UKATILI..!!! MTOTO ACHOMWA MOTO NA MAMA YAKE ETI KISA KULA NYAMA ZA SIKUKUU

Mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Ungindoni kata ya Mji Mwema Kigamboni, jijini Dar es Salaam (jina tunalihifadhi), anadaiwa kuchomwa moto na mama yake mkubwa sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kutumia jalo. Mtoto huyo alifanyiwa ukatili huo Desemba 25, mwaka jana akidaiwa kula vipande viwili vya nyama na hivyo kupewa adhabu na mama yake mkubwa, Rachel Bundala, kwa kuchomwa moto kwenye paja, goti na mikono yote miwili. SHUHUDA ASIMULIA Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Salima Salehe, alisema majirani walibaini kujeruhiwa kwa mtoto huyo baada ya kuitwa kutoka nje na kuonekana akichechemea na walipomhoji alieleza kuwa alifanyiwa ukatili huo na mama yake huku akiwaonyesha vidonda. “Kama mwanamke, niliumia sana na kuchukua jukumu la kumwambia Rachel kuwa kitendo alichokifanya hakikuwa kizuri, hivyo alipaswa kumpeleka mtoto hospitali kwa matibabu,” alisema. RAFIKI WA MTOTO AELEZA Shuhuda mwingine ni mtoto wa darasa la pili mwenye umri wa miaka minane (jina tunalihifadhi), ambaye ni rafiki wa mtoto huyo. Mtoto huyo alisema kuwa alimwona rafiki yake akiwa na majeraha mkononi na kumwuliza kilichomtokea na kujibiwa kuwa ameunguzwa moto. Alisema wakati rafiki yake huyo akimweleza mkasa uliompata, alimsihi iwe siri yake mama yake mkubwa asijue kuhofia akijua atafukuzwa nyumbani hapo. “Mimi kama mtoto mwenzangu, nimeumia sana kwa kitendo alichofanyiwa rafiki yangu, kwanza amefurahia Krismas akiwa na vidonda ambavyo havikutibiwa,” alieleza mtoto huyo. KAULI YA MWENYE NYUMBA Naye mmiliki wa nyumba anayoishi mama huyo, Kaunda Malale, ambaye pia ni mjumbe wa shina namba nane, alisema kwa muda wa siku tano alikuwa hajajulishwa tukio hilo hadi juzi alipoelezwa na wapangaji wake. “Baada ya kuelezwa na wapangaji wangu, nilikwenda kumuona mtoto huyo na kusikitika sana kwani hakupatiwa matibabu kabisa,” alisema. MTOTO ANENA Kwa upande wake, mtoto aliyejeruhiwa, akisimulia mkasa huo, alisema sababu kubwa ya kupigwa na mama yake mkubwa ilitokana na yeye kula nyama vipande viwili siku ya sikukuu ya Krismas. “Nilipigwa kwa kutumia mwiko nikaangukia kwenye jiko la moto, nimeumia sana,” alisema mtoto huyo bila kutoa maelezo zaidi. KAULI YA MTUHUMIWA Naye mtuhumiwa Rachel akizungumza na mwandishi wa habari hizi, alisema kuwa alichukua uamuzi wa kumpiga baada ya kubaini alikula mboga na alipoulizwa alikataa kufanya kitendo hicho. “Najua hiyo ilikuwa bahati mbaya kwani mara nyingi nilikuwa nikimweleza aache wizi bila kumpiga, lakini nimempiga mambo yamekuwa makubwa, lakini pia nakiri nilifanya kosa la kutompeleka hospitali kutibiwa,” alisema. Kufuatia tukio hilo, jirani yao, Joseph Mathias, alijitolea kwenda polisi kutoa taarifa na kupatiwa hati ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo yenye kumbukumbu MJ/RB/1976/2014. Alisema baada ya kupata hati hiyo, mtuhumiwa alikamatwa alfajiri na kufikishwa katika kituo kidogo cha polisi cha Mji Mwema kwa ajili ya kutoa maelezo ya utangulizi ili hatua za kisheria zichukuliwe. “Nimeumia baada ya kuona majeraha ya mtoto bila ya kutibiwa, kama mzazi ninapata shida kuona ukatili wa aina hii unaendelea kutokea. Nitamlea huyo hadi taasisi nyingine zitakapomsaidia,” alisema. MWENYEKITI WA MTAA Mwenyekiti wa mtaa wa Ungindoni (Chadema), Abed Ryoba, alisema tukio hilo ni la kusikitisha, hivyo serikali inapaswa kuchukua hatua za kisheria. “Sisi kama serikali ya mtaa, tunaendelea kujipanga kuona namna ambavyo mtoto huyo tutamsaidia huku taratibu nyingine zikiendelea,” alisema. POLISI WAZUNGUMZA Naye Mkuu wa Kituo kidogo cha Polisi Mji Mwema Kigamboni, Madei Mkupala, alisema kuwa tayari Jeshi la Polisi limetekeleza wajibu wake wa kumkamata mtuhumiwa na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria. “Tayari yupo katika mikono salama na maelezo yake yamekamilika, hivyo taratibu za kumfikisha mahakamani zikikamilika, atafikishwa mahakamani kwa kuwa kesi tayari imefunguliwa ya kujeruhi,” alisema. Na Leonce Zimbandu-Nipashe
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: