KOPUNOVIC NI MWENDO WA MBIOMBIO

KOPUNOVIC NI MWENDO WA MBIOMBIO Na Saleh Ally TAYARI uongozi umefanya mazungumzo na Kocha Goran Kopunovic raia wa Serbia amekubali kuja nchini, anatua leo asubuhi tayari kwa ajili ya kuingia mkataba na mara moja kuanza kazi. Kopunovic ni mmoja wa makocha wenye jina kubwa nchini Rwanda, anatua Simba kuchukua nafasi ya Patrick Phiri ambaye kazi yake haijawa nzuri tokea ametua kwani katika mechi nane za Ligi Kuu Bara, ameshinda moja, sare sita na kupoteza moja. Simba wanataka mabadiliko, Kopunovic hawezi kuwa kila kitu lakini kuna mambo ambayo wachezaji, mashabiki na wadau wengine wa soka wayatarajie mara baada ya kutua nchini na kuanza kazi. Huenda kila kitu kisiwe bora katika kipindi kifupi, lakini Kopunovic ni kocha mwenye mambo mengi, mazuri na mengine yanakera, yeye ni binadamu pia. Uchezaji: Wakati anaingoza Polisi Rwanda kwa misimu miwili, ilisifika kwa kucheza kwa kasi, wachezaji wake walikimbia muda wote na sifa yake kubwa ni kuwa na kikosi chenye wachezaji wenye pumzi ya kutosha. Kutengeneza pumzi ya kutosha si jambo rahisi, lazima mazoezi makali. Kopunovic ni kocha anayependa kikosi chake kiwe fiti kwa kucheza kasi ya dakika 120 katika dakika 90, hivyo wachezaji wavivu wa mazoezi Simba, watakiona. Mafanikio: Hakuwahi kubeba ubingwa wa Rwanda, lakini aliisaidia Polisi kubadilika na kufikia kuwa tishio. Kwani kwa misimu mitatu aliyoifundisha, mmoja alishika nafasi ya tatu ukiwa ni wa kwanza kwake na miwili, yote alishika nafasi ya pili, nafasi ambayo ilikuwa ni aghalabu kwa kikosi hicho kuipata. Mara ya kwanza alishika nafasi ya pili nyuma ya APR waliokuwa wakinolewa na Ernie Brandts ambaye baadaye alikuja kuinoa Yanga. Msimu uliofuatia alishika tena nafasi hiyo nyuma ya Rayon Sports iliyokuwa inanolewa Didier Gomez raia wa Ufaransa. Kwa nafasi hizo mbili, ilikuwa ni mafanikio makubwa sana kwa Polisi ambayo awali haikuwa kwenye hadhi ya vigogo wawili, yaani Rayon Sports inayoongoza kwa mashabiki Rwanda na APR inayomilikiwa na jeshi. Pia aliingia fainali ya Kombe la Amani mara mbili dhidi ya APR, zote akapoteza kwa 4-2 na 2-1. Alipata nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho, lakini wakaishia raundi ya kwanza. Kubadili: Pamoja na kuwa na uwezo wa kukibadili kikosi chake kama atapewa nafasi ya kufanya kazi kwa uhakika, Kopunovic ana sifa ya kuwabadili wachezaji hadi kuwa hatari. Kwa wachezaji wasio wavivu ni rahisi kubadilika na kupanda kiwango kama ilivyokuwa kwa Meddy Kagere, Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda ambaye alikuwa tishio hadi kufikia Yanga kumtaka kwa udi na uvumba, lakini ikashindwa. Jazba: Hili ni tatizo lake kubwa, kuanzia kwa wachezaji wake hasa wale ambao hawamuelewi, lakini Goran si mvumilivu sana kwa marefa ambao wataonekana hawakitendei haki kikosi chake. Wakati fulani ukiwa ni msimu wake wa pili kuinoa Polisi, kidogo amtwange refa aliyekuwa akimtuhumu kuiuma Polisi katika mechi ya ligi ya nchini humo. Amekuwa mwepesi kuomba radhi kila baada ya kuboronga. Yanga: Anaijua Yanga kwa mambo mawili, kwanza ilimfunga mabao 2-1 katika mechi ya kirafiki kwenye Uwanja wa Nyamirambo mwaka 2012, baada ya kuwa imetwaa Kombe la Kagame, halafu ikafanya ziara hadi Kigali na kulipeleka Ikulu ya Rais Paul Kagame. Katika mechi hiyo iliyokuwa ya kasi ya juu, Yanga ikiwa chini ya Tom Saintfiet ilishinda kwa mabao hayo yaliyofungwa na Stefano Mwasyika na Hamis Kiiza. Pili anaijua Yanga kwa kuwa ilikubaliana naye aje kuifundisha, kila kitu kikawa kimeenda sawa, lakini katika hatua za mwisho kabisa, uongozi ukamtosa na nafasi yake kuchukuliwa na Brandts. Ingawa wajumbe wengi wa Yanga waliamini Kopunovic ni bora zaidi ya Brandts, lakini hoja ya vipi timu yake imeshika nafasi ya pili na Brandts amebeba ubingwa, ndiyo iliyoifanya Yanga ibadili mawazo hatua ya mwisho na kumtosa Mserbia huyo ambaye aliishapaki mabegi tayari kuja Dar. Kopunovic anatua nchini leo akitokea Hungary anakoishi, amezaliwa Februari Mosi, 1967 na alicheza soka la kulipwa katika nchi za Serbia, Hungary na Hispania. Alikuwa mmoja wa washambuliaji wakali na inaelezwa ana uwezo mkubwa wa kuwatengeneza washambuliaji na kuwa tishio
Share on Google Plus

About Rafiki Fm Ludewa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: