PADRI NA WATU WENGINE WAWILI WAFA WAKIOGELEA
Watu watatu wamekufa maji akiwamo Padri wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Same, Amedeus Mangia na wengine tisa kuokolewa baada ya kupigwa na dhoruba kali wakati wakiogelea kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu lililopo wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga, alisema kuwa tukio hilo limetokea juzi na kwamba watu wengine wawili waliopoteza maisha katika tukio hilo bado hawajatambuliwa majina yao.
Alisema walionusurika ni wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Chanjale kinachomilikiwa na Parokia ya Mtakatifu Stephen ya Same, ambao wote waliokolewa wakiwa hoi.
Ndemanga alisema siku ya tukio, wanafunzi hao wakiwa na mwalimu ambaye ni Padri Amedeus, walikwenda katika Bwawa la Nyumba ya Mungu kufanya hafla fupi ya kujipongeza kwa kuogelea na ghafla wakiwa majini, wimbi kubwa la maji liliwapiga na ndipo baadhi yao wakpoteza maisha.Watu walioshuhudia tukio hilo, walisema Padri Amedeus, kabla ya kufikwa na mauti hayo aliendesha ibada katika kanisa dogo lililopo eneo la bwawani Nyumba ya Mungu.
Baba mzazi wa padri huyo, Saimon Mangi, alisema mwanaye aliopolewa na wavuvi kutoka bwawani akiwa tayari ameshafariki.
MVUA YALETA MAAFA
Katika hatua nyingine, Ndemanga ambaye pia Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama katika wilaya yake, alisema kuwa mtoto ambaye bado hajafahamika jina, mkazi wa kijiji cha Tolowa wilayani hapa, alipoteza maisha baada ya kusombwa na mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kuonyesha wilayani humo na maeneo mengine mkoani Kilimanjaro.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Geofrey Kamwela, alipoulizwa alikiri pia kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa uchunguzi utakapokamilika taarifa zaidi zitatolewa kwa vyombo vya habari.
(CHANZO: NIPASHE)
0 comments:
Post a Comment