KUBADILISHA WAAMUZI, JULIO AWACHARUKIA TFF
Kocha wa Mwadui FC ya Shinyanga, inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amewavaa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kitendo cha kubadilisha waamuzi bila ya sababu za msingi.
Hayo yamekuja baada ya mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza kati ya Mwadui FC na Toto Africans uliopigwa juzi kubadilishwa waamuzi siku moja kabla ya mchezo huo, hivyo Julio kulichukulia hilo kama hujuma dhidi ya timu yake ingawa walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.
Julio amesema kuwa kitendo cha kubadilishwa waamuzi kimyakimya hakileti picha nzuri, hivyo wahusika wanatakiwa kulitazama hilo kwa jicho la tatu, alisisitiza kuwa TFF wasiwe na timu wanayotaka ipande badala yake waache kila timu ipande kwa uwezo wake.
“TFF ndiyo baba wa soka, kwa hiyo wahakikishe wanafuata kanuni na utaratibu wa kuongoza soka. Inakuwaje waamuzi wanabadilishwa siku moja kabla ya mchezo, tena usiku? Huoni hapa kama kuna ujanja-ujanja unajaribu kutengenezwa?
“TFF waliangalie sana hili, linaharibu mpira wetu. Waamuzi wale walibadilishwa kwa lengo lipi? Sisi hatujui. Wasitake kulazimisha timu fulani ipande, waache timu ipande kwa uwezo wake na si kubebwa-bebwa,” alifoka Julio.
Alipotafutwa Ofisa wa Ligi, Joel Balisidya, kwa njia ya simu kulizungumzia suala hilo jana Jumapili hakupatikana huku ofisi za bodi hiyo zikiwa zimepigwa kufuli..
Michezo yote kwa hisani ya salehe jembe
0 comments:
Post a Comment