchezo wa kwanza wa klabu bingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri jijini Dar es Salaam mwaka 2003 msimu ambao Simba ilifika hatua ya makundi ‘Ligi ya mabingwa Afrika’ baada ya kuwavua ubingwa Zamalek iliyokuwa pia mabingwa mara nyingi zaidi wa michuano hiyo (mara 5).
Gabriel atarejea tena uwanjani baada ya takribani miaka minne ya kuwa nje ya uwanja kwa kile alichosema kusumbuliwa na majeraha ya goti. Atajiunga na timu ya ligi daraja la kwanza ya Friend Rangers FC ya Magomeni jijni hapa katika mzunguko wa pili msimu huu.
Rangers ambayo inakusudia kupanda ligi kuu baada ya kuangushwa kwa fitna msimu uliopita inamsaini Gabriel kwa lengo la kutumia uzoefu wake kuisaidia timu hiyo kutimiza malengo yake ya kucheza ligi kuu msimu ujao.
Si Emma tu, klabu ya Panone FC ya Kilimanjaro yenyewe imemsaini mlinzi mahiri wa zamani wa kushoto, Ramadhani Wasso Ramadhani ambaye pia alikuwa sehemu ya kikosi kilichofanya vizuri mwaka 2003 sambamba na Gabriel katika timu ya Simba. Wasso, ni nani asiyempa heshima yake? Mrundi huyu alijitambulisha na kujijengea jina kuwa nchini kutokana na uwezo wake wa kupandisha mashambulizi, kuzuia na kupiga krosi.
Wachezaji hawa wawili ni mfano tu, lakini kuna wazoefu wengi ambao watarejea tena uwanjani na hatuna budi kuwaunga mkono kwa sababu kama wachezaji vijana wanakuwa na malengo watapata nafasi ya kujifunza, kupata ushauri, na hata jinsi ya kucheza mpira wa malengo kutoka wa ‘Ma-legend’ hawa ambao walifanya mambo makubwa sana wakati wao wakiwa vijana.
“Mchango wanao mkubwa Emanuel kachezea Friends fainali ya Magufuli Cup katupia 2 mechi ya fainali tumepata milioni saba na nusu”, anasema Herry Mzozo kocha wa Rangers ambaye anaamini kuwa Gabriel ni mchezaji ambaye anaweza kuwasaidia sana katika ufungaji. Jukumu ambalo tayari amelifanya katika baadhi ya mashindano akiichezea timu hiyo.
Kuna watu pia wanaponda urejeo wa wachezaji hao kwa madai kuwa wakati wao umepita bila kutazama uwezo wao wa sasa. Naamini Rangers itapata faida kwa usajili huu wa Gabriel na itakuwa hivyo pia kwa Panone hata kama wachezaji hao hawatacheza mara kwa mara.
“Tatizo Watanzania tunajua sana kuponda au kudharau na hii ndiyo inafanya hata katika vilabu vyetu mchezaji akicheza zaidi ya miaka 5 utasikia eti kazeeka bila kuangali uwezo wake na hii hutokea kwa wachezaji wanaopata umaarufu na kuwa super star katika vilabu vya Simba na Yanga. Anasema mlinzi wa kati wa zamani wa APR ya Rwanda, Yanga SC na timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Hamis Yusuph ‘Waziri wa Ulinzi’.
“Huwa najiuliza ni kwanini, sipati jibu wakati mwingine naishia kufikiria labda ni utendaji wao mzuri au kuwa katika timu kubwa . Naimani bado kuna wachezaji waliocheza nao na mpaka sasa bado wanacheza pia wanaonekana ni ‘poapoa’ tu sababu hawakucheza Simba au Yanga.
“Lakini tukumbuke na kufikiria uwepo wao kwenye hizo timu ni muhimu sana kiushauri, kiufundi na morali ya wachezaji itaongezeka kuona wapo na Gabriel au Wasso. Tupo nyuma yao uwezo wa wachezaji wa zamani tofauti na wasasa watafanya vizuri tu”.
Ludewa yetu na maendeleo yetu
0 comments:
Post a Comment