. JULIUS MTATIRO: NITAGOMBEA UBUNGE JIMBO LA SEGEREA – DAR ES SALAAM.

NITAGOMBEA UBUNGE JIMBO LA SEGEREA – DAR ES SALAAM. Ndugu zangu, kesho Jumatatu 09 Machi 2015 saa 4.00 asubuhi, nitachukua fomu ya kuwania ubunge katika jimbo la Segerea kama ambavyo taratibu za ndani ya chama changu zinaruhusu. Hakutakuwa na mbwembwe vifijo wala nderemo kwa sababu bado hatutajajua kwa hapa Dar Es Salaam jimbo gani litaachwa kwa chama gani au ikiwa wagombea wa vyama vyote vya UKAWA watakutanishwa na kupigiwa kura ya maoni, vyovyote vile iwavyo niko tayari kukabiliana na demokrasia ya ndani ya chama changu na hata ndani ya UKAWA. Hivi sasa nina umri wa miaka 32 tu lakini nikiwa nimepitia kila aina ya uzoefu wa kiuongozi, kisiasa n.k. Naamini kuwa nina uzoefu wa kutosha kuwavusha wana Segerea mahali ambako nimeishi kwa takribani miaka 12 huku shughuli zangu zote za ujasiriamali zikiwa jimboni humu. Ninalifahamu jimbo hili vizuri, watu wake, matatizo yao na changamoto zinazowakabili. Zaidi ya yote nina uwezo wa kushirikiana na wananchi tukioneshana njia ya kuzitatua changamoto hizi na wakati ukifika nitazieleza huku nikiweka wazi njia za kupita. Pamoja na kwamba nina elimu ya darasani ya kutosha, uzoefu wa uongozi usio na shaka na tabia na mienendo ya maadili huku nikiwapenda watu wa kila namna, natambua kuwa kazi ya kuwa mbunge ni zaidi ya hayo, inahitaji weledi, wepesi, staha na heshima, kujali, kuwa karibu na watu na kujitolea kwa hali na mali kuwapigania wale ambao haki zao na mahitaji yao yanacheleweshwa – kaliba ya namna hii imejengeka na sina shaka kuwa ninakidhi sifa na vigezo hivi vya nyongeza. Mimi ni muumini wa demokrasia, nitasaidia wagombea wote waliojitokeza kunipinga na kushindana nami ikiwa kutakuwa na haja hiyo, sitamtukana wala kumsema vibaya yeyote yule, kazi yangu kuelekea Oktoba ni kujinadi na kueleza sifa zangu na uwezo wangu huku nikivihusianisha na utatuzi wa matatizo ya wananchi wa Segerea kwa kushirikiana na wananchi. Nawaomba wanachama wengine wa vyama vya UKAWA wenye sifa, vigezo na uwezo wajitokeze kwa wingi. Sote tutapimwa kwa uwezo na vigezo vyetu na mwisho wa siku atapatikana mmoja wetu na ataungwa mkono na sisi sote. Baada ya Oktoba 2015, Segerea itakuwa na mpambanaji mpya, mbunge wa wananchi na atakayepigana hadi tone la mwisho la damu kwa ajili ya wananchi wake. Na labda mtu huyo atakuwa ni mimi. Nawatakia kila la heri Julius Mtatiro, +255 787 536 759, 0755 855 144, Juliusmtatiro@ yahoo.com
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: